Siku moja baada ya kutokea mapambano ya zaidi ya saa 16 baina ya Jeshi
la Polisi na watu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi kwenye mapango ya
mlima ya Utemini, wananchi wa eneo hilo wameingiwa na hofu ya usalama
wao baada ya baadhi yao kuona wahalifu wakitoroka wakati wa tukio hilo.
Wananchi hao wana hofu kuwa majambazi waliotoroka wanaweza kurejea na kuwadhuru na tayari baadhi wameanza kuhama makazi yao.
Hofu
ya wananchi hao imekuja baada ya polisi kupambana na watu hao usiku wa
kuamkia juzi, wakitumia silaha kali zilizo sababisha kizaazaa kwa wakazi
wa Utemini, kutokana na milio ya risasi na mabomu.
Mwenyekiti
wa Mtaa wa Utemini Ibanda, kata ya Mkolani, Jukael Kiula jana alisema baadhi
ya wananchi wanaoishi jirani na mapango hayo wameanza kuhama makazi yao
wakihofia kurejea kwa majambazi hao.
“Kwa mujibu wa maelezo ya
baadhi ya majirani, walikuwa wakiwaona watu wakipanda na kushuka kutoka
kwenye milima yenye mapango waliyojificha watu hao. Lakini hawakuwatilia
shaka wakidhani ni watu wanaopasua mawe, hadi siku polisi walipopambana
na majambazi hayo,” alisema Kiula.
Mwenyekiti huyo aliiomba Serikali kuimarisha ulinzi na doria kwenye mtaa huo ili kuwahakikishia usalama wananchi.
“Hata ikibidi, askari wa Jeshi la Wananchi waweke kambi ya muda kwenye eneo hilo kudhibiti vitendo vyovyote vya uvamizi,”alisema.
Akizungumza
na wakazi wa Utemini jana, mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Baraka Konisaga
aliwahakikishia kuwa Serikali itaimarisha ulinzi kudhibiti uwezekano wa
wahalifu kuendelea kutumia mapango hayo kujificha.
Konisaga
ambaye alitembelea eneo la tukio jana, aliwaomba wakazi kutoa taarifa za
maficho ya wahalifu pale wanapohisi kuna nyendo zinazotilia shaka.
Kamanda
wa polisi wa Mwanza, Ahmed Msangi alisema kiama cha wahalifu kimefika
na kwamba tayari vyombo vya dola vimebaini mitandao ya uhalifu na
wahusika na itawasaka usiku na mchana.
“Hatutakuwa na msalie
mtume katika mapambano dhidi ya ujambazi Mwanza. Wote wanaojihusha na
ujambazi watambue kuwa yatawakuta yaliyowakuta wenzao waliojaribu
kupambana na polisi,” alionya Kamanda Msangi.
Mkuu wa Mkoa, John
Mongella alisema mkakati wa kuifanya Mwanzaa iwe salama umeanza na
hakuna mhalifu atakayeingia Mwanza na kutoka salama.
|
June 7, 2016
MAJAMBAZI YALIYOTOROKA MAPANGONI JIJINI MWANZA YAZUA HOFU...BAADHI YA WANANCHI WAANZA KUYAHAMA MAKAZI YAO
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment