| Naibu Waziri
wa Kilimo, Mifugo, na Uvuvi, Mhe. William Ole Nasha (Kulia) akizungumza na Mwenyekiti
wa Baraza la Kilimo Tanzania, Dkt. Sinare Yusuf Sinare (Kushoto) na Mkurugenzi Mwendeshaji
wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), Bw. Thomas Samkyi (Wapili Kushoto) wakati wa Warsha ya
Kitaifa ya Wadau ya Sekta ya Kilimo inayofanyika katika Hoteli ya Blue Pearl,
jijini Dar es Salaam.
Na
Mwandishi wetu,
Benki ya
Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imedhamiria kusaidia upatikanaji wa Masoko ili
kuongeza Mapinduzi yenye tija katika Sekta ya Kilimo nchini ili kuchagiza na
kusaidia kuwezesha Sekta ya Kilimo kutoka kilimo cha kujikimu kwenda kilimo cha
kibiashara ili kukuza uchumi na kupunguza umaskini nchini.
Akizungumzia
katika Warsha ya Kitaifa ya Wadau ya Sekta ya Kilimo inayofanyika katika Hoteli
ya Blue Pearl, jijini Dar es Salaam, yenye Mada Kuu ya Warsha hiyo, “Wazalishaji
Tuanze na Soko, Mkurugenzi Mwendeshaji wa TADB, Bw. Thomas Samkyi
amesema kuwa ukosefu wa masoko ya mazao unaowakabili wakulima umekuwa ni
moja ya changamoto kuu zinazorudisha nyuma maendeleo ya sekta ya kilimo nchini.
Bw. Samkyi
amesema kuwa ili kusaidia kutokomeza changamoto hiyo na nyinginezo Serikali iliamua
kuanzisha TADB ili kusaidia kukabiliana na mapungufu hayo na kuhuisha
upatikanaji wa mikopo na masoko katika sekta ya kilimo ili kuleta mapinduzi katika
kilimo nchini.
“Katika
kutekeleza majukumu yetu Benki ya
Maendeleo ya Kilimo Tanzania imeanza huduma zake kwa kulenga minyororo michache
ya ongezeko la thamani katika kilimo ambapo mikopo ya aina mbalimbali hutolewa kuwezesha wakulima
kuongeza tija na uzalishaji katika sekta ya kilimo nchini Tanzania,” alisema
Bw. Samkyi.
Kwa mujibu wa Bw. Samkyi, Benki inatoa
mikopo kwa ajili ya uwekezaji kwenye
ujenzi viwanda vya kusindika mazao, ununuzi wa mitambo na ufungaji wa
mitambo ya usindikaji wa mahindi na kuongeza thamani, ununuzi
wa vifaa vya uvunaji wa kisasa wa mahindi, vifungashio vya kisasa vya
kuhifadhia mahindi na teknolojia ya uhifadhi wa mahindi kupunguza upotevu wa mazao.
“Kwa
sasa tumejikita katika mnyororo mzima wa uongezaji wa thamani kuanzia uandaaji
wa shamban hadi kwa upatikanaji wa masoko, ikiwemo mahitaji ya uzalishaji wenye tija kwenye sekta nzima
ya kilimo kuanzia hatua za awali za utayarishaji wa mashamba, kupima ubora wa
udongo na virutubisho vinavyohitajika kwenye uzalishaji wa mahindi, upatikanaji
wa pembejeo za kilimo zikiwemo mbegu bora, mbolea, madawa na vifaa na
teknolojia mbali mbali za umwagiliaji na fedha kwa ajili ya kulipia gharama
mbalimbali za uzalishaji wa mahindi,” aliongeza.
Mkurugenzi
Samkyi, ameongeza kuwa Benki imejipanga kutoa mikopo ya ununuzo wa mitambo na
mashine za ukaushaji, usafishaji na uchambuzi wa madaraja ya mahindi pamoja na
mitambo ya usindikaji na usagaji wa nafaka na ujenzi wa viwanda vya kusindikia
mazao ikiwamo fedha kwa ajili ya kulipia gharama mbalimbali za uendeshaji
katika kuongeza thamani ya mazao
Pia,
Benki inatoa mikopo kwa ajili ya ujenzi
na uboreshaji wa miundombinu ya kilimo katika kuimarisha minyororo ya
thamani katika kilimo ambapo inajumuisha ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji
na mitambo ya umwagiliaji, uchimbaji wa visima vya maji ya umwagiliaji, ujenzi
wa mabawa ya uvunaji maji ya mvua, ujenzi wa maghala bora ya kuhifadhia mahindi
na ujenzi wa miundombinu ya masoko.
