Baadhi ya washiriki wa Mkutano wa Mwaka wa Serikali Mtandao wakifuatilia mkutano huo leo jijini Arusha. |
…………………………………………………………………………………….
Na Aron Msigwa -Arusha
Serikali imezitaka
Wizara,Idara,Wakala na Taasisi mbalimbali kuanza kujiandaa na mageuzi
makubwa ya matumizi ya Mfumo mmoja wa Mawasiliano kupitia Serikali
Mtandao ili kupunguza gharama za uendeshaji na kuondoa urudufu wa mifumo
ya TEHAMA inayofanya kazi za aina moja serikalini.
Hatua hiyo ya Serikali imekuja
kufuatia kuwepo kwa mifumo ya TEHAMA ya kutolea huduma kwa umma katika
Taasisi mbalimbali za Serikali isiyoweza kuwasiliana na kubadilishana
taarifa jambo linalosababisha usumbufu kwa wanannchi wanapotakiwa
kuwasilisha taarifa za aina moja kwenye taasisi tofauti za serikali.
Akifungua Mkutano wa Serikali
Mtandao wa Makatibu Wakuu,Makatibu Tawala wa Mikoa, Wakurugenzi na
Watendaji Wakuu wa Taasisi na Wakala za Serikali leo jijini Arusha
Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue amesema kuwa mabadiliko hayo ni
Sehemu ya mpango wa Serikali wa kuhakikisha kuwa inawafikishia
wananchi huduma bora kwa haraka, gharama nafuu na mahali walipo.
Ameeleza kuwa hatua ya Tanzania
kuweka msukumo kwenye Serikali Mtandao haiepukiki kwa kuwa imelenga
kuboresha utendaji wa kazi ndani ya Serikali, kuongeza tija, ufanisi na
kasi ya ubadilishanaji wa taarifa ndani ya Serikali.
“Jambo hili la Serikali mtandao
tumeshalizungumza sana Serikalini kutokana na umuhimu wake tumekutana
watoa maamuzi kwa mara ya kwanza ili kufikia malengo ya Serikali mtandao
tuliyojiwekea kila mmoja achukue hatua kuhakikisha kuwa fursa zilizopo
zinatumika ipasavyo,tumeshaanza hakuna kurudi nyuma katika jambo hili”
Amesema Serikali imefanya
mageuzi makubwa katika uwekezaji wa miundombinu ya TEHAMA ikiwemo
uanzishaji wa Mkongo wa Taifa, Kituo cha Taarifa Serikalini (National
Data Centres) ili kuhakikisha kuwa huduma za Serikali zinapatikana kwa
urahisi, haraka,uwazi,gharama nafuu,wakati wowote na mahali popote
nchini.
“Serikali tumefanya uwekezaji
mkubwa kwenye miundombinu ya TEHAMA ikiwemo Mkongo wa Taifa (NICTBB),
Mtandao wa Serikali (GovNet),Vituo vya kitaifa vya Data na kutenga
Masafa ya Intaneti ya Serikali, hii yote ni kuwahakikishia wananchi
huduma bora za Serikali mtandao” Amesisitiza Balozi Sefue.
Amefafanua kuwa Serikali imeendelea kuboresha Sera na sheria, kutokana kutungwa kwa Sera ya TEHAMA ya mwaka 2003 na Mpango Mkakati wa Kitaifa wa Serikali Mtandao 2013 pamoja na sheria ya Elekroniki na Mawasiliano ya Posta (Elektonic and Postal Communicatins),Sheria ya Miamala ya Kielektroniki 2015 na Sheria ya Makaosa ya Mitandao ya mwaka 2015.
Ameongeza kuwa Serikali
inaendelea kujenga uwezo wake wa ndani ili kuondoa utegemezi wa
wakandarasi wa nje katika ujengaji wa mifumo ya TEHAMA hapa nchini ambao
huigharimu serikali fedha nyingi.
