Pembe za Ndovu |
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili kwa muda mrefu
unaonyesha kuwa wanafunzi wa shule za msingi wanaoshiriki ujangili huo
ni wa kuanzia darasa la nne hadi la saba na kwamba kazi hiyo wanaifanya
kwa baraka za wazazi wao.
Baadhi ya wazazi wa wanafunzi hao wameamua kuwapa
baraka watoto wao kuingia kwenye hifadhi kuwinda wanyamapori ili
wakikamatwa na maofisa wanyamapori wahurumiwe na kuachiwa kutokana na
umri wao mdogo.
Shule za msingi na sekondari zinazokabiliwa na
tatizo la utoro wa wanafunzi za Kata ya Sedeko, Mbalibali na Machochwe
ambazo ziko kando kando ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na Mapori ya
Akiba ya Ikorongo na Gurumeti.
Uchunguzi wa gazeti hili uliofanywa katika maeneo
hayo na kuthibitishwa na walimu, waratibu elimu, madiwani, waendesha
mashtaka na wadau mbalimbali umebaini vitendo hivyo hufanywa kwa sababu
mbalimbali.
Jinsi ujangili unavyofanyika
Chacha Joseph mkazi wa Kijiji cha Machochwe
anasema kuna aina nyingi ya uwindaji unaofanywa na wanafunzi hao
mojawapo ni wanafunzi kuwinda wanyamapori usiku wakiwa na ng’ombe wao
ili kukwepa kuonekana na askari wa hifadhi. Anasema hufanya kazi mbili
kwa wakati mmoja, moja kuwapatia malisho ng’ombe wao ambao hawana sehemu
ya kuwalishia wakati wa mchana na kufanya kazi ya uwindaji.
Uwindaji hufanywa kwa kutumia kurunzi kubwa yenye
mwanga mkali na njia ya pili ya kuwakimbiza wanyamapori wakiwa katika
makundi kuwaelekeza katika makorongo makubwa yaliyopo katika hifadhi
hiyo ambako hutumbikia na kufa.
Anasema wakiingia eneo la hifadhi huwaacha ng’ombe
wakiendelea kula majani, wao huelekea ndani zaidi ya hifadhi kutafuta
wanyamapori ambako hupatikana kwa wingi.
Chacha anasema kwa kutumia kurunzi maarufu kama
‘kombora’ wanafunzi hao wakiwa katika kundi la watu 10 hadi 15,
wakiwaona wanyama kama vile swala, pofu, nyumbu huwafuata taratibu kisha
kuwamulika ghafla na kurunzi hiyo, hivyo kutokana na mwanga wake kuwa
mkali huwachaganya na hivyo, kwa kutumia mbwa na mikuki huwashambulia
na kuwaua.
Anasema njia hii ya uwindaji huwafanya waue zaidi ya wanyama watano kwa siku.
Hata hivyo, anasema kwa njia ya kuwinda kwa
kuwafukuza wanyama kwa kuwaelekeza katika makorongo makubwa huua wanyama
wengi zaidi.CHANZO MWANANCHI
No comments:
Post a Comment