KWA MAONI AU USHAURI E-mail: inocomm2014@gmail.com, PIGA SIMU: 0714555668

www.utt-pid.org


TEMBELEA: www.utt-pid.org

May 23, 2018

RAIS WA TLS, FATMA KARUME AKUTANA NA KUFANYA MAJADILIANO NA IGP SIRRO

Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), Fatma Karume amemtembelea mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro ofisini kwake akieleza wamejadiliana mambo manne yanayohusu masuala ya sheria na haki.

Wakati Fatma akieleza hayo jana, msemaji wa Jeshi la Polisi, Barnabas Mwakalukwa alisema: “Alikuja kujitambulisha kuwa yeye ni rais wa TLS. Ilikuwa ziara ya kawaida na binafsi, hapa tunapokea wageni wa kila aina.” 

Fatma ameyataja mambo waliyojadiliana kwakina na IGP Sirro kuwa ni wanasheria kutobughudhiwa wanapokuwa kwenye vituo vya polisi, hali ya usafi na usalama wa mahabusu wawapo rumande, haki ya maandamano na uhuru wa polisi kufanya uamuzi bila kushinikizwa na wanasiasa.

Fatma ambaye ni wakili wa kujitegemea alichaguliwa kuongoza TLS Aprili 14, akichukua mikoba ya Tundu Lissu aliyemaliza muda wake wa uongozi.

Alisema wanasheria wamekuwa hawatendewi haki wanapokuwa katika vituo vya polisi kutetea wateja wao.

Fatma alisema ni haki ya kila raia kuwa na mwanasheria anapopata tatizo la kisheria na ni haki ya wanasheria kutimiza majukumu yao bila kuingiliwa.

Pia, alisema walijadiliana kuhusu usafi wa mahabusu na kutojaza watuhumiwa kwenye vyumba vidogo.

Alisema alizungumzia haki ya wananchi kuandamana na umuhimu wa kufanya hivyo.

Kuhusu uhuru wa polisi kufanya kazi bila kuingiliwa alisema: “Natambua kuwa sheria ya mfumo mzima wa Jeshi la Polisi haijakaa sawa, ingekuwa amri yangu ingebadilishwa ili kuwe na usawa katika utendaji na wao wafanye kazi zao bila kuingiliwa na wanasiasa.”

“Nchi zilizoendelea wakuu wa polisi wanateuliwa na kamati, lakini sheria za nchini wanateuliwa na Rais, jambo ambalo linawawia vigumu kufanya kazi kwa kujitegemea,” alisema Fatma.

Alisema anatambua hilo lipo nje ya uwezo wa Polisi, hivyo kitu pekee wanachopaswa kufanya ni kuhakikisha wanafanya kazi kwa mujibu wa sheria.

Fatma alisema IGP Sirro aliwaomba kuelimisha wananchi kuhusu sheria, kutambua haki zao na wajibu wao katika kuzitekeleza.

“Nimelichukua hili, tutatafuta majukwaa kuhakikisha tunatoa elimu kwa jamii kuhusu sheria, namna ya kuzitekeleza na wajibu wao,” alisema Fatma.

No comments:

Post a Comment