
Na Mwandishi Wetu.
Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji
Mhe. Charles Mwijage ameipongeza na kuishukuru Mamlaka ya Mapato
Tanzania (TRA) kwa jitihada za kuendelea kuelimisha wafanyabiashara
kutambua umuhimu wa kulipa kodi utakaoiwezesha Serikali kusonga mbele
katika suala zima na ukuzaji wa viwanda vya ndani hapa nchini.
Mhe. Mwijage aliyasema hayo wakati wa
ufunguzi wa mkutano wa nne wa mwaka wa Taasisi isiyo ya kiserikali
inayotoa Msimbomilia (Barcode) za bidhaa (GS1); uliofanyika tarehe 29
Novemba 2016 katika ukumbi wa mikutano wa Karimjee jijini Dar es Salaam.
Mkutano huo uliandaliwa kwa ushirikiano
kati ya GS1 na TRA kwa lengo la kujadili masuala mbalimbali yanayowahusu
wadau wao, kujadili mambo muhimu ya kodi yanayohusu umuhimu wa Namba ya
Utambulisho wa Mlipakodi (TIN) katika kuweza kupata msimbomilia
(barcodes 620) na kuweza kuzitambulisha bidhaa za Tanzania kimataifa
pamoja na kuadhimisha miaka mitano tangu kuanzishwa kwa taasisi hiyo.
Waziri Mwijage aliliagiza Shirika la
Viwango Tanzania (TBS) kuhakikisha kila mfanyabiashara anayemiliki
viwanda vidogo na vya kati kuhakikisha anakuwa na TIN na namba ya
msimbomilia 620 inayotolewa na GS1 Tanzania kabla ya kuhuisha vyeti vyao
vya biashara.
Aidha Waziri Mwijage amesema kuwa uchumi
wa viwanda unatakiwa kukua nchini ili kuweza kuzalisha bidhaa bora
zitakazouzwa ndani na nje ya nchi na kukusanya kodi stahiki
itakayoiwezesha Serikali kutoa huduma bora za kijamii kwa maendeleo ya
wananchi wa Tanzania .
“Ifike wakati wafanyabiashara muwaelewe
vizuri TRA na kulipa kodi stahiki ya Serikali, ili nchi iweze kusonga
mbele” alisema Mhe. Mwijage.
Kwa upande wake Afisa Mkuu wa Elimu kwa
Mlipakodi kutoka TRA Bi. Rose Mahendeka alisema kuwa wafanyabiashara
wote ambao wanahitaji kutumia mfumo wa kuuza bidhaa kwa kuweka
msimbomilia (Barcode 620) wanapaswa kupitia TRA kwa ajili ya usajili na
uhakiki wa Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN) kabla ya kwenda
kupata huduma ya msimbomilia 620.
Bi. Mahendeka aliwasisitiza wadau hao
kuhakikisha wanajisajili na TIN na wale waliojisajili kuhakikisha
wanahakiki taarifa zao ili kurahisisha upatikanaji wa Msimbomilia 620 na
kuiwezesha TRA kupata takwimu sahihi za wafanyabiashara wazalishaji na
wanaouza bidhaa zao nje ya nchi.
“Wafanyabiashara wote ambao wanahitaji
kutumia mfumo wa kuuza bidhaa kwa kuweka Msimbomilia(Barcode 620)
wanapaswa kupitia TRA kwa ajili ya usajili na uhakiki wa Namba ya
Utambulisho wa Mlipakodi(TIN) kabla ya kwenda kupata huduma” alisisitiza
Bi. Mahendeka.
Aidha Bi. Mahendeka alisema kuwa
wafanyabiashara ambao wanahitaji kuuza bidhaa zao kwa kutumia
msimbomilia wanapaswa kulipa kodi bila ya kukwepa ili kuiwezesha
Tanzania kupiga hatua kufikia uchumi wa viwanda na vilevile kuweza kutoa
huduma bora kwa maendeleo ya jamii.
Naye Mwenyekiti wa bodi ya GS1 Bw. Gideon
Mazara alitoa rai kwa wafanyabiashara wanaozalisha bidhaa kutumia
Msimbomilia 620 wa Tanzania na kuweza kutangaza bidhaa za hapa nchini
ili kupata soko la kimataifa litakalowezesha nchi kufikia uchumi wa kati
.
No comments:
Post a Comment