JUMUIYA
ya Wanataaluma ya Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOMASA) imesema kilichotokea
si walimu kugoma kufundisha programu ya Stashahada Maalumu ya Elimu,
Sayansi, Hisabati na Tehama, bali tatizo ni kutoelewana na Menejimenti
ya chuo kutokana na mazingira mabovu ya uendeshaji wa programu hiyo
chuoni hapo.
Aidha,
imelaani kitendo cha wanafunzi 7,802 wa Programu Maalumu ya Ualimu wa
Msingi na Sekondari, waliorudishwa nyumbani bila kupewa muda wa kutosha
kujiandaa kwa kuzingatia umri wao na mazingira waliyokuwa wanaishi, hali
inayofanya wazagae mitaani huku wakiwa hawana pa kwenda.
Hayo
yako kwenye tamko lililotolewa jana na Katibu wa jumuiya hiyo, Lameck
Thomas, ambalo lilieleza kuwa lawama zimekuwa zikitupwa kwa walimu
kutokana na taarifa hizo kutolewa na upande mmoja, ambao ni Menejimenti
ya chuo kwenda serikalini bila kuwepo na taarifa yoyote kutoka kwa
walimu kupitia jumuiya yao.
Thomas
alisema si kweli kama walimu waligoma kufundisha lakini tatizo kubwa ni
kutoelewana kati ya walimu na Menejimenti ya chuo kutokana na mazingira
mabovu ya uendeshaji wa programu hiyo chuoni hapo.
"Hatuzungumzii
fedha zaidi tunazungumzia suala la kuboresha elimu ili taifa lipate
walimu wa baadaye katika kufundisha Sayansi, Hisabati na Tehama, vifaa
vya kufundishia navyo ni changamoto kubwa,” alisema.
Katibu
huyo alisema kama Jumuiya ya Wanataaluma wanapata hisia kwamba Wizara
ya Elimu, imeamua kwa makusudi kushirikiana na uongozi wa chuo kupotosha
uhalisia wa jambo hilo kwani hakuna hata wakati moja ambao wamefanya
mawasiliano na walimu wenyewe kupata ukweli kutoka upande wao.
“Alichosema
waziri bungeni juzi ni taarifa ya upande mmoja ambayo haitatupeleka
kwenye utatuzi wa kudumu wa suala hili kutokana na ukweli kwamba walimu
nao wana mengi ya kuzungumza,” alisema katibu huyo.
Alisema
serikali imejenga desturi ya kuonana na menejimenti za vyuo pindi
yanapotokea matatizo bila kupata taarifa kutoka vyanzo vingine hali
ambayo imekuwa inasababisha vyanzo sahihi vya matatizo kutojulikana kwa
uwazi.
Alisema
changamoto za ufundishaji kutokana na uhaba na walimu kulingana na
idadi ya wanafunzi waliopo. Akitoa mfano alisema kwa sasa Chuo cha
Sayansi Asilia na Hesabu, kina upungufu wa walimu 128 waliokuwa
wanahitajika kufundisha programu hiyo kwa ufanisi; na kwa muhula
uliopita walimu 72 tu ndio walibeba mzigo wa upungufu huo na muhula huu
hali ilikuwa inaelekea kuwa mbaya zaidi.
“Wingi
wa wanafunzi na uhaba huu wa walimu ulisababisha upangaji wa ratiba na
kufundisha kutokana na ukweli kwamba kozi ziligawanywa katika mikondo
mingi ambayo walimu walilazimishwa kuifundisha huku wakiwa na majukumu
ya kufundisha kozi za shahada na majukumu mengine,” alifafanua.
Alisema
chuo kimekuwa na desturi ya kupokea wanafunzi wengi bila kuzingatia
idadi ya walimu waliopo na miundombinu ya kufundishia na kujifunzia na
hiyo si mara ya kwanza kwa chuo kufanya hivyo, kwani mwaka 2008 walileta
wanafunzi wengi ambao matokeo yake walimu kufundisha masomo mengi
kuliko uwezo wao wa kazi.
Alisema
taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma
ilipotoshwa, kwani haijaeleza ukweli wa madai uliowasilishwa na chuo
husika.
Alisema
katika Chuo cha Sayansi Asilia na Hesabu taarifa inasema
yaliyowasilishwa ni madai ya Sh milioni 367.8 na kupungua mpaka Sh
milioni 90 wakati uhalisia ni kwamba madai hayo hata yangebanwa namna
gani yasingepungua mpaka chini ya Sh milioni 223.7.
Alisema
mfano mwingine ni Chuo cha Elimu Masafa na Sayansi za Kompyuta ambao
taarifa inasema waliwasilisha madai yanayozidi Sh milioni 100 wakati
taarifa ya chuo inasema ni madai ya Sh milioni 53.7 tu.
