Siku moja baada ya kufukuzwa uwaziri, Mbunge wa Muleba Kusini
(CCM), Profesa Anna Tibaijuka amewasili jimboni kwake na kusema, “Bwana
alitoa na Bwana ametwaa.”
Profesa Tibaijuka alivuliwa uwaziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya
Makazi na Rais Jakaya Kikwete juzi kutokana na kuhusika kupokea fedha
katika akaunti binafsi.
Baada ya kuwasili na kupokewa kwa maandamano, Profesa Tibaijuka
aliwaomba wananchi kukaa kimya kwa dakika moja ili kumkumbuka katibu
wake wa jimbo aliyefariki dunia wakati sakata hilo likijadiliwa bungeni.
Profesa Tibaijuka aliyepokewa kwa msafara wa magari kutoka Uwanja wa
Ndege wa Bukoba, aliwaeleza wananchi kuwa ilikuwa ni lazima kutafuta
msaada kwa watu wengi ili aweze kuwasomesha watoto anaowasaidia kielimu.
“Kuna suala la escrow, zamani kulikuwa na aspro ambayo ilikuwa ni dawa
ya kweli, sasa suala hili limefikia tamati hamkunichagua ili nikawe
waziri, ni sawa na kusema Bwana alitoa na Bwana ametwaa,” alisema
Profesa Tibaijuka.
Aliambatana na mtoto wa kike akisema ni mmoja wapo wa wanafunzi wasio na
uwezo anaowasomesha katika Shule ya Babro Johanson, inayotajwa kuwa
ndiyo iliyopokea Sh1.6 bilioni alizoingiziwa katika akaunti yake
binafsi, katika Benki ya Mkombozi.
Profesa Tibaijuka alitumia muda mfupi kuelezea suala la kuhusishwa
katika kashfa ya Akaunti ya Tegeta Escrow akisema Taifa lina changamoto
ya kupata elimu bora na wapo viongozi wachache kama yeye wenye moyo wa
kusaidia masuala ya elimu.
“Teknolojia sasa imekua, naamini mlikuwa mnafuatilia mambo yalivyokuwa
yanakwenda, yalikuwa ni mambo makubwa, kazi ya uwaziri nisingeipata bila
nyinyi wananchi. Nilikuwa na majukumu mengi, sasa nitapata muda wa
kukaa jimboni.
“Taifa bado lina changamoto ya kupata elimu bora, hiyo shule mnayoisikia
ada yake kwa mwaka ni zaidi ya Sh4 milioni, hivyo lazima nitafute mtu
wa kunisaidia. Hakuna mtoto wangu hata mmoja anayesoma kwenye shule
hizo,” alisema Tibaijuka.
Huku hotuba yake ikikatizwa na watu waliokuwa wakishangilia, Profesa
Tibaijuka aliwaonya wanaotaka kulinyemelea jimbo hilo kuwa yuko ‘fiti’
na anawasubiri kukutana nao ulingoni.
Alisema atakuwa tayari kufanya kazi katika maeneo yanayoongozwa na vyama
vya upinzani jimboni kwake akiamini kuwa pia wapo wanachama wa CCM.
No comments:
Post a Comment