KWA MAONI AU USHAURI E-mail: inocomm2014@gmail.com, PIGA SIMU: 0714555668

www.utt-pid.org


TEMBELEA: www.utt-pid.org

August 20, 2015

DR MAGUFULI NA LOWASSA WALA VIAPO MAHAKAMA KUU VYA KUWANIA URAIS MASISHA


MGOMBEA urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli pamoja na mwenzake kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), chini ya mwamvuli wa Ukawa, Edward Lowassa, jana walifika mahakama kuu kanda  ya  Dar  es  Salaam kwa  ajili  ya   kusaka viapo vya mahakama kuthibitisha rasmi kuwania nafasi hiyo.

Magufuli na Lowassa kwa sasa wamekuwa mahasimu wa kisiasa tangu waziri mkuu huyo wa zamani alipotangaza kuihama CCM baada ya mchakato wa urais uliofanyika mjini Dodoma Julai mwaka huu.

Wagombea hao walikwenda jana Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam na kupewa fomu kila mmoja kwa wakati wake ya kumthibitisha kuwania nafasi hiyo ya juu katika  uongozi wa nchi.

Wagombea hao walithibitisha fomu hizo mbele ya Jaji Sakieli Kihiyo kwa matakwa ya kanuni za uchaguzi wa Rais na Bunge za mwaka 2015.

MAGUFULI NA SAMIA
Dk. Magufuli alikwenda  mahakamani hapo akiwa ameandamana na mgombea mwenza wake, Samia Suluhu Hassan  mbele ya Jaji Kihiyo saa tano na walikaa katika chumba cha mahakama kwa zaidi ya saa moja kwa ajili ya kusaini.

Baada ya kumaliza kuapa na kusaini Dk. Magufuli alitoka nje ya mahakama na kuzungumza kwa kifupi na wanahabari.

“Katika fomu ya kugombea nafasi ya urais inaeleza kwamba mtu anayetaka kushika madaraka makubwa azingatie kanuni na sheria zilizoainishwa .

“Kilichonileta hapa leo (jana) ni kukamilisha sehemu ya kanuni na sheria, kukagua fomu kwa ukamilifu na kusaini kiapo, naomba Watanzania waniombee,”alisema na kuondoka.

LOWASSA ATUA
Waziri Mkuu Mstaafu, Lowasa alifika eneo la mahakama saa saba adhuhuri na kuelekea moja kwa moja katika chumba cha mahakama kwa ajili ya kuapa na kusaini fomu ya kugombea urais.

Lowassa alichukua nusu saa kumaliza mchakato huo na kutoka na alipotakiwa kuzungumza na waandishi wa habari alisema hawezi kusema chochote.

“Siwezi kusema lolote, tusubiri Tume ya Uchaguzi ikinipitisha nitazungumza,”alisema kwa kifupi Lowassa.

MSAJILI MAHAKAMA KUU
Akitoa ufafanuzi kwa waandishi wa habari Msajili wa Mahakama Kuu John Kahyoza, alisema katika fomu za kugombea udiwani, ubunge na urais kuna kipengele cha tamko au kiapo cha kisheria cha mgombea.

“Leo wagombea urais wamekuja kuthibitisha kwa kiapo waliyoyajaza katika fomu ya kugombea nafasi hiyo ni sahihi, wamefanya hivyo kwa matakwa ya kanuni za uchaguzi na Bunge za mwaka 2015.

“Miongoni mwa wanayothibitisha ni kwamba wao ni raia wa Tanzania, wametimiza umri unaohitajika kisheria, hawajawahi kutiwa hatiani na kufungwa kwa kosa lolote ikiwemo kukwepa kodi.

“Fomu ikisharudishwa na kubainika kwamba miongoni mwa waliyoapa walisema uongo ni kosa la jinai hivyo aliyeapa anastahili kuchukuliwa hatua,”alisema.

Alisema madiwani na wabunge wanatakiwa kuapa mbele ya hakimu lakini haikueleza ni hakimu wa mahakama gani hivyo wanaweza kuapa kwa hakimu wa mahakama yoyote.

Alipoulizwa sababu ya Dk. Magufuli kutumia zaidi ya nusu saa, Kahyoza alisema wagombea urais walitakiwa kupita katika mikoa kumi kwa ajili ya kusaka wadhamini hivyo fomu zinatakiwa ziwe 40.

“Kundi la kwanza lililoingia la Dk. Magufuli lilikuwa na fomu zote 40, zikathibitishwa na kusainiwa.

“Kundi la pili la Lowassa waliingia na fomu zao nne, nikawauliza wakajibu ndizo walizoelekezwa, nikawashauri wakaongeze mbili, walifanya hivyo zikathibitishwa na kusainiwa.

“Kwa maana hiyo fomu 34 hazikuingia kwa ajili ya kusainiwa, sisi hata mgombea akija na fomu moja anasainiwa,”alisema na kuongeza kwamba hiyo ndiyo sababu iliyofanya mmoja atumie muda mwingi na mwingine atumie muda mfupi
Mpekuzi

No comments:

Post a Comment