Dar es Salaam. Klabu ya Majimaji ya Songea imejiunga na klabu nyingine za Ligi Kuu kuajiri kocha kutoka nje ya Afrika.
Klabu
hiyo imemwajiri kocha kutoka Finland, Mika Lonnstrom aliyetua nchini
juzi usiku na kuahidi kuifanyia makubwa timu hiyo maarufu, Wanalizombe.
Mika (41) ambaye alipokewa na mwenyeji wake, Makamu Mwenyekiti wa Majimaji, John Nchimbi alipelekwa katika Hoteli ya Sea Cliff.
Gharama
za kulala katika hoteli hiyo ya kitalii ni Dola 250 (Sh500,000) kwa
siku. Kocha huyo ataishi hotelini hapo kwa siku tatu, sawa na Sh1.5
milioni na leo alitarajiwa kwenda Songea, Ruvuma kwa ndege tayari kuanza
maandalizi yake ya msimu mpya wa Ligi Kuu.
Majimaji
inayodhaminiwa na Kampuni Symbion, imesaini mkataba wa mwaka moja na
kocha huyo mwenye vyeti vya Shirikisho la Soka Ulaya (Uefa), leseni A.
Akizungumza
na mwandishi wetu, Mika ambaye uongozi umemtambulisha kama mkurugenzi
wa benchi la ufundi, lakini ipo wazi ndiye atakayekuwa kocha mkuu,
alisema: “Nimekuja Majimaji kwa lengo la kuifanya iwe timu ya ushindani.
“Nimefuatilia
na kugundua kuwa ilikuwa timu kubwa na maarufu hapo zamani, lakini
ikashuka, mimi nataka kuirudisha kwenye heshima yake.”
Kwa
upande wa Nchimbi, alisema: “Tumeamua kumleta Mika kwa ajili ya
kuboresha timu yetu, yeye ni mgeni amefundisha timu mbalimbali na
maelezo yake binafsi yameonyesha ni mzuri kiufundi na ataisaidia timu
yetu.”
Aliongeza: “Pia imekuwa kawaida kwa wachezaji
wetu, wanapokuwa na kocha wa kigeni, nidhamu inakuwa juu tofauti na
wanapofundishwa na kocha mzawa.”
Aliyekuwa kocha wa klabu hiyo, Hassan Banyai ataendelea na ajira yake ya ukocha kama kawaida.
Mika
amewahi kufundisha soka Wales, Finland na Thailand akiwa na klabu za
Roi Eti United FC, Gulf Saraburi FC na Police United FC, zote za Ligi
Kuu.
No comments:
Post a Comment