HAMFREY POLEPOLE AMGALAGAZA VIBAYA MCHUNGAJI MSIGWA KWENYE MDAHARO |
Hamfrey Polepole na Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter
Msigwa wamekabana kwa hoja kali kuhusu uamuzi wa Chadema na Ukawa kwa ujumla
kumpokea Edward Lowassa na kumpa nafasi ya kugombea Urais.
Polepole na Msigwa walikutana jana katika kipindi cha ‘Mada
Moto’ kinachorushwa na kituo cha runinga cha Chanel Ten kujadili mada
iliyotajwa kama ‘Lowassa Ndani ya CCM’.Polepole alionesha msimamo wake wa
kumkataa Edward Lowassa kuwa sio kiongozi sahihi aliyepaswa kuungana na Ukawa
katika safari yao ya kutaka kuongoza dola na kupata katiba mpya ya wananchi kwa
kuwa ana tuhuma nzito zilizompa madoa.
Aliongeza kuwa dhana ya upinzani na mwenendo wa Ukawa
ulipotea pale walipomkaribisha Lowassa huku wakisahau kuwa ni miaka michache
iliyopita walizunguka nchi nzima kuwaaminisha watanzania kuwa ni fisadi na kwamba
wana ushahidi wa kutosha.
Polepole ambaye alikuwa mjumbe wa iliyokuwa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba iyoongozwa na Jaji Warioba, alisema kuwa Ukawa iliundwa
kwa madhumuni ya kutetea Katiba ya Wananchi na sio kwa lengo la kisiasa kama
ilivyo sasa.
Alisema kuwa Edward Lowassa hana msimamo thabiti kwenye
maamuzi yake kuhusu Katiba anayoitaka kwa kuwa aliwahi kumhoji awali akasema
anahitaji muundo wa serikali tatu lakini baadae alimfuata na kumueleza kuwa amebadili
anataka muundo wa serikali mbili.
“Lowassa niliongea naye wakati huo nakusanya maoni kuhusu
katiba mpya, mara ya kwanza alisema anataka serikali tatu na akaandika kwenye
kumbukumbu maalum za bunge. Lakini baadae alinifuata tena na kubadili msimamo wake
akitaka serikali mbili,” alisema Polepole.
Aliasema kilichomshangaza zaidi kwa Lowassa ni pale
alipopendekeza kuwa anataka muundo wa serikali mbili na kwamba serikali hizi
mbili ziwe na uhusiano wa kijeshi pekee.
Akiendelea kutetea hoja yake ya kumpinga Lowassa, PolePole
alisema kuwa amewahi kufanya kazi na Lowassa na kwa undani kabisa aligundua
kuwa ni mbinafsi.
“Watanzania mnatakiwa kufahamu kuwa mnapokutana na Lowassa,
Ninyi sio kitu bali kitu ni Lowassa,” alisema.
Mjadala huo ulitawaliwa na mivutano binafsi iliyowalazimisha
kutoka nje ya mada mara kadhaa hususan baada ya Mchungaji Msigwa kutoa tuhuma
za Polepole hadharani kisha akampa nafasi ya kujitetea.
Baada ya PolePole Kujitetea kufuatia tuhuma hizo, Mchungaji
Msigwa alimueleza kuwa alichokifanya ndio kinaitwa ‘natural justice’ ambayo
Edward Lowassa hakupewa wakati ule.
Akizijibu hoja za Polepole huku kukiwa na majibishano ya
hapa na pale, Mchungaji Msigwa alikiri kuwa yeye ni mmoja kati ya wanachama wa
Ukawa waliomsema sana Edward Lowassa na kumuita fisadi lakini sasa ameamua
kukaa kimya.
“It’s true tulisema. Hata mimi nilisema, it’s true I can’t
deny it. Lakini hata Joe Biden (Makomo wa pili wa Marekani) alikuwa anamsema
Obama kuwa ‘he does not fit for Commander in Chief, lakini alipochaguliwa
wakafanya kazi pamoja.
Hatuwezi kusema kana kwamba Lowassa ndiye muovu kuliko
mtanzania yeyote hapa nchini,” alisema.
