KWA MAONI AU USHAURI E-mail: inocomm2014@gmail.com, PIGA SIMU: 0714555668

www.utt-pid.org


TEMBELEA: www.utt-pid.org

September 24, 2018

TAARIFA MUHIMU TOKA BODI YA MIKOPO YA WANAFUNZI WA ELIMU YA JUU (HESLB)

Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) inapenda kuwataarifu waombaji wa mikopo kwa mwaka wa masomo 2018/2019 na umma kwa ujumla kwamba imetangaza orodha ya baadhi ya waombaji mikopo ambao fomu zao za maombi ya mikopo zina upungufu ili waweze kufanya marekebisho kwa njia ya mtandao https://olas.heslb.go.tz kwa siku saba (7) kuanzia Jumatatu  Septemba 24 hadi Jumapili  Septemba 30, 2018.

Katika kipindi hicho waombaji wote wa mikopo ambao fomu zao zina upungufu wa baadhi ya taarifa na nyaraka zao ama za wadhamimi wao, watapaswa kusoma majina yao kwenye orodha iliyowekwa kwenye tovuti ya HESLB www.heslb.go.tz na kisha kuingia kwenye mtandao wa maombi ya mikopo ili kufanya masahihisho kwa kufuata hatua zilizowekwa na baada kukamilisha, waziwasilishe ndani ya muda uliopangwa bila kutuma kwa njia ya EMS.

Nyaraka zote zinazokosekana ikiwa ni pamoja na vyeti vya kuzaliwa au vya vifo vya wazazi, kurasa za taarifa na saini za mwombaji na/au mdhamini wake zinapaswa kujazwa kwa ukamilifu, kuwa ‘scanned’ na kisha kupakiwa kwenye mtandao baada ya kuthibitishwa na mamlaka husika.

Zoezi la Uhakiki wa Taarifa za Waombaji wa mikopo
Baada kukamilika kwa muda wa kupokea maombi ya mikopo Julai 31, 2018, HESLB ilikuwa imepokea jumla ya maombi 78,833 ambapo baada ya uhakiki, HESLB ilibaini jumla ya waombaji zaidi ya 25,000 fomu zao za maombi zikiwa na upungufu wa nyaraka na uthibitisho wa kuwezesha kuendelea na hatua inayofuata ya kupangiwa mikopo katikati ya mwezi Oktoba, 2018.

Hitimisho
Kwa taarifa hii pia tunapenda kuwakumbusha waombaji wa mikopo ambao wamo katika orodha hiyo yenye upungufu wa taarifa kusoma kwa umakini na kurekebisha kasoro hizo ili waweze kupangiwa mikopo. 

Aidha tunawatahadharisha dhidi ya matapeli wanaoweza kutumia taarifa hiyo kuwalaghai waombaji mikopo kuwa wanaweza kuwasaidia kupata mikopo. Tangazo maalum na mwongozo wa marekebisho vinapatikana katika tovuti ya HESLB (www.heslb.go.tz).

Iwapo wana maswali, wawasiliane nasi kupitia:
Simu:   0736665533 au 022 5507910

Taarifa hii pia inapatikana kwenye tovuti ya HESLB www.heslb.go.tz

Imetolewa na:
Mkurugenzi Mtendaji
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu

HABARI ZILIZOPO KATIKA MAGAZETI YA LEO JUMATATU SEPTEMBA 24

September 14, 2018

TUME YA TAIFA YA UCHAGUZI (NEC) YATANGAZA UCHAGUZI MDOGO WA UDIWANI KATIKA KATA 37

Mwandishi wetu
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetangaza uchaguzi mdogo wa udiwani katika kata 37 za Tanzania Bara zilizopo katika Halmashauri 27 na mikoa 13 ya Tanzania Bara,  utakaofanyika tarehe 13 Oktoba mwaka huu.

Akitangaza uchaguzi huo, Mwenyekiti wa NEC Jaji wa Mahakama ya Rufaa Semistocles Kaijage, alisema fomu za uteuzi wa wagombea katika uchaguzi huo zitatolewa kati ya tarehe 15 hadi 21 Septemba, mwaka huu.

Alisema uteuzi wa wagombea utafanyika tarehe 21 Septemba, mwaka huu wakati kampeni za Uchaguzi zitafanyika kuanzia tarehe 22 Septemba hadi tarehe 12 Oktoba mwaka huu.

Jaji Kaijage alifafanua kuwa uchaguzi huo unafuatia Tume kupokea taarifa ya uwepo wa nafasi wazi za udiwani kwenye kata hizo kutoka kwa Waziri mwenye dhamana na Serikali za Mitaa kwa kutumia kifungu cha 13(1) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa.

“Baada ya kupokea taarifa hiyo na kwa kuzingatia masharti ya kifungu cha 13(3) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa; Tume ina utaarifu umma kuhusu kuwepo kwa Uchaguzi mdogo katika Kata hizo thelathini na saba (37).”, alisema Jaji Kaijage.

Kufuatia uchaguzi huo, Mwenyekiti huyo wa NEC alivialika Vyama vya Siasa, Wadau wote wa Uchaguzi na Wananchi kwa ujumla kushiriki katika Uchaguzi huo.

Aliongeza kwa kuviasa Vyama vya Siasa na Wadau wa Uchaguzi kuzingatia matakwa ya Katiba, Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Kanuni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa (Madiwani), 2015, Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2015 na maelekezo yote yaliyotolewa au yatakayotolewa na Tume wakati wote wa Uchaguzi huo.

Wakati huo, Tume ya Taifa ya Uchaguzi imewateua Madiwani watatu Wanawake wa Viti Maalum kujaza nafasi wazi za madiwani katika Halmashauri tatu za Tanzania Bara.

Akitangaza uteuzi huo, Mwenyekiti wa NEC Jaji wa Mahakama ya Rufaa Semistocles Kaijage, aliwataja madiwani hao kuwa ni Halima Salum Kisenga (CCM) wa Halmashauri ya Wilaya ya Kigamboni.

Wengine walioteuliwa ni Emmy Anania Shemweta kupitia CCM katika Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto na Nuru Mwalimu Chuma kupitia Chama cha Wananchi (CUF) katika Halmashauri ya Manispaa ya Ilala.

Jaji Kaijage alisema uteuzi huo umefanyika baada ya kupokea taarifa kutoka kwa Waziri mwenye dhamana ya Serikali za Mitaa, ambaye aliitarifu Tume kuwepo kwa nafasi wazi kupitia vyama hivyo baada ya walioteuliwa kufariki dunia na kujiuzulu.

HABARI ZILIZOPO KATIKA MAGAZETI YA LEO IJUMAA YA SEPTEMBA 14

September 13, 2018

MGOMBEA CHADEMA UKONGA AHOFIA KUTEKWA

Mgombea ubunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) jimbo la Ukonga jijini Dar es salaam Asia Msangi amesema miongoni mwa changamoto anazokutana nazo kuelekea uchaguzi wa marudio jimbo hilo utakaofanyika siku ya jumapili ya  septemba 16, ni hofu ya kutekwa na watu wasiojulikana.

Akizungumza katika kituo cha EATV leo, mgombea huyo wa CHADEMA amesema kupitia viongozi wa juu wa chama chake wamepokea taarifa juu ya uvumi wa kutaka kutekwa siku moja kabla ya zoezi la kupiga kura.

“…Baadhi ya changamoto kwenye uchaguzi huu wa marudio ninazokutana nazo .., kuna baadhi ya watu wetu wanatishiwa kutekwa na kuna mwingine alitekwa ila kwa ushirikiano na mwenyekiti jana amepatikana.., lakini pia kupitia viongozi wa juu wa chama tumepokea taarifa ya mimi kutaka kutekwa kabla ya jumamosi na hili jambo tutalifikisha polisi. ” Amesema Asia Msangi

Aidha Asia Msangi amesema licha ya  miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na Chama cha Mapinduzi (CCM) kupitia seikali ya awamu ya tano ikiwemo reli ya kisasa (SGR), ununuaji wa ndege pamoja na Shirika la ndege la Tanzania ATCL anaamini miradi hiyo haiwezi kuwa kikwazo cha kutoshinda uchaguzi wa jimbo hilo.

“ Licha ya miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Rais Magufuli bado maisha ya mwananchi mmoja mmoja wa jimbo la ukonga ni magumu.., hiyo miradi haiakisi chochote.., wananchi wa ukonga hawawezi kunufaika..”Ameongeza Asia Msangi

Uchaguzi wa jimbo la Ukonga unarudiwa kufuatia aliyekua Mbunge wa jimbo hilo kupitia CHADEMA Mwita Waitara kutangaza kujivua nafasi hiyo Julai 28 mwaka huu kwa madai ya kuwa na mgogoro na Mwenyekiti wa chama hicho Freeman Mbowe.

SERIKALI KUWEZESHA VITUO VYA UTAFITI ILI KUONGEZA UZALISHAJI WA AINA MPYA WA MBEGU BORA

Na Mathias Canal-WK, Arusha
Serikali imeahidi kuendelea kuwezesha vituo vyake vya utafiti kote nchini kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa aina mpya za mbegu bora za mazao mbali mbali.

