KWA MAONI AU USHAURI E-mail: inocomm2014@gmail.com, PIGA SIMU: 0714555668

www.utt-pid.org


TEMBELEA: www.utt-pid.org

September 26, 2016

MBUNGE BONNAH KALUWA ACHANGISHA MILIONI 13.7 UNUNUZI WA ENEO LA KITUO CHA YATIMA

Mbunge wa Jimbo la Segerea, Mh. Bonnah Kaluwa ameongoza harambee ya uchangishaji wa fedha za kununua eneo la kituo cha kutoa huduma kwa watoto wanaoishi katika mazingira magumu eneo la Tegeta, harambee iliyoendeshwa na  CVC Deliverance Centre Victorius Church (CVC), chini ya Kiongozi Mkuu Mchungaji Jehu Mkono.
Harambee hiyo ilifanyika katika Kanisa la CVC Deliverance Centre Victorius Tegeta kwa Ndevu, jijini Dar es Salaam, ambapo Mh. Bonnah Kaluwa alikuwa mgeni rasmi na kufanikiwa kukusanya kiasi cha fedha shilingi 13,730,000 ambazo zilipatikana kwa ahadi, michango ya waumini, wageni waalikwa na kufanyika kwa mnada ulionadi vitu mbalimbali.
Katika harambee hiyo Mbunge, Mh. Kaluwa alitoa shilingi milioni mbili yeye pamoja na mumewe huku akiendesha mnada uliotunisha mfuko wa kununua eneo la kituo hicho. Awali akizungumza katika harambee hiyo Mwenyekiti wa umoja wa akinamama wa CVC, Rose Haji Mwalimu alisema harambee hiyo itawezesha kupatikana kwa fedha za kununua eneo la kituo pamoja na upanuzi wa kanisa la CVC eneo la Tegeta mradi unaotarajia kutumia shilingi milioni 40.
Akizungumza wakati wa harambee hiyo, Mh. Kaluwa alimpongeza Kiongozi Mkuu wa CVC Deliverance Centre Victorius Church, Jehu Mkono kwa nia yake ya kuwasaidia watoto wanaoishi katika mazingira magumu kwa kuwajengea nyumba na kumuahidi yeye kama mwakilishi wa serikali atahakikisha analifikisha wazo hilo serikalini ili kuona jinsi gani serikali itamsaidia kutimiza malengo yake.
“Nikupongeze mtumishi kwa jambo ambalo umepanga kulifanya, mimi nitalifikisha wazo lako ili kama serikali tuone jinsi gani tunatoa mchango wetu na kuhakikisha mipango ambayo umeipanga ya kujenga nyumba kwa ajili ya watoto wanaoishi katika mazingira magumu wanapata nyumba ya kuishi,” alisema Mh. Kaluwa.
Mbali na kufundisha neno la Mungu, Kanisa la CVC Deliverance Centre Victorius limekuwa likitoa huduma za kijamii kwa kuhifadhi watoto wanaoishi katika mazingira magumu na watoto yatima ambao kwa namna moja au nyingine wamekuwa wakiishi katika mazingira hatarishi, kituo kikubwa kikiwa Mbeya kilicho na watoto 154.
unnamed-7
Kiongozi Mkuu wa CVC Deliverance Centre Victorius, Mchungaji Jehu Mkono (kulia) akishusha maombi kabla ya kuanza kwa harambee hiyo ya uchangishaji wa fedha za ujenzi wa kituo cha kutoa huduma kwa watoto wanaoishi katika mazingira magumu eneo la Tegeta.
unnamed-3
Mgeni rasmi Mbunge wa Jimbo la Segerea, Mh. Bonnah Kaluwa (wa pili kulia) akipeana mkono na Mwenyekiti wa umoja wa akinamama Kanisa la CVC Deliverance Centre, Rose Haji Mwalimu (kulia) mara baada kukabidhi risala ya harambee hiyo. Kushoto ni Hoyce Temu, ambaye ni mwanakamati wa harambee hiyo.
unnamed-5
Bishop Fedrick Ndonde ambaye ni rafiki wa karibu wa Kiongozi Mkuu wa CVC Deliverance Centre Victorius Church, Mchungaji Jehu Mkono akizungumza machache kabla ya kumkaribisha Mgeni rasmi Mbunge wa Jimbo la Segerea, Mh. Bonnah Kaluwa (hayupo pichani) kuzungumza na wageni waalikwa pamoja na waumini.
unnamed-1
Mgeni rasmi Mbunge wa Jimbo la Segerea, Mh. Bonnah Kaluwa akizungumza katika harambee ya kuchangisha fedha za ujenzi wa kituo cha kutoa huduma kwa watoto wanaoishi katika mazingira magumu eneo la Tegeta, harambee hiyo iliyoendeshwa na Kanisa la CVC Deliverance Centre Victorius, chini ya Kiongozi Mkuu wa kanisa la CVC Deliverance Centre, Mchungaji Jehu Mkono.
unnamed-12
Kiongozi Mkuu wa CVC Deliverance Centre Victorius Church, Mchungaji Jehu Mkono (katikati) akitoa ahadi yake mbele ya mgeni rasmi Mbunge wa Jimbo la Segerea, Mh. Bonnah Kaluwa (kulia).
unnamed-13
Mgeni rasmi Mbunge wa Jimbo la Segerea, Mh. Bonnah Kaluwa akiendesha mnada wa vitu mbalimbali kwenye harambee hiyo.

No comments:

Post a Comment