Aliongeza kuwa kitu kikubwa alichojifunza kwa Lowassa na
kumfanya amheshimu sana, ni moyo wa uvumilivu na kukaa kimya hata pale
alipokuwa akitukanwa kila kona na kuitwa Fisadi.
Alisema moyo huo wa uvumilivu hata watumishi wengi wa Mungu
hawana.
Alifafanua kuwa katika ulimwengu wa siasa ni kawaida kufanya
kazi na mwanasiasa ambaye awali ulikuwa ukimpinga sana kwa kuwa muda ukifika
akaamua kubadilika mambo hubadilika pia.
Msigwa alisema kuwa chama chao ni chama cha demokrasia na
maendeleo na kwamba hilo ndilo limewapelekea kumfungulia mlango Edward Lowassa
baada ya kumhoji na kumuelewa.
Alipinga hoja ya Polepole kuwa Lowassa ana mapesa mengi
ambayo ameyapata kwa njia zisizofahamika, Msingwa alisema kuwa maelezo hayo
hutolewa bila kuelezewa kwa undani kama ana pesa nyingi kuliko nani
(serikalini).
“Unasema Lowassa ana mapesa mengi, ni kama vile unajua
akaunti zote za Lowassa zina shilingi ngapi. Na husema ana fedha nyingi kuliko
nani?”
Aliwataka watanzania kutomchukulia Lowassa kama vile ndiye
mtanzania mwenye dhambi nyingi kuliko wote bali wajikite katika kuangalia nia
yake ya dhati ya kuleta mabadiliko ya kweli nchini.
Alisisitiza kuwa Chadema hawana muda wa kumsafisha Lowassa
kwa kuwa umati uliofurika kumsindikiza kuchukua fomu ya kugombea urais katika
ofisi za Tume ya Uchaguzi Mkuu (NEC) inaonesha jinsi ambavyo watanzania wana
Imani naye.Alisema kuwa kwa mujibu wa tafiti zilizofanyika hivi karibuni
zinaonesha kuwa ni asilimia 5 hadi 8 tu ya watanzania ambao wamejikita katika
kufahamu ufisadi wa wagombea na kwamba umma mkubwa unataka mabadiliko kwa kuwa
wamechoshwa na muundo.
Msigwa alimtaka PolePole kutomzungumzia Lowassa pekee kwa
mtazamo hasi bali azungumzie pia ubaya wa Magufuli ambaye anaunga mkono muundo
wa serikali mbili kinyume na ile anayoisapoti Polepole na Tume Ya Mabadiliko Ya
Katiba.
Na kwamba yapo maovu mengi kwenye wizara ya ujenzi
inayoongozwa na Magufuli.
Akijibu hoja ya Msigwa, PolePole alisema kuwa yeye ni mmoja
kati ya watu walioishawishi CCM kukata majina ya wagombea wote wenye madoa
katika mchakato wa kura za maoni kumpata mgombea urais.
Alisisitiza kuwa ingawa CCM ni chama chake, hatampigia
kampeni Magufuli hadi pale ambapo rufaa zilizokatwa dhidi ya wagombea
waliotangazwa kuwa washindi wa kura za maoni ziangaliwe na wote wenye madoa
waondolewe.
“Ili niwaunge mkono, CCM mnatakiwa kuwakata watu wote katika
mchakato wa kura za maoni wanaotuhumiwa kwa kashfa mbalimbali,” alisema
Polepole ambaye awali alitangaza kutembea nchi nzima kuhamasisha watu
wasimchague Lowassa.
PolePole alitoa ushauri pia kwa chama chake cha CCM ili kiwe
tofauti na makosa yaliyofanywa na wahasimu wao wa kisiasa, Ukawa.“Viongozi wa
CCM, kama Ukawa wamewachukua watuhumiwa wamewakubali. Nyie onesheni uongozi na
utofauti mhakikishe mnawakata wagombea wote wanaotuhumiwa. Onesheni kwamba
watuhumiwa hawana nafasi kwenu.
Vijimambo
No comments:
Post a Comment