“Tunalo jukumu kubwa la
kuhakikisha tunaimarisha na kujenga uwezo wetu wa ndani ili kuondoa
utegemezi kutoka nje, wataalamu sasa tunao na tutaendelea kujenga uwezo
wetu wa miundombinu ya ndani ili kuwahudumia wananchi”
Ametoa wito kwa wataalam wa
Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Tume ya Mipango na Wakala
ya Serikali Mtandao kushirikiana katika kuhakikisha Serikali Mtando
inaingizwa katika mpango wa taifa wa miaka mitano.
Aidha, amezitaka Taasisi ambazo
zina kiwango kidogo cha utekelezaji wa Serikali mtandao kushirikiana na
Wakala ya Serikali Mtandao kuchukua hatua za haraka ili kuhakikisha
kuwa matumizi ya TEHAMA yanaleta ufanisi katika kujenga Serikali Mtandao
madhubuti.
“Taasisi za Serikali ambazo
bado zina kiwango kidogo cha utekelezaji wa Serikali Mtandao zinatakiwa
kuchagua jambo moja, kukubali kubadilika au kubadilishwa” amesisitiza
na kuongeza kuwa Serikali inaendelea kuzijengea uwezo taasisi hizo
ziweze kuendana na mabadiliko yaliyopo.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa
Arusha Bw.Felix Kijiko Ntibenda akiwakaribisha washiriki wa mkutano huo
jijini Arusha amesema kuwa kufanyika kwa mkutano huo ni mwanzo mzuri wa
kuelekea Serikali Mtandao Imara.
Amesema matumizi ya TEHAMA
katika shughuli za Serikali yameisaidia Serikali kuongeza ufanisi katika
shughuli mbalimbali ikiwemo utambuzi, tiba, ukusanyaji wa mapato ya
Serikali na huduma za matibabu.
Amesema kupitia mifumo ya
ukusanyaji wa mapato kwa njia ya mtandao mkoa wa Arusha anaouongoza
umenufaika kwa kiasi kikubwa kwa kuongeza mapato ya ndani na kufanikiwa
kupunguza vitendo vya wizi na ubadhirifu.
Awali akizungumza kuhusu
mkutano huo Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Serikali Mtandao (e Government
Agency) Bw. Jabir Bakari amesema kuwa mkutano huo umelenga kuongeza
ufanisi katika matumizi ya Rasilimali za TEHAMA nchini.
Amesema Serikali inaendelea
kufanya vizuri katika kufanikisha lengo kubwa la kufikisha huduma kwa
wananchi pia kufanikisha mpango wa kuwa na mfumo mmoja utakaowezesha
taarifa zote za wananchi kuwa katika sehemu moja.
Kuhusu mkutano huo Dkt.Jabiri
amesema kuwa washiriki watapata fursa ya kujadili masuala mbalimbali
ya ushirikiano katika kutekeleza jitihada za Serikali Mtandao nchini
pamoja na Kutafuta ufumbuzi wa changamoto za serikali mtandao zilizopo
nchini ili kuleta maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Aidha,amesema washiriki
watapata fursa ya kujifunza kutoka kwa wataalam wengine wanaohusika na
Serikali Mtandao kutoka nchi zinazofanya vizuri katika eneo la Serikali
mtandao zikiwemo India na Singapore.
Pia amesema mada mbalimbali
zitajadiliwa zikiwemo za usimamizi wa Serikali Mtandao nchini Tanzania,
Hali ya miundombinu ya Serikali mtandao na Utekelezaji wa Mpango wa
Uendeshaji wa Serikali kwa uwazi.
Mada nyingine zitahusu
uimarishaji wa uwazi na Mfumo wa Takwimu huria nchini Tanzania na
uimarishaji wa huduma za Serikali kupitia simu za mkononi na mifumo
inayotumika kutoa huduma kwa wananchi.
No comments:
Post a Comment