Akizungumzia aina
ya mikopo itolewayo na benki hiyo, Mkurugenzi wa Biashara na Mikopo Bw. Robert
Pascal amesema kuwa Benki inatoa mikopo ya aina tatu ambayo ni Mikopo ya muda mfupi (Short term loans), mikopo hii ni ya muda mfupi
usiozidi miaka miwili (au miezi 24), Mikopo
ya muda wa kati (Medium term loan), mikopo ya muda wa kati hutolewa kwa kipindi cha miaka
2 hadi 5 (yaani kati ya miezi 24 na 60) na Mikopo ya muda mrefu, mikopo hii hutolewa kwa ajili ya kugharamia
shughuli za uwekezaji mkubwa kwenye kilimo na ambazo marejesho yake yatafanyika
katika kipindi cha miezi 60 hadi 180 (yaani kati ya miaka 5 hadi 15).
Bw. Pascal
ameongeza kuwa riba itozwayo kwa upande wa Mikopo
ya muda mfupi (Short term loans) ni riba ya asilimia saba (7%)
mpaka (8%) kwa mwaka. Ambapo mikopo hii Hutolewa kwa ajili ya kufanikisha
shughuli za kilimo kwenye mnyororo wa thamani. Kwa mfano, kugharamia shughuli
za kilimo zinazofanywa kabla ya mazao kuvunwa, na mara baada ya kuvunwa,
ununuzi wa mazao, ununuzi wa zana na mashine za kilimo na mahitaji mengine ya
kifedha katika mnyororo wa thamani.
Ameongeza kuwa mikopo
ya muda wa kati hutolewa kwa kipindi cha miaka 2 hadi 5 (yaani kati ya miezi 24
na 60) na hutozwa riba ya asilimia tisa (9%) mpaka (10%) kwa mwaka. Na mikopo
hii hutolewa ili kufanikisha mahitaji maalumu, mathalani: kupanua
mashamba, kuzalisha aina mpya za
mbegu, mifugo, na samaki na kuongeza kiwango cha rasilimali au uwekezaji,
kuboresha miundombinu, pamoja na kuziba pengo la mahitaji mengine ya muda wa kati
kwenye mnyororo wa thamani.
Na kwa upande wa Mikopo ya muda mrefu hutozwa riba ya asilimia
kumi na moja (11%) mpaka (12%). Mikopo hii hutolewa kugharamia mahitaji ya muda
mrefu, mathalani: gharama za kupata rasilimali, kujenga miundombinu mikubwa ya
kilimo, kupanua mashamba makubwa na ya kati, pamoja na shughuli nyingine
za kilimo zinazohitaji mikopo ya muda
mrefu. Mikopo ya muda mrefu inalenga kufanikisha uwekezaji kwenye miradi ya
kilimo, ufugaji, uvuvi na mahitaji mengine ya muda mrefu.
“Mikopo hii
hutolewa kwa ajili ya kujenga/kukarabati miundombinu katika sekta ya kilimo
kwenye mnyororo wa thamani, kwa mfano: skimu/mifumo ya umwagiliaji, maghala ya
kisasa ya kuhifadhia mazao, pamoja na mahitaji mengine ya miundombinu ya kilimo,”
aliongeza Bw. Pascal.
TADB ilianzishwa
kwa Sheria Namba 5 ya mwaka 2006 inayosimamia Benki na Taasisi za Fedha, pamoja
na Kanuni za Uanzishaji wa Benki na Taasisi za Fedha (Development Finance) za
mwaka 2012. Lengo la msingi la kuanzishwa kwa TADB ni kutoa mikopo ya muda
mfupi, kati na muda mrefu kwa sekta ya kilimo ili kuleta mapinduzi ya kilimo
nchini.
|
No comments:
Post a Comment