Mwenyekiti
wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Jakaya Kikwete, amesema mgombea urais wa
chama hicho, Dk. John Magufuli, ni chaguo la Mungu.
Akizungumza
na wazee, wanawake, vijana na wanachama wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam
jana, alisema jina la Dk. Magufuli lilijitokeza katika hatua zote za
uteuzi ikiwamo vikao vya wazee na hata katika Mkutano Mkuu alichaguliwa
na maelfu, jambo linaloonyesha anakubalika kwa wote.
Alisema Mungu ametoa hukumu yake kwa mtu wake na Watanzania ndiyo wataamua katika sanduku la kura.
“Magufuli
ni mgombea wa sampuli nyingine, ni mzalendo anapenda watu, nchi yake
kwa dhati, asiyejikweza hana makuu, anamwamini Mungu, anatambua CCM
imemfikisha alipo leo, ni kada mzoefu... sifa yake nyingine anapenda
kuona matokeo ya kazi anayoifanya na aliyopewa kuifanya,” alisema.
Kikwete
ambaye ni Rais wa Awamu ya nne, alimwagia sifa Dk. Magufuli kuwa ni
mmoja wa watumishi wa umma ambaye hakusita kutangaza Ilani ya chama
chake na chama kwa ujumla, hivyo ni kada wa uhakika, mzoefu ndani ya CCM
anayestahili kuunda serikali ya awamu ya tano.
“Wapo
maafisa wa serikali wanaona haya kusema wanatekeleza ilani ya CCM,
lakini Magufuli katika kazi zake zote alisema anatekeleza Ilani ya CCM
na anatambua yupo alipo kwa sababu ya chama na siyo kwa ujanja na fedha
zake kwa kuwa hana fedha,” alibainisha.
Kikwete
alisema uteuzi wa Magufuli unakipa sifa chama kuwa hakinunuliki kwa
kuwa hakuwahi kujivuna kwa fedha wala mali, kwani ndani ya siasa mtu
anaweza kuwalipa wachache kwa tamaa na njaa zao, lakini huwezi kununua
chama.
“Nawaambia watalipa wachache, lakini hawatawanunua Watanzania wataamua,” alisema na kuongeza:
“Sifa
nyingine ni Mungu ametaka Magufuli awe rais, kwani aliwahi kuja Ikulu
kuzungumza nami masuala ya makandarasi, nikamuuliza naona wenzako
wanachukua fomu wewe huchukui?”
"Aliniuliza kwani na mimi natosha? Nilimwambia wana-CCM ndiyo wataamua kama unatosha au la,” alisema.
Alisema Dk. Magufuli ni kada aliyechukua fomu kimya kimya bila kuita waandishi wa habari.
“Alichukua
fomu bila mbwembwe, alitembea kutafuta wadhamini bila wapambe na
alirudisha bila mbwembwe na mgombea wa namna hiyo anakifaa chama na
Watanzania,” alisema
Alisema
mgombea huyo hana mbwembwe kwani alipoulizwa kama ana kikosi cha kazi,
alisema anaweza kufanyakazi na yeyote na kukiachia chama kupanga timu ya
ushindi ya makada 32.
Aidha,
alimmimina sifa Dk. Magufuli kuwa hakubali kushindwa katika jambo
lolote, mbunifu, anachukia wazembe, wababaishaji wala rushwa na kwamba
atapendwa na kila Mtanzania anayechukia mambo hayo.
Kwa
upande wake, Dk. Magufuli alisema anatosha pande zote, mbele, katikati,
nyuma, kulia kushoto na ubavuni, na yupo tayari kupeperusha bendera ya
CCM na kuongoza serikali ya awamu ya tano.
“Mwalimu
alipotaka kwenda kupigana vita na Idd Amini, alianzia Dar es Salaam,
marais wote waliopita walipoaanza safari ya kwenda Ikulu walianzia hapa,
nimekuja kwenu wazee wa Dar es Salaam, vijana na kinamama kuomba
baraka, nasaha, busara na dua zenu kabla ya kuanza safari yangu.
Jumapili nitaongea mengi leo (jana) ni hayo tu,” alisema.
Alisema
yuko tayari kupeperusha bendera ya CCM bila kigugumizi, kinyongo,
uchovu na manunguniko hadi kuhakikisha serikali ya awamu ya tano
inaingia Ikulu.
“Wana
CCM tushikamane kura za maoni za urais, ubunge na udiwani zimekwisha,
jukumu letu liwe kuhakikisha tunafanya kampeni uvungu kwa uvungu,
kitanda kwa kitanda, chumba kwa chumba na nyumba kwa nyumba kuhakikisha
CCM inaunda serikali ijayo, ni chama kikubwa kimehimili mengi na kina
uwezo wa kuendelea kutawala,” alibainisha na kuongeza:
“Nawathibitishia
natosha na ninatosha kweli kweli, mbele, katikati, nyuma na ubavuni,
wanatosha mgombea mwenza, madiwani na wabunge.”
Shida za wana-Dar es Salaam na Watanzania nazifahamu...uzoefu wa miaka 20 serikalini unanitosha, sikuwahi kushindwa mahali.”
Mgombea
Mwenza, Samia Suluhu, alisema ni mama wa watoto wanne, hivyo matatizo
ya Watanzania anayajua kama mama anayeijua familia yake na kuwataka
kujitokeza kwa wingi kuiunga mkono CCM.
Mpekuzi
No comments:
Post a Comment