Kauli hiyo imetolewa na Mhe Dkt Charles Tizeba Waziri wa Kilimo, wakati akifungua mkutano wa siku mbili wa wadau wa mbegu ambapo ni mjumuiko wa Jumuiya ya Wafanyabiashara ya Mbegu (TASTA), TOSCI, USAID East Africa Trade Investment Hub, AGRA-MIRA Project, AATF, ASA na TPRI kwa kushirikiana na wizara ya Kilimo na wadau wengine wa maendeleo unaofanyika katika Ukumbi wa Mount Meru Hotel Jijini Arusha.

Alisema kuwa katika kuhakikisha kuwa Wizara ya kilimo inafikia hatua ya kuwa na uzalishaji Wa aina mpya za mbegu bora za Mazao mbalimbali tayari serikali imechukua hatua ya kuanzisha Taasisi ya Utafiti Wa kilimo - TARI kwa lengo la kuboresha utendaji wa kitafiti ili kuleta tija katika ugunduzi wa aina mpya za mbegu.

Alisema kuwa TARI itasaidia kuongeza uzalishaji wa mbegu bora hapa nchini na hivyo kuwa na matokeo chanya ya uhakika wa chakula katika ngazi ya kaya na Taifa kwa ujumla pia kuongeza kipato kutokana na ziada.

Dkt Tizeba alisema kuwa Mpango wa Kuendeleza sekta ya Kilimo awamu ya pili – ASDP II ambao Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli ameuzindua hivi karibuni unasisitiza masuala ya uendelezaji wa kilimo chenye tija, Kilimo biashara chenye kuboresha mapato ya mkulima na kilimo  kinachomhakikishia mkulima usalama wa chakula na lishe.

"Haiwezi kuwa rahisi kuongeza uzalishaji wa kilimo hapa nchini kama msingi wa kilimo ambao ni uzalishaji wa mbegu bado tutakuwa tumeuacha nyuma pasina kuweka msisitizo hapo, hivyo tunapaswa kutazama upya namna bora ya kupunguza gharama ya mbegu" Alikaririwa Mhe Dkt Tizeba na kuongeza kuwa

"Baada ya serikali kujitoa katika uendeshaji wa biashara mbalimbali na kuruhusu sekta binafsi kufanya biashara, hii ilitoa fursa kwa sekta binafsi kushiriki katika tasnia mbalimbali ikiwemo hii ya mbegu, lengo kuu la dhana hii ya ushirikishaji wa sekta binafsi na ile ya umma (PPP) ni kuwezesha na kuhakikisha kwamba maslahi mapana ya wakulima yanalindwa na mazingira ya biashara yanaboreshwa ili wakulima na sekta binafsi wote wafaidike na jitihada wanazozifanya"

Waziri Tizeba aliongeza kuwa Ili kutekeleza lengo la kuongeza tija na uzalishaji katika sekta ya mbegu, Wizara ya Kilimo kupitia Sheria ya Mbegu ya Mwaka 2003, imeweka mifumo mbalimbali ya namna ya kutoa na kufikisha huduma kwa wakulima kwa kushirikiana na sekta binafsi kwa lengo la kuboresha huduma hizo ili kuongeza kasi ya ukuaji wa maendeleo ya wakulima.

Alizitaja jitihada hizo kuwa ni katika kutekeleza majukumu ya pamoja katika ubia baina ya sekta ya umma na ile ya binafsi. "Lakini kwa bahati mbaya juhudi hizi hazijazaa matunda yaliyotarajiwa na ndiyo maana mpaka sasa bado tunakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo uzalishaji mdogo wa mbegu, uwepo wa mbegu zisizokidhi viwango vya ubora sokoni na kutegemea mbegu za kuagizwa kutoka nje. Hali hii tunatakiwa kuondokana nayo na kuhakikisha tunazalisha mbegu za kutosha mahitaji ya ndani na ziada kuuza nje" Alisistiza Dkt Tizeba

Aidha, alidema juhudi mbalimbali zinaendelea kufanyika kati ya Serikali na Sekta binafsi katika kupambana na uwepo wa mbegu zisizokidhi viwango vya ubora sokoni. Miongoni mwa juhudi hizo ni kuweka karatasi yenye maelezo na utambulisho ‘label’’ katika vifungashio vya mbegu. "Hii ni sehemu ya utekelezaji wa Sheria ya Mbegu ya mwaka 2003 ambapo utekelezaji wake umekuwa na changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na malalamiko ya wafanyabiashara kudai kuwa hizo ‘lebel’ zinaongeza gharama. Hivyo napenda kuchukua fursa hii kuwafahamisha wadau wote wa sekta ya mbegu kuwa hilo ni takwa la kisheria hivyo ni budi sote tulizingatie" Alisema

MWISHO.