MGOMBEA urais wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kupitia Chama
cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa, amepata
kashikashi baada ya polisi kumzuia kumzika mwasisi wa Chama cha TANU na
CCM, Peter Kisumo, kwa madai kuwa wamepata maagizo kutoka juu.
Msafara wa Lowassa ulioanzia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa
Kilimanjaro (KIA), ulikutana na kizuizi cha polisi katika Kijiji cha
Maroro, kilomita moja kutoka Mwanga kuelekea Ugweno, ambako Kisumo
alizikwa jana.
Lowassa akiongozana na viongozi mbalimbali, akiwamo Mwenyekiti wa
NCCR-Mageuzi, James Mbatia, Mwenyekiti wa Chadema Kilimanjaro, Philemon
Ndesamburo na Mbunge wa Vunjo, Augustine Mrema, walikuwa na msafara wa
magari na pikipiki zaidi ya 100.
Licha ya kwamba msafara wa kiongozi huyo ulitoka KIA ukiwa na magari
machache, idadi ya magari na pikipiki iliongezeka kadiri safari
ilipokuwa ikiendelea kutokana na baadhi kujiunga kila alipokuwa akipita.
KIZUIZI
Akizungumza na waandishi wa habari waliokuwapo kwenye msafara huo,
Mbatia alisema kuwa alizungumza na Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Ernest
Mangu na akawaruhusu kuendelea na safari, lakini Mkuu wa Polisi Mwanga
alikataa kutii agizo hilo.
“Nimeongea na IGP akiwa Kibondo, tukakubaliana na kutoa maelekezo kwa
RPC, lakini tuliporuhusiwa na kuanza kuondoka, ikaja amri kutoka kwa OC
CID akiwa huko juu msibani, ya kwamba hakuna kuruhusu msafara huo, kama
kupanda ni gari moja tu la Lowassa na langu,” Alisema Mbatia na
kuongeza.
“Lowassa ni Waziri Mkuu mstaafu, huwezi kusema eti iende gari moja tu, na pia siye viongozi wengine wanatunyima haki yetu.
“CCM sasa wameamua kuipasua nchi, Serikali ya CCM inatupeleka kwenye
hali ya kutozikana, wametuzuia kwenda kumzika mzee wetu Kisumo, kisa
woga tu.”
Wakati yote hayo yakiendelea, Lowassa na Ndesamburo, walikuwa kwenye magari.
Lakini hata hivyo, baada ya mazungumzo ya muda mfupi, hatimaye majira
ya saa 6:53 mchana, msafara huo uliofika eneo hilo saa 6:42,
uliruhusiwa kuendelea na safari wakitakiwa kuondoa bendera za Chadema
kwenye magari na pikipiki.
MTANZANIA
No comments:
Post a Comment