KWA MAONI AU USHAURI E-mail: inocomm2014@gmail.com, PIGA SIMU: 0714555668

www.utt-pid.org


TEMBELEA: www.utt-pid.org

June 8, 2018

SERIKALI KUIRUDISHA RUZUKU CCBRT

Serikali  inakusudia kukaa mezani na uongozi wa Hospitali ya CCBRT kujadili kwa kina ili ianze tena kuipatia ruzuku kama ilivyokuwa awali.

Hayo yalielezwa   na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, alipozungumza mbele ya Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan aliyetembelea hospitali hiyo, Dares Salaam  jana.

“Serikali inatambua mchango mkubwa wa CCBRT katika kuhudumia wananchi tena huduma nyingine mnatoa bila malipo.

“Hii inamaanisha mnatoa huduma zaidi bila kujali faida, mnafanya vizuri katika huduma za tiba ya mifupa, macho na afya ya mama na mtoto.

“Mnasaidia mno kupunguza mrundikano wa wagonjwa katika hospitali zetu za serikali, ni kweli awali serikali ilikuwa inawapatia ruzuku lakini katika awamu hii ya tano ilisitishwa.

“Tunakusudia kukaa nanyi tena mezani tujadiliane na tukubaliane,  lengo letu tunataka ile ruzuku tutakapokuwa tunaileta iwafikie watumishi husika moja wa moja, tunataka kujua tunawalipa wauguzi au madaktari kiasi gani,” alisema.

Alisema   CCBRT imekuwa mdau mzuri katika sekta ya afya kwa kushirikiana na serikali ambako imekuwa ikiwajengea uwezo watumishi wake.

“Kwa mantiki hiyo tunakusudia kuipandisha hadhi CCBRT na kuifanya hospitali ya pekee inayoshirikiana na serikali katika kutoa matibabu dhidi ya tatizo la fistula,” alisema.

Awali, Ofisa Mtendaji Mkuu wa CCBRT, Erwin Telemans aliiomba serikali kuipunguzia kodi hospitali hiyo  iweze kuendelea kutoa huduma bora kwa jamii.

“Hatua hiyo itatuwezesha kuendele kununua vifaa tiba vya kutosha na hata kuwalipa maslahi mazuri wafanyakazi wetu ikizingatiwa kwamba zipo huduma ambazo wagonjwa huhudumiwa bila malipo ikiwamo ya fistula,” alisema.

Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan alisema serikali imepokea ombi hilo na   italifanyia kazi hasa kupitia meza hiyo ya majadiliano.

“Waziri amesema itaandaliwa meza ya majadiliano, hivyo ni imani yangu kwamba mtajieleza vizuri kwa kina kuhusu huduma mnazotoa na kuonyesha matokeo ya kazi mlizofanya.

“Sisi (serikali) tupo tayari kushirikiana nanyi ili tuendelee kuboresha huduma za afya nchini kwa pamoja.

“Mmenieleza kwa siku mnapokea wagonjwa wapatao 700, binafsi nimeguswa kwa jinsi mlivyoboresha afya ya mama na mtoto na namna mnavyowarejeshea furaha watu waliopoteza viungo.

“Hakika hii ni kazi ya kiungu na mnatoa sadaka kubwa kwa watanzania,” alisema.

No comments:

Post a Comment