KWA MAONI AU USHAURI E-mail: inocomm2014@gmail.com, PIGA SIMU: 0714555668

www.utt-pid.org


TEMBELEA: www.utt-pid.org

June 8, 2018

BREAKING: SERIKALI YAIKANA BARUA WALIYOANDIKIWA KKKT IKIWATAKA WAFUTE WARAKA WAO WA PASAKA

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba amesema barua iliyoandikwa na wizara hiyo ya kulitaka Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT) kuufuta waraka wa Pasaka ni batili.

Akizungumza leo Juni 8 katika mkutano na wanahabari, Dk Nchemba amesema taarifa zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii ni batili na siyo maelekezo ya serikali au wizara.

“Tunawaomba viongozi wa dini waendelee na kazi zao, nasema jamii iwe macho na taarifa zinazosambaa kwenye mitandao ya jamii na wasifanyie kazi taarifa hizo,” amesema.

Kadhalika, Dk Nchemba amesema amefuatilia barua hizo na kuona zina mkanganyiko wa anuani.

“Viongozi wa dini wasiwe na taharuki na taarifa hizo, hazina baraka za Serikali. Wasisite kuwasiliana na Serikali kujua uhalali wake.” Amesema.

Pia Dk Nchemba amesema waraka wa viongozi wa dini uliotolewa miezi iliyopita ni jambo lililopita na hivyo akawataka viongozi wa dini waendelee na kazi zao.

Dk Nchemba amewataka viongozi wa dini kuendelea na kazi zao. “Nchi yetu ni moja na tunaishi kwa taratibu tulizojiwekea na tuna madhehebu mengi.” Amesema na kuongeza: “Wengine wameliona jambo hilo kama ajenda. Wananchi wawe makini, wasiwafuate watu hao wanaotaka kuwagawa.”


Mbali na hato Waziri Nchemba ameonya wanasiasa wanaoingilia jambo hilo kisiasa kwa kusema kwamba kama umakini usipowekwa amani ya nchi itavurugika na ingawa bado wanaendelea na uchunguzi kuwabaini wahusika ili hatua zaidi ziweze kuchukuliwa.

No comments:

Post a Comment