Mwenyekiti
wa jumuiya hiyo, Edson Baradyana alisikitishwa na yaliyotokea na
kuitaka serikali kufanya jitihada za makusudi ili kumaliza mgogoro huo
na hilo litawezekana kama walimu, wanafunzi na Menejimenti kukaa pamoja.
Baradyana
alisema wanafunzi hawakutendewa haki kwani ilitolewa notisi ya ghafla
ya kuondoka chuoni huku wengine wakiwa hawana nauli na hawakujua pa
kwenda hali inayofanya waendelee kuzurura mitaani.
Alisema
wanaamini kama Menejimenti ya chuo ingeonesha ushirikiano wa karibu kwa
walimu wanaofundisha programu hiyo na kushirikiana, hayo yasingetokea
au yasingekuwa makubwa kiasi hicho.
“Lazima
kuangaliwa na kutatuliwa kwa changamoto nyingine zilizoibuliwa na
wanataaluma na wanafunzi katika uendeshaji wa programu hiyo badala ya
kujikita kwenye suala la malipo tu, serikali iwe na utaratibu wa
kuwasiliana na walimu na wanafunzi mara kunapotokea matatizo vyuoni ili
kupata taarifa toshelezi kutoka pande zote,” alisema Mwenyekiti wa Udomasa.
Aidha,
wakati wa kurejeshwa nyumbani kwa wanafunzi hao wa Udom kukibebwa
kisiasa na vyama vya upinzani, taarifa ya serikali imeeleza kuwa
wahadhiri waliogoma, walitaka kulipwa posho ya zaidi ya Sh milioni 900.
Akitoa
taarifa ya pili bungeni juzi usiku, Waziri wa Elimu, Sayansi,
Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako alisema
wanafunzi hao si sehemu ya kazi zilizoko katika mikataba ya ajira ya
wahadhiri hao, ila ni sehemu ya kazi ya ziada.
Kwa
kuwa kazi hiyo ni ya ziada, Profesa Ndalichako alisema walikubaliana
walipwe posho ya kazi ya nyongeza ambayo uongozi wa Chuo Kikuu cha
Dodoma ulikuwa tayari kutoa zaidi ya Sh milioni 200.
Kwa
mujibu wa Profesa Ndalichako, wahadhiri hao walisisitiza kuwa wanataka
posho hiyo iwe zaidi ya Sh milioni 900, jambo lililokataliwa na Mkaguzi
wa Ndani wa Mahesabu wa Udom aliyesema kuwa kiwango hicho ni kikubwa
kuliko uhalisia wa kazi yenyewe.
Kutokana
na kutokubaliana kati ya wahadhiri hao na uongozi wa Udom, wahadhiri
hao ndio wakaitisha mgomo wa kufundisha wanafunzi hao huku wakiendelea
na kazi za kufundisha walio katika programu za shahada ya kwanza na
kuendelea.
Profesa
Ndalichako alisema kwa uamuzi huo wa wahadhiri, serikali isingeweza
kuwachukulia hatua kwa kuwa wamegomea kazi ya ziada na si kazi
waliyoajiriwa na kuingia mkataba na chuo.
Kwa
hali hiyo, Profesa Ndalichako alisema serikali ililazimika kuingilia
kati ambapo Mei 10, mwaka huu Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia
na Mafunzo ya Ufundi, Stella Manyanya alikwenda chuoni hapo kutafuta
suluhu.
Mbali
na Naibu Waziri, alisema hata makatibu wakuu wa wizara hiyo nao
walikwenda kuzungumza na wahadhiri hao bila mafanikio, huku wanafunzi
hao wakikaa chuoni bila kuingia darasani kwa wiki ya tatu.
Profesa
Ndalichako alisema mbali na madai ya wahadhiri hao, pia wakati wa
kutafuta suluhu ya jambo hilo, walitazama suala la tija kwa wanafunzi
hao wa diploma maalumu ambao ni zaidi ya 7,800 na pia kwa wanafunzi wa
shahada ya kwanza ambao pia wanapaswa kufundishwa na wahadhiri hao.
Kutokana
na kukosa masomo kwa wiki tatu mfululizo na kuwepo kwa uwezekano wa
kukosekana tija katika ufundishaji, Profesa Ndalichako alisema ndio
uamuzi wa kuwarudisha nyumbani wanafunzi hao ukafanyika ili serikali
iangalie upya utaratibu wenye tija zaidi wa kuwaendeleza wanafunzi hao.
Aidha,
Profesa Ndalichako alisema wakati wanafunzi hao wakitakiwa kurudi
nyumbani, walizingatia hali yao ya kipato, kwa kuwa tayari walikuwa
wameshapewa fedha za kujikimu za siku 60 tangu Aprili 21, mwaka huu.
Profesa
Ndalichako aliwataka wanafunzi hao kuvuta subira wakati serikali
inatafuta namna bora ya kuwapatia elimu hiyo kwa kuzingatia tija kwao.
|
No comments:
Post a Comment