KWA MAONI AU USHAURI E-mail: inocomm2014@gmail.com, PIGA SIMU: 0714555668

www.utt-pid.org


TEMBELEA: www.utt-pid.org

December 7, 2016

WAZIRI MKUU ATAKA NYARAKA ZA FARU JOHN

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa ameugiza uongozi wa Mamlaka ya Hifadhi ya  Ngorongoro (NCAA), kumpelekea nyaraka zote zilizotumika katika kumhamisha faru maarufu kwa jina la John katika hifadhi hiyo ifikapo Desemba 8, 2016.

Majaliwa amesema ana taarifa kuwa walimhamisha Faru John Kreta kwa siri na kumpeleka  V I P Grumet  Serengeti Disemba 17, 2015 na waliahidiwa kupewa sh. milioni 200 ambapo  na wamepewa sh.  milioni 100 kwa ahadi ya kumaliziwa sh. milioni 100 nyingine baadaye.

Amesema hayo Desemba 6, 2016 alipotembelea Ofisi za makao makuu ya NCAA, zilizoko wilayani Ngorongoro mkoa Arusha  wakati akizungumza na watumishi wa mamlaka hiyo pamoja na Wajumbe wa  Baraza la Wafugaji ikiwa ni  sehemu ya ziara yake ya kikazi mkoani hapa.

“Naomba niletewe nyaraka zote zilizotumika kumuomba na kumuondoa faru huyo na barua zilizotumika kujadili suala la faru John. Nasikia amekufa naomba pembe ziletwe ofisini na iwapo itathibitika aliondoka bila ya kufuata taratibu wahusika wote watachukuliwa hatua kali za kisheria,”.

Aidha, Majaliwa amepiga marufuku tabia ya baadhi ya watumishi wa mamlaka hiyo ambao wanawakabidhi watoto kupeleka ng’ombe wao ndani ya kreta. “ Watumishi wa Ngorongoro ndiyo wanaopeleka ng’ombe ndani ya kreta na si wenyeji. Sasa marufuku na tutakayemkuta hatutakuwa na msamaha naye,”.

Amewataka watumishi hao kuhakikisha wanakuwa waadilifu na wanafanyakazi kwa kufuata misingi ya kiutumishi na kuacha tabia za kuendekeza rushwa na wizi.

Wakati huo huo Waziri Mkuu amemsimamisha kazi Mhasibu Mkuu wa NCAA, Sezzary Simfukwe kutokana na tuhuma za ubadhilifu wa fedha zinazomkabili na tayari  anahojiwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).

“Haiwezekani mtumishi  awe anachunguzwa  na TAKUKURU halafu aendelee kuwa ofisini si atavuruga uchunguzi. Asimamishwe kazi kuanzia leo mpaka hapo uchunguzi utakapokamilika na aikibainika kwamba hana hatia atarudi kazini,” alisema

No comments:

Post a Comment