Mwenyekiti
wa askari wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) waliokosa ajira baada ya
mafunzo, George Mgoba (pichani), amedai kutekwa na kuteswa na watu wasiofahamika
huku wakimtaka kuwataja wanaowashinikiza kwenda Ikulu.
Akizungumza na NIPASHE Jumamosi katika mahojiano maalumu kwa njia
ya simu, mwenyekiti huyo ambaye amelazwa Hospitali ya Amana alisema
kuwa, Jumatatu ya wiki hii alipigiwa simu na mtu aliyejitambulisha kuwa
ni mmoja wa askari wa JKT ambaye alimtaka wakutane kituo cha mabasi cha
Mabibo.
Alisema alipofika kituoni hapo aliwakuta wanaume wawili na mwanamke
mmoja ambao baada ya kusalimiana kwa kupeana mikono mmoja wao
alimweleza kuwa, atoe mdudu kwenye sikio.
“Mkono ambao nilitoa kusalimiana nao ndiyo niliounyanyua kumtoa
mdudu niliyeelezwa cha ajabu ni kwamba baada ya tendo hilo nilipoteza
fahamu,” alisema na kuongeza:
“Nilipopata fahamu nilisikia mwangwi na nilipofungua macho niliona
nashushwa chini kwenye jengo la ghorofa, wakati tunakaribia kufika chini
nilisikia sauti ya redio call inaongea, lakini sikujua kilichokuwa
kikizungumzwa kwa sababu ilikuwa mbali,” alisema.
Mgoba alisema alisikia mmoja wa wale alioenda nao, wakiamuru redio
call hiyo izimwe na baada ya kufikishwa chini alifunikwa macho na
kitambaa cheusi.
“Waliniamuru nitoe simu na namba ya siri, lakini kwa sababu
walikuwa wameniziba macho na namba yangu ya siri ni ya kuchora
niliwaomba wanifungue kitambaa, walinitoa upande mmoja wa jicho
nikaifungua simu,” alisema.
Alisema alifunguliwa jicho moja na kuona buti la jeshi pamoja na
mwanamke mmoja ambaye alikuwa amesimama mbele yake ambaye hamfahamu.
Alisema watu hao walimbana wakimtaka aeleze anayewatuma kama ni Ukawa au Lowassa.
Pia alisema walimuuliza endapo watapata nafasi ya kwenda kwa Rais watamweleza nini.
“Wakati naulizwa maswali hayo walikuwa wananibana sehemu za siri
ili niseme ukweli ni Ukawa au Lowassa aliyetutuma kufanya hivyo,
niliwaeleza kuwa, lengo letu la kukutana na Rais ni kutaka kujua hatma
ya barua tunazomwandikia Kikwete na si vinginevyo,” alisema.
Mgoba alisema watu hao kwa kuwa walikuwa na lengo la kutana kujua
anayewatuma, waliendelea kumtesa kwa kumpiga fimbo mgongoni na
kumwingiza kichwa kwenye maji.
Alisema baada ya mateso hayo siku iliyofuata asubuhi, aliletwa mwanamke ambaye alitakiwa afanye nae mapenzi.
“Sikuweza kutekeleza hilo kwa sababu mwili ulikuwa hauna nguvu na
sehemu zangu za siri zilikuwa zinauma sana, wakati wakinishinikiza
nitekeleze hilo, alifika mtu mwingine ambaye ni kiongozi wao na kutaka
kujua walikofikia hivyo alielezwa,” alisema kuongeza:
“Aliwaamuru wanimalizie, nilinyolewa nywele wakataka kunipiga
sindano sikujua ilikuwa imewekwa nini lakini mshipa wa kichwani
haukuonekana hivyo wakakubaliana wanichome mkono wa kulia baada ya
kutekeleza hilo mwili ukafa ganzi,” alisema.
Mgoba alisema baada ya hapo, aliingizwa kwenye gari na kutelekezwa
kwenye moja ya mapori mkoani Pwani majira ya jioni ambapo alisikia mmoja
wao akiamuru simu yake ichukuliwe lakini hawakufanya hivyo.
Alisema baada ya kupata nguvu kidogo alijikokota hadi barabarani
ambapo huko alipita dereva wa pikipiki ambaye alimsaidia kumpeleka kituo
cha polisi cha Mkoa wa Pwani.
