KWA MAONI AU USHAURI E-mail: inocomm2014@gmail.com, PIGA SIMU: 0714555668

www.utt-pid.org


TEMBELEA: www.utt-pid.org

April 21, 2017

MAMA SALMA AMUULIZA WAZIRI MKUU KUHUSU UFISADI WA KOROSHO

Mbunge wa Kuteuliwa, Salma Kikwete (CCM), ameeleza kushangazwa kwa kitendo cha Serikali kukaa kimya juu ya ubadhirifu wa Sh bilioni 30 Bodi ya Korosho.

Mke huyo wa Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete, alitoa kauli hiyo bungeni jana wakati akiuliza swali la papo kwa hapo kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

“Umekuwapo ushahidi wa kutosha kabisa kuhusiana na wizi unaofanyika kwenye biashara ya korosho, hasa katika mikoa ya Mtwara na Lindi, ukiachilia mbali kazi iliyofanywa na Takukuru iliyobainisha kwamba kumekuwa na upotevu wa kiasi kikubwa cha fedha shilingi bilioni 30 kutoka Bodi ya Korosho.

“Serikali hatujasikia, mimi binafsi na wengine hawajasikia juu ya jambo hili. Je, Serikali leo inatuambia nini kuhusu ubadhirifu huu uliotokea hapa nchini kwetu, hasa wananchi wa Mtwara na Lindi kwa sababu jambo hili linaweza kutokea sehemu yoyote nchini mwetu,” alihoji.

Akijibu swali hilo, Majaliwa alisema mienendo ya vyama vya ushirika nchini imeonyesha si mizuri kwa kuonyesha upotevu wa fedha na inawakatisha tamaa wakulima.

“Mienendo ya vyama vyetu vya ushirika nchini vimeonesha si mizuri kwa kuonesha upotevu wa fedha na unakatisha tamaa wakulima wetu na Serikali inafanya mapitio ya vyama vyote na tumeanza na vyama vya ushirika wa kilimo.

“Tulikuwa na kikao Bagamoyo kwa ajili ya ubadhirifu huo wa bilioni 30 na Serikali iliunda timu maalumu na ikagundua kuwa ni hasara ya Sh bil 6 si bilioni 30 na haikusababishwa na bodi bali vyama vikuu na vyama vya ushirika vilivyopo kata na wilaya, vyama vya msingi na vyama vikuu na vyote vilifanyiwa uchunguzi na hatua zimeanza kuchukuliwa,” alisema.

Pamoja na majibu hayo ya Waziri Mkuu, Salma aliuliza swali la nyongeza akisema haijalishi ni kiasi gani cha fedha kimechukuliwa, lakini watalipwa lini.

“Haijalishi ni kiasi gani cha fedha kimechukuliwa, hizi bilioni sita na hizi ni haki za wananchi je, wananchi wanazipataje fedha hizo?” alihoji mbunge huyo.

No comments:

Post a Comment