KWA MAONI AU USHAURI E-mail: inocomm2014@gmail.com, PIGA SIMU: 0714555668

www.utt-pid.org


TEMBELEA: www.utt-pid.org

May 18, 2018

SETHI AGOMA KUVULIWA MADARAKA IPTL


SeeBait
Siku chache baada ya kuondolewa katika Bodi ya Wakurugenzi ya Kampuni ya Kufua Umeme ya IPTL, mfanyabiashara Herbinder Sethi ameeleza kusikitishwa kwake na hatua hiyo, huku akisema hautambui uongozi mpya uliowekwa madarakani.

Uamuzi wa kumwondoa Sethi katika bodi ya wakurugenzi ambayo pia ilimvua uenyekiti wa IPTL, ulifikiwa baada ya kushindwa kushiriki na kuhudhuria mikutano ya bodi kwa miezi sita mfululizo bila ruhusa, tangu Juni 19, 2017 alipokamatwa na kushtakiwa.

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ilimsomea Sethi mashtaka 12 ya uhujumu uchumi, utakatishaji fedha na kuisababishia Serikali hasara ya Dola 22.198 milioni za Marekani (Sh309.5 bilioni).

Hata hivyo, taarifa kutoka kwa wakili wake, Hajra Mungula iliyotolewa jana kupitia mitandao ya jamii ilisema Sethi hatambui mabadiliko ya uongozi uliowekwa na kwamba yeye ni mmiliki halali wa IPTL ambayo kimsingi inamilikiwa na kampuni anayoimiliki ya Pan African Power Solutions (PAP).

“Pamoja na kuagiza wanasheria wake kuchukua hatua za haraka za kisheria, Mwenyekiti Sethi pia hana taarifa zozote juu ya mabadiliko hivyo anapenda kuutaarifu umma wazipuuze taarifa hizo kwa kuwa hazitokani na mamlaka halali ya kisheria ya kampuni hiyo,” ilisema taarifa ya Mungula

Mungula alisema mabadiliko hayo yamekwenda kinyume na notisi ya katazo la Mwanasheria Mkuu wa Serikali la Februari 12, 2018 lenye kumbukumbu Na. AGS234 lililozuia aina yoyote ya uhamishaji wa mali na umiliki wa mali za IPTL.

“Kimsingi mabadiliko hayo batili yanaathiri na kwenda kinyume na maelekezo ya Serikali.

“Pamoja na kwamba Mwenyekiti bado yuko mahabusu akituhumiwa kwa mashtaka kadhaa ya jinai, hiyo haiondoi ukweli kuwa IPTL ni kampuni binafsi yenye wamiliki halali wenye hisa halali, hivyo haiwezekani kwa mtu asiyehusika na asiye mwanahisa kutangaza mabadiliko ya uongozi bila kufuata taratibu zilizopo kisheria,” alisema Mungula.

Alisisitiza kwamba licha ya Sethi kuwa na mashtaka ya jinai yanayomkabili, lakini Watanzania wajue bado kampuni hiyo iko chini ya usimamizi salama wa PAP na kwamba madeni yote, madai ya mali na stahiki zote zinazohusiana na kampuni hiyo zipo katika mikono salama.

No comments:

Post a Comment