“Mmoja wa askari aliwasiliana na mkuu wa kituo hicho akimweleza
tukio langu na hali niliyokuwa nayo wakati huo, lakini mkuu huyo
alimjibu waniweke mahabusu, yule askari na wenzake nilisikia
wakishauriana kuhusu kauli ya mkubwa wao, wakakubaliana wanipeleke
Hospitali ya Tumbi kutokana na hali yangu,” alisema.
Alisema ndugu zake walipofika hospitalini aliwaeleza kuhusu sindano
aliyochomwa na kumuomba daktari mara baada ya vipimo wamchukue kwenda
Dar es Salaam kwa matibabu zaidi, ombi ambalo lilikubaliwa.
Alisema juzi asubuhi aliruhusiwa lakini katika hali isiyo ya
kawaida, polisi walimtaka arudishwe kituoni kwa maelezo zaidi na
walipofika walimng’ang’ania kuwa watampeleka hospitali wenyewe.
“Baada ya mvutano baina ya wazazi wangu na polisi, wazazi
walikasirika na kuondoka, hivyo polisi walinichukua kuja Dar es Salaam
hadi Kituo cha Polisi Kati badala ya hospitali,” alisema na kuongeza:
“Walinitaka niandike maelezo ambayo nilishindwa kutokana na hali
yangu kutokuwa nzuri, waliandika wao wanachokijua na kunitaka nisaini
nilikataa ndipo wakaniweka mahabusu,” alisema.
Alisema baada ya dakika kadhaa walimtoa na kumpa maelezo
waliyoandika ili ayasome ambayo baadhi ya vipengele kama vya kuwekwa
mahabusu vilikuwa havijawekwa.
“Niliwaomba waweke na hilo lakini walikataa na kunilazimisha
nisaini, nilitekeleza ndipo wakaniambia niandike barua ya kujidhamini na
waliniachia saa 3:00 usiku na kunipa Sh. 2,000 baada ya kuwaeleza sina
hela,” alisema.
Alisema baada ya kutembea kidogo alidondoka na alipozinduka
alijikuta hospitali ya Mnazi Mmoja ambapo baadaye alihamishiwa hospitali
ya Amana kwa matibabu zaidi.
Alisema tatizo linalomsumbua hivi sasa ni mwili kupata ganzi mara
kwa mara na maumivu makali sehemu za siri na kwenye majeraha ya vipigo.
Alisema kwa sasa daktari wake amempatia dawa ya kuondoa sumu ya sindano aliyochomwa.
Alisema simu yake ya mkononi, leseni ya udereva na kadi mbili za benki zinashikiliwa na jeshi la polisi mkoani Pwani.
Awali, akizungumza na gazeti hili, Parali Kiwango ambaye ni makamu
mwenyekiti wa askari hao, alisisitiza kuwa, lengo lao la kwenda Ikulu ni
kushinikiza kwa nini barua zao wanazomwandikia Rais hazimfikii na siyo
kwenda kudai ajira.
Kiwango na askari wenzake jana walikusanyika eneo la uwanja wa
mpira nje ya Shule ya Msingi Msimbazi Mseto na Mivinjeni, wakijadili
hatma ya mwenzao.
Katika mkutano huo watumishi kutoka Kituo cha Sheria na Haki za
Binadamu (LHRC) walifika kwa ajili ya kupata maelezo kuhusu tukio hilo
na baadaye walielekea hospitali ya Amana kwa mahojiano zaidi.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Pwani, Ulrich Matei, alipopigiwa simu
kuzungumzia tukio hilo alisema anashangaa kusikia cheo cha uwenyekiti
kwenye jeshi wakati cheo hicho hakipo.
Alisema mtu huyo aliokotwa barabarani na watu bila kuitaja
hospitali aliyopelekwa huku akimtaka mwandishi awasiliane na Kamanda wa
Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Camilius Wambura, kwa maelezo zaidi.
Kamanda Wambura alisema mtu huyo aliokotwa mkoa wa Pwani na kwamba
hafahamu chochote kuhusiana na tukio hilo huku akimtaka mwandishi
azungumze na kamanda wa mkoa wa Pwani.
Hata hivyo, alipoelezwa majibu ya kamanda wa mkoa wa Pwani, alisisitiza kuwa, tukio hilo lilitokea huko.
Naye, Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman
Kova, alisema wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo kwa sababu mhusika
alidai kutekwa eneo la Mabibo, utakapokamilika atazungumza na waandishi
wa habari.
CHANZO:
NIPASHE



No comments:
Post a Comment