KWA MAONI AU USHAURI E-mail: inocomm2014@gmail.com, PIGA SIMU: 0714555668

www.utt-pid.org


TEMBELEA: www.utt-pid.org

October 2, 2014

UZINDUZI WA REDIO JAMII UVINZA

DSC_0177
Mkuu wa Wilaya ya Uvinza, Mwalimu Hadijah Nyembo (kulia), akitoa nasaha zake kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Luteni Kanali Mstaafu Issa Machibya (wa pili kulia), kuzungumza na wakazi wa Wilaya ya Uvinza, kwenye sherehe za uzinduzi wa kituo cha Redio jamii Uvinza FM mkoani Kigoma. Kutoka kushoto ni Meneja wa Huduma za Kijamii wa Airtel Tanzania, Hawa Bayumi, Mshauri na Mkufunzi kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), ambao ndio wadhamini wakuu wa Redio Uvinza FM, Bi. Rose Haji, Mwalimu na Mkurugenzi Mtendaji wa Uvinza FM Redio, Bi. Nuru Kalufya.

Na Mwandishi wetu, Uvinza – Kigoma

Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Luteni Kanali Mstaafu Issa Machibya amesisitiza uadilifu katika vyombo vya habari jamii kwa kutangaza habari zisizoumiza hisia kwa wananchi wengine na kuepuka migogoro.

Akizindua kituo cha redio jamii cha Uvinza FM, Luteni Kanali Mstaafu Machibya alisema kuwa vyombo vina wakati mgumu hasa katika kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu mwaka 2015.

“Changamoto hii inaweza kuepukika kwa kuhakikisha habari zinazotolewa zinalenga kuendeleza utamaduni wa amani, upendo, utulivu na uvumilivu na kuepuka viashiria vinavyoweza kusambaza chuki kwa lengo la kufanikisha chaguzi salama.

Mkuu wa Mkoa huyo amesisitiza umuhimu wa kuutumia uhuru wa kutoa na kupata habari vizuri kwa kusema kwamba uhuru huo usitumike kutoa habari zinazopendelea upande mmoja na kukandamiza mwingine kwa kuwa hali kama hiyo husababisha machafuko.

“Kwa mujibu wa Ibara ya 18 (b) ya Katiba ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, kila mtu anayo haki ya kutafuta, kupokea na kutoa habari bila ya kujali mipaka ya nchi, lakini haki hiyo iende sambamba kwa kuzingatia Sheria za nchi na kuhakikisha habari hizo haziumizi hisia za wananchi wengine,”
DSC_0206
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Luteni Kanali Mstaafu Issa Machibya, akisoma risala wakati wa uzinduzi wa kituo cha Redio Jamii, Uvinza FM, ambapo alilipongeza shirika la UNESCO kwa juhudi na kuwaweka karibu wananchi na serikali kupitia mawasiliano ya redio.

Luteni Kanali Mstaafu Issa Machibya, ameitaka redio jamii Uvinza kuonyesha uwezo wao ili waweze kujitangaza na kujijengea imani kwa wanajamii wao kuwa wanaweza. 

“Ni kwa hali hiyo tu mtaweza kujulikana, kutambulika na kupata udhamini na matangazo ya kutosha.”

Amewataka wanajamii kukitumia vyema kituo chao cha redio ili kiwe chachu ya kuleta na kukuza maendeleo katika vijiji, wilaya, mkoa na taifa kwa ujumla.

Wakati huo huo Mkuu wa Mkoa ameitaka redio jamii ya Uvinza kutangaza habari zenye kuonyesha madhara ya mila potofu na kujenga uelewa wa jamii kuhusu mila hizo hususan mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi (albino), kufichua wagonjwa wanaohofia kuwa na dalili za ugonjwa wa ebola na uharibifu wa mazingira.

Amelipongeza shirika la umoja wa mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) kwa kutoa msaada wa vifaa vya kituo hicho na kuendesha mafunzo ya kuwajengea uwezo wanahabari jamii, Kampuni ya simu za mkononi ya Airtel kwa kuruhusu matangazo ya Uvinza FM Redio yarushwe kupitia mnara wake na waanzilishi wa kituo hicho.
DSC_0264 
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Luteni Kanali Mstaafu Issa Machibya, akikata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa kituo cha redio jamii Uvinza FM, chini ya ufadhili wa Shirika la UNESCO na kampuni ya simu za mkononi ya Airtel Tanzania. Wanaoshuhudia tukio hilo kutoka kulia ni Meneja wa Huduma za Kijamii wa Airtel Tanzania, Hawa Bayumi, Mwalikishi wa Shirika la Kimataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), ambaye pia ni Mshauri na Mkufunzi wa redio jamii, Bi Rose Haji Mwalimu, pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Uvinza FM Radio Bi. Nuru Kalufya.
DSC_0285 
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Luteni Kanali Mstaafu Issa Machibya, akifanyiwa mahojiano mafupi ndani ya studio za redio jamii Uvinza FM na Mtangazaji wa kituo hicho, Kadisilaus Simon, mara baada ya kuzindua rasmi redio hiyo.

No comments:

Post a Comment