NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar
kimewaahidi Wananchi wa Jimbo la Dimani na maeneo mengine nchini kuwa
kitasimamia Serikali Kuu Kuhakikisha inatekeleza kwa vitendo ahadi zote
walizoahidiwa wananchi hao.
Ahadi hiyo imetolewa na Katibu wa
Idara Maalum ya NEC, Itikadi na Uenezi Zanzibar wakati akitoa Pongezi
kwa Wafuasi wa CCM na Wananchi wa Jimbo la Dimani kupitia taarifa kwa
vyombo vya habari hapo Ofisi kwake Kisiwandui Zanzibar.
Alisema Chama hicho kimejengwa
katika misingi ya ukweli na uwazi katika utekelezaji wa ahadi zake kwa
umma hivyo ni lazima kiisimamie serikali kwa kuikumbusha utekelezaji wa
ahadi ambazo hazijafanyiwa kazi kwa baadhi ya maeneo.
Kupitia Taarifa hiyo aliwapongeza
kwa dhati Wanachama wa Chama hicho na wananchi kwa ujumla jimboni humo
kwa kuonyesha imani na mapenzi makubwa juu ya CCM hatua iliyofanikisha
ushindi kwa Juma Ali Juma aliyepata kura 4,860 na kumshinda mpinzani
wake kutoka CUF, Abdulrazak Khatib Ramadhan aliepata kura 1,234.
Katika Uchaguzi huo wapiga kura
walikuwa 6, 172 kati ya wapiga kura 9,275 waliojiandikisha katika
Daftari la Wapiga kura Jimboni humo.
Alisema ushindi wa mgombea wa
Chama hicho katika uchaguzi huo umekuwa mkubwa kuliko ule wa uchaguzi wa
mwaka 2015, ishara inayotoa matumaini ya kuwa wananchi wa jimbo hilo
wanaendelea kuiunga mkono CCM.
Aliwapongeza viongozi na
watumishi wa CCM Zanzibar kwa ngazi mbali mbali waliosaidia kwa njia
moja ama nyingine kufanikisha uchaguzi huo.
Pia alisifu juhudi zilizofanywa na
vyombo vya Ulinzi na Usalama katika kulinda Amani na Utulivu katika
maeneo yaliyofanyika Uchaguzi ndani ya jimbo hilo kuwa ni wajibu wao
kufanya hivyo lakini wamesaidia kulinda amani kwa ufanisi mkubwa.
Waride alisema ushindi huo
umetokana na sera na mipango endelevu vinavyotekelezwa na chama hicho
kwa vitendo katika maeneo mbali mbali nchini hasa katika Jimbo la
Dimani.
“ Siri ya ushindi wetu ni ukweli,
utu na kusimamia misingi ya haki bila ya ubaguzi vinavyofanywa na
viongozi wa CCM kwa kuwatumikia wananchi wetu bila ubaguzi.
Pia Mgombea wetu alikuwa na vigezo
vyote vya kuwa kiongozi wa jimbo hilo kutokana na sifa zake za utendaji
unaoambatana uadilifu katika kutekeleza ahadi anazotoa kwa jamii.”,
alifafanua Waride na kuwataka viongozi, watendaji na Wana CCM kuendelea
kujipanga kikamilifu katika Chaguzi zingine zijazo.
Aidha aliahidi kuwa CCM itasimamia
kikamilifu viongozi wake wanaotokana na ridhaa za Wananchi hasa
Wabunge, Wawakilishi na Madiwani ili waweze kutekeleza Ilani ya Uchaguzi
ya Chama hicho ya mwaka 2015/2020 kwa mujibu wa mahitaji halisi ya
wananchi.
Akizungumzia tathimini ya CCM
katika Uchaguzi huo alisema umefanyika katika mazingira yaliyokuwa huru
na Kidemokrasia kwa kuzingatia maelekezo na masharti ya NEC
yaliyotolewa kabla ya kuanza zoezi hilo.
Alisema licha ya kuwepo kwa kasoro
ndogo ndogo zilizoundwa na wafuasi wanaosadikiwa kuwa wa Chama Cha CUF
kwa nia ya kuvuruga uchaguzi huo kwa baadhi ya maeneo lakini Vyombo vya
ulinzi vimetekeleza wajibu bila kusababisha vurugu.
Uchaguzi huo uliofanyika Juzi kwa
lengo la kuziba nafasi ya Aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Dimani marehemu
Hafidh Ali Tahir aliyefariki akiwa mbungeni Dodoma mwaka jana, hatimaye
limepata mrithi wake kutoka ndani ya CCM.
|
January 23, 2017
CCM Z’BAR YAWAPONGEZA WANANCHI WA JIMBO LA DIMANI.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment