Mitazamo
ya wananchi kuhusu elimu bure imebadilika kwa kiasi kikubwa ndani ya
miaka 12 iliyopita: mwaka 2005, zaidi ya nusu ya wananchi (56%) walisema
kuwa ‘ni bora elimu itolewe bure kwa watoto wetu, hata kama kiwango cha
elimu ni cha chini’.
Mwaka 2017, wananchi 9 kati ya 10 (87%) wanasema ‘ni bora tukaongeza viwango vya elimu, hata kama itatulazimu kulipa ada.’
Wananchi
9 kati ya 10 (87%) wangependa serikali itumie fedha kwenye mpango wa
kutoa mafunzo na kuwasaidia walimu kuliko kugawa sare za shule bure
ikilenga kuwaondolea wazazi mzigo wa kununua sare hizo.
Matokeo
haya yametolewa na Twaweza katika utafiti wake uitwao Elimu Bora au
Bora Elimu? Elimu waitakayo watanzania. Matokeo ya muhtasari huu
yanatokana na takwimu za utafiti wa Sauti za Wananchi, utafiti wa kwanza
barani Afrika wenye uwakilishi wa kitaifa unaotumia simu za mikononi.
Matokeo
haya yanatokana na takwimu zilizokusanywa kutoka kwa wahojiwa 1,786
kutoka maeneo mbalimbali ya Tanzania Bara (Zanzibar haihusiki kwenye
utafiti huu) kati ya mwezi Septemba na Oktoba 2017.
Utafiti
huu umebaini kwamba ni wazazi wachache sana huzingatia ada nafuu (6%)
na umbali wa shule (18%) wakati wa kuchagua shule za sekondari kwa ajili
ya watoto wao. Badala yake wazazi wengi huzingatia zaidi viwango vya
juu vya ufaulu wa shule husika (asilimia 72) na walimu wanaojituma
(asilimia 72 pia). Wazazi wanataka elimu bora na wameonesha utayari wa
kuigharamia.
Idadi
ya kaya zinazowapeleka watoto wao kwenye shule za binafsi (asilimia 10)
haijabadilika kati ya Agosti/Septemba mwaka 2016 na Septemba/Oktoba
2017.
Hata
hivyo, uandikishaji wa watoto kwenye shule binafsi hutofautiana kutoka
na ngazi ya elimu, wazazi 3 kati ya 10 (27%) huchagua shule binafsi kwa
ajili ya elimu ya awali na 2 kati ya 10 (17%) kwa ngazi ya sekondari
ukilinganisha na mzazi mmoja kati ya kumi (7%) wanaoandikisha watoto wao
kwenye shule za msingi za binafsi.
Hata
hivyo, wazazi wanajitahidi kutekeleza majukumu yao: zaidi ya wazazi 5
kati ya 10 (53%) walichangia ujenzi wa shule mwaka uliopita; 4 kati ya
10 (38%) walitoa fedha, 1 kati ya 10 (18%) walichangia nguvu kazi na 1
kati ya 10 (9%) walitoa vifaa.
Na
kwa kawaida wazazi pia hulipia vifaa kama vile vya kuandikia (98%),
sare za shule (75%), mabegi ya shule (26%) na vitabu (15%). Zaidi, 85%
wanasema walikutana na walimu wa watoto wao angalau mara moja au mbili
mwaka uliopita, ukilinganisha na 79% waliofanya hivyo mwaka 2016. Wazazi
wengi zaidi (30%) wana uwezekano wa kukutana na walimu kila baada ya
miezi michache ukilinganisha na mwaka 2016 (21%).
Zaidi
ya nusu ya wazazi wnalipokea jukumu la msingi la kuhakikisha watoto
wanajifunza japokuwa idadi kubwa kidogo (46%) pia wanasema jukumu hilo
ni la walimu.
Hakuna
mzazi aliyesema jukumu la watoto kujifunza ni la maafisa elimu,
wanasiasa au yeyote serikalini. Na pale walipouliuzwa ni kwa namna gani
wanausaidia uongozi wa shule, wazazi wengi (52%) walizungumzia jukumu
lao katika kuwaadhibu watoto wao na wengine wachache wakitaja ushiriki
wao kwenye harambee za kuchangisha fedha (22%), kufuatilia mahudhurio ya
walimu (14%) au kutoa maoni kwenye ukaguzi wa mahesabu ya shule (4%).
Mkurugenzi
Mtendaji wa Twaweza, Aidan Eyakuze, anasema: “Ujumbe wa msingi wa
wananchi kuhusu suala la elimu nchini ni huu: wako tayari kuilipia elimu
bora kwa ajili ya watoto wao.
Mitazamo
ya wananchi inaonekana kubadilika kwa kiasi kikubwa katika kipindi
fulani, ikiashiria kuwa sasa wanaelewa kilichofanyika na walichopoteza.
Utafiti huu unadhihirisha kuwa wananchi wanapaswa kuwa sehemu muhimu ya
mjadala wa kitaifa utakaolenga kuboresha matokeo ya elimu yetu.”
No comments:
Post a Comment