Benki
ya Exim ya China imekubali kutoa mkopo wenye masharti nafuu wa dola za
Marekani Bilioni 7.6 sawa na zaidi ya Shilingi Trilioni 16 za
kitanzania kwa ajili ya kugharamia ujenzi wa mradi mkubwa wa reli ya
kati hapa nchini kwa kiwango cha kisasa (Standard Gauge) unaotarajiwa
kuanza katika mwaka huu wa fedha.
Rais
wa Benki ya Exim ya China Bw. Liu Liang amemueleza Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli jana tarehe 20 Julai, 2016
katika Ikulu ndogo ya Chamwino Mkoani Dodoma, kuwa pamoja na kutoa
fedha hizo zitakazofanikisha ujenzi wa kilometa 2,190 za reli ya kati
benki hiyo itashirikiana na Tanzania katika kubadilishana uzoefu na
utaalamu katika ujenzi na uendeshaji wa reli.
Pamoja
na kukubali kutoa fedha hizo, Rais huyo wa Benki ya Exim ya China
amempongeza Rais Magufuli na serikali yake kwa dhamira ya dhati ya
kuiletea nchi maendeleo ikiwemo kuharakisha ujenzi wa reli ya kati na
ameahidi kuwa benki yake itatoa ushirikiano wa karibu katika kufanikisha
mradi huo na miradi mingine ya maendeleo.
“Kuhusu
huu mradi wa reli ya kati tuna mtazamo chanya, tunauona ni mradi mzuri
na tutatoa ushirikiano wowote utakaohitajika. Tunaamini kuwa kwa
ushirikiano na serikali ya Tanzania mchakato wa utekelezaji wa mradi huu
utafanyika kwa mafanikio na kwa kuzingatia muda” Amesema Rais Magufuli.
Kwa
upande wake Rais Magufuli amemshukuru Rais wa Benki ya Exim ya China
Bw. Liu Liang kwa kukubali kutoa fedha hizo na amemuhakikishia kuwa
Tanzania imedhamiria kutekeleza mradi huo ambao tayari ujenzi wake
umepangwa kuanza katika mwaka huu wa fedha kwa kutumia fedha za ndani
kiasi cha shilingi Trilioni 1 zilizotengwa katika bajeti.
Rais
Magufuli amebainisha kuwa kutekelezwa kwa mradi huo kutasaidia kuinua
uchumi wa Tanzania na nchi jirani zisizopakana na bahari zikiwemo
Uganda, Rwanda, Burundi, na Congo.
“Kwa
hiyo kukubali kwao ambako ilikuwa ni kitu kikubwa, inaonesha kwamba
juhudi za Tanzania kwenda haraka haraka zinakubalika kimataifa, na
wenzetu hawa wachina wana pesa nyingi.
“Na
kule kuaminika kwamba tunakopeshwa kwa masharti nafuu, riba yake ni
ndogo na huku kwetu ni mafanikio makubwa, kwa hiyo mizigo mingi tutakuwa
tunaisafirisha, tutaendeleza reli yetu na bandari zetu” Amesema Rais Magufuli.
Mradi
wa ujenzi wa reli ya kati utahusisha ujenzi wa reli kwa kiwango cha
kisasa (Standard Gauge) kutoka Dar es salaam-Tabora-Isaka-Mwanza,
Tabora-Mpanda-Kalemela, Tabora-Uvinza-Kigoma na Isaka-Keza-Msongati.
Mazungumzo
kati ya Rais Magufuli na Rais wa benki ya Exim ya China yamehudhuriwa
na Balozi wa China hapa nchini Dkt. Lu Youqing, Waziri wa Ujenzi,
Mawasiliano na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa Mnyaa, Waziri wa Fedha na
Mipango Dkt. Philip Mpango na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Suzan Kolimba.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
20 Julai, 2016
No comments:
Post a Comment