Mhadhiri Mkuu wa Chuo Kikuu cha
Dar es Salaam Profesa Haji Semboja amesema kuwa Serikali imepiga hatua
kubwa kutekeleza dhana ya kujitegemea katika maendeleo ya Taifa kuelekea
miaka 55 ya Uhuru wa Tanzania Bara.
Profesa Semboja amebainisha hayo
leo Jijini Dar es Salaam wakati wa mahojiano maalum na mwandishi wa
habari hizi kuhusiana na hatua mbalimbali ambazo Serikali ya awamu ya
Tano imezifanya.
Ameeleza kuwa Serikali ya Awamu
ya Tano chini ya Uongozi wa Rais John Pombe Magufuli imeweka kipaumbele
katika kusimamia matumizi yake na kuongeza ukusanyaji mapato na kubadili
mifumo ya kisera pamoja na kupunguza kutegemea misaada ya nje.
“Wakati wa Uhuru hayati Baba wa
Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliweka kipaumbele katika
kupambana na Ujinga, Maradhi, Umaskini na Rushwa, na hilo limeendelea
katika awamu zote nne na hivyo kwa nyakati tofauti Taifa limeweza
kusonga mbele na na mfumo wa ujamaa na kujitegemea pia ulitufanya
kutambulika vyema Duniani,” Alisema Profesa Semboja.
Aidha amesema kuwa kuanzia mwaka
1961 Serikali zetu za awamu tano zimejikita katika kuijenga Jamii pamoja
na soko Huria kwa ujumla.
Kwa upande wa maboresho katika
Utumishi wa Umma anasema kuwa uwajibikaji ulikuwa umedorora lakini kwa
sasa umerudi katika hali nzuri kutokana na usimamizi kuwa bora na pia
idadi ya watumishi imeongezeka na Ubora wa elimu umekuwa wa hali ya juu.
Aidha anaongeza kuwa hali ya kiuchumi na afya imeboreka na kuzidi kufanya maendeleo ya jamii kuwa bora zaidi.
Maadhimisho ya miaka 55 ya uhuru
mwaka huu yanafanyika tarehe 09/11/2016 katika viwanja vya Uhuru jijini
Dar es Salaam huku kauli mbiu ikiwa ni “Tuunge Mkono Jitihada za
Kupingaji Rushwa, Ufisadi na Kuimarisha Uchumi wa Viwanda kwa Maendeleo
Yetu”.
No comments:
Post a Comment