Na. Immaculate Makilika – MAELEZO
Mtandao wa Merriam Webster (2016)
umeelezea manufaa ya umma kama jambo ama kitu chenye manufaa kwa kila
mwanajumuiya ama jamii. Wakati nayo kamusi ya Encyclopedia Brtitannica
(2016) ikisema kuwa hili ni jambo lenye faida kwa jamii.
Nashawishika kusema kuwa vita hii
ya madawa ya kulevya ni ya kwa manufaa kwa umma, na hivyo hatuna budi
kuiunga mkono kwa akili na nguvu zetu zote.
Lakini pia kama ilivyo ada
maendeleo ya kitu chochote yanahitaji utashi wa kisiasa, uamuzi pamoja
na dhana ya uendelevu wa jambo, kwa mantiki hiyo vita ya madawa ya
kulevya ni lazima iwe na maendeleo kwa faida ya vizazi vya sasa na hata
vijavyo, hii si vita ya Rais Magufuli ,Makonda, wala Kamishna Sianga ni
ya watanzania wote.
Ni takribani siku kadhaa tangu
Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda aanzishe vuguvugu la kutaja
majina ya watu 65 wenye tuhuma mbalimbali kuhusu utumiaji, uuzaji na
usambazaji wa madawa ya kulevya na baadae Mheshimiwa Rais akasisitiza
mapambano dhidi ya madawa ya kulevya kwa kumteua Kamishna Mkuu wa
Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Madawa ya Kulevya Bw. Rogers Sianga.
Kamishna Sianga, hivi karibuni
akihojiwa na kituo cha televisheni cha Azam, anasema kuwa aina zote za
madawa ya kulevya zina madhara makubwa na Serikali haitasita kuendelea
kupiga marufuku ikiwa ni pamoja na kuwachukulia hatua wale wote
wanaojihusisha na biashara hiyo haramu nchini, japokuwa baadhi ya nchi
zinaruhusu matumizi ya dawa hizo.
“ Hatuwezi kuiga nchi jirani kwa
kuwa kuna madhara makubwa, mfano wagonjwa wengi wa akili katika
hospitali zetu wanatokana na matumizi ya madawa ya kulevya aina ya
bangi”, anasema Kamishna Sianga.
Ni dhahiri kuwa tunawaona ndugu
zetu, rafiki zetu na wasanii mbalimbali ambao wamekuwa waraibu wa madawa
ya kulevya, wakifikwa na maswaibu mbalimbali ambayo yaliyasabisha
kupoteza mwelekeo wa maisha yao na kusababisha vifo.
Athari hizi pia, zinaikumba
Serikali na Taifa kwa ujumla kwa kutumia fedha nyingi kwa ajili ya
kununua madawa aina ya methadone, pamoja na kuendesha proramu maalumu
kwa vijana kuhusu madhara ya matumizi ya madawa ya kulevya.
Ikumbukwe kwamba, Sheria mpya ya
Kupambana na Kudhibiti Dawa za Kulevya ya mwaka 2015, inaruhusu
kuwakamata waraibuni kuzungumza nao na kisha kuwapatia matibabu.
Lakini pia hatua hiyo inasaidia
Mamlaka zinazohusika kupata taarifa muhimu za waauzaji na wasambazaji wa
dawa hizo mitaani. Nadhani kitu pekee tunachotakiwa kufanya katika
kuunga mkono jitihada hizi ni kuwaripoti na kuwapeleka waraibu wa dawa
hizi hatari katika sehemu husika kwa lengo la kuwasaidia watu hao.
Aidha, Serikali imejitoa
kuwasaidia waraibu hawa kwa kuwatibu magonjwa mbalimbali ambayo mhusika
atakutwa nayo, yakiwemo magonjwa ya TB na Virusi vya Ukimwi. Hii ni
dhahiri kuwa serikali ina nia njema.
Mkazi wa Dar es Salaam, Antony
Shedrack ,mwenye umri wa miaka 23 anasema ametumia madawa kwa muda wa
miaka 6, na madhara aliyoyapata ni makubwa kwa vile hakuweza kumaliza
shule, hana kazi anayofanya na hivyo amekua tegemezi kwa ndugu na
marafiki.
Hali hii si ngeni kwa vijana
wengi wa kitanzania, kwa vile utumiaji wa madawa ya kulevya umekuwa
sehemu ya maisha yao kiasi ambacho wamepoteza mwelekeo na dira ya
maisha. Ili kulinda utu, heshima na kwa faida ya vizazi vijavyo na
ustawi wa taifa hili, ni lazima tuunge mkono vita dhidi ya madawa kwa
vile hii ni vita yetu sote na ni vita ya manufaa kwa umma.
|
February 22, 2017
VITA YA MADAWA YA KULEVYA NI YA MANUFAA KWA UMMA- MAKALA/MAONI
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment