| Waziri wa nchi (Ofisi ya Rais) Mahusiano na Uratibu, Mhe. Dkt. Mary Nagu (Kulia) akizungumza na Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Dkt. Philip Mpango (Kushoto) wakati alipofanya ziara ya kujitambulisha kwa Tume ya Mipango. |
| Naibu Katibu Mtendaji (Biashara za Kimataifa na ya Kiuchumi), Bw. Paul Sangawe (Kushoto) akimkabidhi zawadi ya kitenge Waziri wa nchi (Ofisi ya Rais) Mahusiano na Uratibu, Mhe. Dkt. Mary Nagu alipofanya ziara ya kujitambulisha kwa Tume ya Mipango. Anayeshuhudia ni Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Dkt. Philip Mpango. |
| Waziri wa nchi (Ofisi ya Rais) Mahusiano na Uratibu, Mhe. Dkt. Mary Nagu akizungumza na watumishi na viongozi wa Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango (Hawapo pichani) wakati alipofanya ziara ya kujitambulisha kwa Tume ya Mipango. |
| Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Dkt. Philip Mpango (Kushoto) akiagana na Waziri wa nchi (Ofisi ya Rais) Mahusiano na Uratibu, Mhe. Dkt. Mary Nagu mara alipomaliza ziara yake ya kujitambulisha kwa Tume ya Mipango |
| Baadhi
ya watumishi wa Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango wakimsikiliza Waziri wa nchi
(Ofisi ya Rais) na Uratibu, Mhe. Dkt. Mary Nagu (Hayupo pichani) alipotembelea
na kujitambulisha Tume ya Mipango.
Na Saidi Mkabakuli
Waziri wa nchi (Ofisi ya
Rais) Mahusiano na Uratibu, Mhe. Dkt. Mary Nagu amefanya ziara ya
kujitambulisha kwa Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango ambayo ni moja taasisi
anazoziratibu.
Akizungumza wakati wa ziara
hiyo Dkt. Nagu alitoa wito kwa Tume ya Mipango ijielekeze katika kujibu changamoto kuu za kiuchumi
zinazowakabili watanzania kwa sasa ikiwemo umaskini miongoni kwa Watanzania
walioko vijijini, ukosefu wa wa viwanda
vya kuongeza thamani mazao hasa kipindi hiki Tanzania inapoelekea kwenye uchumi
wa gesi.
Dkt. Nagu aliasa Tume ya Mipango kufanya tafiti mbalimbali za kiuchumi na
kijamii zitakazotoa majibu ya changamoto hizo.
“Kwa kuwa moja ya majukumu ya Tume ya Mipango ni kuandaa mipango
ya maendeleo ya muda mrefu, kati na ile ya kila mwaka na pia kufanya tafiti
mbalimbali za kiuchumi na kijamii, napenda kusisitiza kuwa mipango
inayoandaliwa ijielekeze katika kujibu changamoto hizo kubwa zinazowakabili
wananchi wetu ili kuhakikisha kuwa tunafikia malengo ya Dira ya Taifa ya
Maendeleo 2025,” alisema Dkt. Nagu.
Kwa mujibu wa malengo makuu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025, serikali
imejipanga kuhakikisha maisha bora na mazuri kwa kila mtanzania, utawala bora
unaozingatia sheria, na kujenga uchumi imara, wa kisasa na ushindani.
Akizungumza wakati wa kumkaribisha Dkt. Nagu, Katibu Mtendaji
wa Tume ya Mipango, Dkt. Philip Mpango alisema kuwa majukumu ya msingi ya Tume ya Mipango ni kutoa dira na
mwongozo wa uchumi wa Taifa pamoja na kubuni sera za uchumi na mikakati ya
mipango ya maendeleo ya Taifa; usimamizi wa uchumi na kufanya utafiti katika
nyanja za uchumi na maendeleo ya jamii.
Dkt. Mpango aliongeza kuwa kwa sasa Tume ya Mipango inafanya
kazi ya kuratibu utekelezaji wa
Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2014/15 pamoja na uandaaji wa Mpango wa Maendeleo
wa Taifa 2015/16 na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa mwaka 2016/17.
“Vilevile, Tume ya Mipango
tumejidhatiti katika kuandaa Mpango wa
Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano 2016/17 – 2020/21 ambao utajikita katika
kuifikisha tanzania kuwa ni nchi ya viwanda,” alisema Dkt. Mpango.
Kwa mujibu wa Dkt. Mpango, tangu kuundwa upya kwa Tume ya
Mipango mwaka 2008, imefanikiwa kukamilisha kazi kubwa za kitaifa ikiwemo
kufanya mapitio ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025, kuandaa Mpango Elekezi wa
Miaka 15 (2011/12 – 2025/26 pamoja na kuandaa Mpango wa Kwanza wa Maendeleo wa
Miaka Mitano (2011/12 – 2015/16) na kuratibu utekelezaji wa Sera ya Taifa ya
Idadi ya Watu 2006.
Kazi nyingine ni pamoja na kuandaa Mipango ya Maendeleo
ya Taifa kila Mwaka, kuandaa mfumo wa ufuatiliaji na utekelezaji wa miradi ya
Matokeo Makubwa Sasa na kuratibu uanzishwaji wa President Delivery Bureau (PDB), Kuandaa Mwongozo wa Usimamizi wa Uwekezaji katika Sekta ya
Umma (Public Investiment Management - Operational Manual – PIM-OM), na kufanya
tafiti mbalimbali za kiuchumi na kijamii.
|


No comments:
Post a Comment