Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, ambaye ni miongoni mwa mawaziri
13 waliochukua fomu ya kuomba kuteuliwa kugombea urais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), jana alirejesha
fomu hiyo kimya kimya huku akikwepa kuzungumzia safari yake ya kusaka
wadhamini katika mikoa 23 aliyopita.
Magufuli aliyechukua fomu hiyo Juni 5, mwaka huu, Makao Makuu ya
CCM mjini Dodoma, zikiwa ni siku mbili tangu chama hicho kifungue
milango kwa wagombea urais kuchukua fomu.
Hata hivyo, Dk. Magufuli, hakuwahi kutangaza nia wala kuzungumza na
Watanzania kupitia vyombo vya habari kama walivyofanya makada wenzake
waliojitosa kutaka kumrithi Rais Jakaya Kikwete.
Tangu alipotangaza nia, Dk. Magufuli hajawahi kueleza vipaumbele
vyake iwapo atateuliwa na chama chake kugombea kiti hicho, wala
kujinasibu kama wagombea wenzake wanavyofanya kila mkoa waliopita kusaka
wadhamini na kisha kupewa fursa ya kuzungumza na wanachama wa CCM na
wananchi kwa ujumla. Akiwa Makao Makuu ya CCM mjini hapa, Waziri
Magufuli alikabidhi fomu yake kwa Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Bara), Rajab
Luhwavi, saa 4:10 asubuhi ikiwa na wadhamini 450 pekee.
Akikabidhi fomu hiyo, Waziri Magufuli alisema: “Nimezunguka katika
mikoa 23 ya nchi hii na nimepata wadhamini kwenye mikoa 15, kikanuni
inapaswa kuwa hivyo lakini nina ziada ya wadhamini kutoka mikoa ya
Tabora, Geita, Mwanza, Kilimanjaro, Mtwara, Mara, Iringa, Pemba na
Unguja. Mkitaka niwakabidhi pia kuonyesha ninavyokubalika nitawapa,”
alisema na kuongeza: “Mheshimiwa huko kote nilikokwenda nilikuwa natumia
ramani ambayo inaonyesha nimepita wapi na wapi? Nimekuja nayo naomba
nikukabidhi Mheshimiwa Naibu Katibu Mkuu Bara.” Alipomaliza aligoma
kuzungumza na vyombo vya habari na kuondoka.


No comments:
Post a Comment