ESTHER MNYIKA NA MGENI SHABANI DAR ES SALAAM
MAMLAKA ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA) imezuia utengenezaji wa vipodozi tofauti 36 vya krimu na losheni ambavyo vimebainika kuwa na viambato vya steroids vilivyopigwa marufuku.
Vipodozi vilivyobainika kuwa na viambato vilivyopigwa marufuku ni pamoja na siri moisturizing cream lemon, cocoa butter krimu,siri moisturizing cream lemon,lovely body cream lemon, lovely body cream.
Uamuzi huo umechukuliwa baada ya kufanyika uchunguzi wa kina kwa matoleo 57 yaliyochukuliwa kwenye soko na viwanda vilivyovitengeneza.
Akizungumza na wandishi wa habari jana, Mkurugenzi Mkuu wa TFDA, Hiiti Sillo, alisema vipodozi hivyo vimetengenezwa na kampuni nne nchini pamoja na Afrika Kusini.
Alivitaja viwanda vilivyozuiwa utengenezaji huo kuwa ni Chemi & Cotex Limited vya Dar es Salaam ambavyo vimepigwa marufuku kuzalisha vipodozi sita huku Kiwanda cha Mamujee Product Limited cha Tanga kikizuiwa kutengeneza vipodozi 11.
Viwanda vingine ni Tanga Pharmaceutical & Plastic Limited ambacho kimezuiwa kutengeneza vipodozi 15,Tridea Cosmetics Limited cha Dar es Salaam (vipodozi 3) na Johnson & Johnson (pvt) Ltd, Rattray Road, East London, (Afrika Kusini).
“Steroids iliyowekwa ndani ya vipodozi hivyo ni dawa ambayo hutumika kutibu magonjwa ya ngozi ambayo mtu hutakiwa kutumia ndani ya wiki mbili kwa kufuata ushauri wa daktari,”alisema Sillo.
Alisema baadhi ya madhara yanayosababishwa na dawa hizo ni muwasho, kuvimba ngozi, ngozi kuwaka moto, ngozi kukatikatika na kupata chunusi kubwa kwenye ngozi.
“Mbali na kuwakataza kutengeneza pia tumefuta usajili wa vipodozi 31 vilivyokuwa tumevisajili na kuwaelekeza mameneja wa ofisi za kanda kufanya ukaguzi wa maeneo yao kwa kushirikiana na ofisi za halmashauri kuondoa sokoni vipodozi vyote vilivyohusika,”alisema Sillo.
No comments:
Post a Comment