KWA MAONI AU USHAURI E-mail: inocomm2014@gmail.com, PIGA SIMU: 0714555668

www.utt-pid.org


TEMBELEA: www.utt-pid.org

November 17, 2017

SPIKA NDUGAI AWATAKA MAWAZIRI KUACHA KUPIGA STORI BUNGENI

Spika wa Bunge, Job Ndugai amewaonya mawaziri kuacha kupiga stori wanapokuwa bungeni, badala yake wawe makini kusikiliza mijadala na maswali kutoka kwa wabunge.

Ndugai alitoa onyo hilo jana katika kipindi cha maswali na majibu baada ya kuwataja baadhi ya manaibu ili wajibu maswali lakini walishindwa kusimama kwa kuonyesha hawakusikiliza kilichokuwa kimeulizwa na wabunge.

“Waheshimiwa mawaziri acheni kupiga stori ndani ya Bunge, ndiyo maana mnashindwa kusikiliza kinachoendelea humu, hebu punguzeni na mjikite katika kusikiliza,” alisema Ndugai.

Kiongozi huyo alianza na naibu waziri wa Maji na Umwagiliaji, Jumaa Aweso ambaye alimtaka ajibu swali la nyongeza la Mwantumu Dau Haji (viti maalum - CCM) ambalo lililenga katika suala zima la upatikanaji wa maji kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji.

Kabla ya swali hilo, tayari mbunge huyo alishauliza swali la msingi ambalo lilielekezwa ofisi ya Makamu wa Rais na lilijibiwa na naibu waziri wa wizara hiyo, Kangi Lugola likihusu masuala la mabadiliko ya tabia nchi.

Aweso alisimama asijue nini cha kujibu huku akiendelea kutazamana na Spika Ndugai kwa sekunde kadhaa ndipo akaamuliwa kuketi kwa kuwa alikuwa hajui swali gani liliulizwa.

“Tatizo lenu mawaziri hamsikilizi kinachoendelea ndani ya Bunge, mnapiga stori tu. Haya naibu waziri Ofisi ya Makamu wa Rais okoa jahazi hilo,” alisema Ndugai.

Baada ya maswali kadhaa kupita aliwataka naibu mawaziri ofisi ya Rais (Tamisemi), Joseph Kakunda na Joseph Kandege kujibu swali la nyongeza kuhusu umaliziaji wa majengo ambayo yanaanzishwa na wananchi.

“Haya naibu mawaziri Tamisemi, Josephat Kandege naomba ujibu swali hilo. Kama hujajipanga naomba mwenzako Joseph Kakunda ajibu, jamani ndiyo haya niliyosema wapo hapa tu lakini wanapiga stori na hawasikilizi kinachoendelea,” alisema spika.

Ndugai aliwaonya pia wabunge kutozungumza na waziri mkuu na kumtaka kiongozi huyo wa shughuli za Serikali kuzungusha macho ili kuona namna ambavyo wabunge walikuwa wamesimama na kutaka kuuliza maswali kuhusu maji.

“Mheshimiwa waziri mkuu, naomba hao wanaozungumza na wewe wakuache kwanza, hebu geuka nyuma na uangalie pande zote uone namna ambavyo wabunge wamesimama kutaka kuuliza maswali kuhusu maji majimboni kwao, Serikali iangalie jambo hili,” alisema.

Wakati huo spika aliitaka Serikali kutafakari namna ambavyo imekuwa ikitoa maagizo na amri kila wakati kupitia mabaraza ya madiwani akisema siyo afya na haijengi.

Alikuwa akitolea majibu mwongozo ulioulizwa na mbunge wa Babati Mjini (Chadema), Pauline Gekul kuhusu mpango wa Serikali kuagiza wananchi kuendelea kumalizia majengo ya zahanati, maabara na madarasa waliyoyaanzisha.

“Ndugu zangu Serikali, anachokisema mbunge ni sahihi maana sasa imekuwa ni kero kubwa, hebu angalieni jambo hilo kwani kila mahali ni maagizo maagizo na hata tukienda kwenye baraza la madiwani utasikia kuna ajenda ya kudumu ambayo ni maagizo, hii inakera jamani,” alisisiza Ndugai.

Pia, aliwataka viongozi kuangalia namna bora ya kufanya ili kufikisha ujumbe kuliko kuagiza kila mara ambako kunaondoa imani ya wananchi kwa Serikali yao.

Hata hivyo, alisema kumekuwapo na tabia ya baadhi ya viongozi kujiona kama miungu watu na wanaamini kuagiza kila wakati kwa kutumia amri ndiyo itakuwa maendeleo wakati si kweli.

No comments:

Post a Comment