Na Benny Mwaipaja, WFM, Dodoma
WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dkt.
Philip Mpango, ameliambia Bunge Mjini Dodoma, Leo, Juni Mosi, 2016
kwamba serikali imejipanga kuchukua hatua madhubuti zinazolenga kujenga
Taifa linalojitegemea kwa kukuza uchumi na kupunguza umasikini.
Amezitaja hatua hizo kuwa ni
pamoja na kusimamia na kufuatilia kwa ukamilifu utekekelezaji wa Mpango
wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano 2016/17 – 2020/21. Mpango huu
unajikita katika kujenga msingi wa uchumi wa viwanda na maendeleo ya
watu.
Amesema kuwa ili mpango huu uweze
kutekelezwa kwa ufanisi na kupata matokeo tarajiwa, ni dhahiri kuwa
zinahitajika rasilimali za kutosha, hususan rasilimali fedha.
“Wizara ya Fedha na Mipango kwa
kushirikiana na wadau wengine inalo jukumu la kuimarisha ukusanyaji wa
mapato ili kukabiliana na changamoto ya upungufu wa rasilimali fedha”
alisisitiza
Dkt. Mpango amesema kuwa Ilani ya
Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015-2020 imeweka bayana
majukumu ya Wizara ya Fedha na Mipango ya kuimarisha usimamizi na
ukusanyaji wa mapato, kupanua wigo wa vyanzo vipya vya mapato na
kusimamia kwa ufanisi matumizi ya fedha za umma kwa kuzingatia sheria,
kanuni na miongozo mbalimbali.
Amenukuu kauli iliyotolewa na
Waziri Mkuu, Majaliwa Kassim Majaliwa, alipokuwa anawasilisha hotuba
yake katika Bunge, Aprili 25 mwaka 2016, aliposema kuwa mwelekeo wa
Serikali ya Awamu ya Tano yenye falsafa ya HAPA KAZI TU, imelenga
kufikia kipato cha kati na kufanyika mapinduzi makubwa ya viwanda
yanayotegemea sana utulivu wa uchumi.
“Tutasimamia kikamilifu matumizi
ya vifaa na mifumo ya kielektroniki katika ukusanyaji wa mapato ili
kuongeza ufanisi na kudhibiti upotevu wa mapato” Aliongeza Dkt. Mpango
Amesema kuwa serikali
itarasimisha sekta isiyo rasmi kuingia katika mfumo wa kodi na hivyo
kupanua wigo wa kodi na Kuimarisha ufuatiliaji wa mapato yanayokusanywa
na taasisi na mamlaka mbalimbali za Serikali ili kuongeza ukusanyaji wa
mapato ya Serikali.
Dkt. Mpango amebainisha kuwa
watasimamia na kuimarisha ukusanyaji wa mapato yasiyo ya kodi na
kuboresha usimamizi wake chini ya Mamlaka ya Mapato Tanzania kutokana na
uzoefu na mifumo ya ukusanyaji iliyopo nchi nzima
“Tutaendelea kuchukua hatua za
kudhibiti na kupunguza misamaha ya kodi isiyo na tija na Kuendelea
kuimarisha usimamizi na kufanya ukaguzi wa mara kwa mara bandarini na
maeneo ya mipakani ili kuhakikisha kwamba kodi stahiki zinakusanywa”
aliongeza Dkt. Mpango.
Ametaja mikakati hiyo kuwa ni moja ya njia ya kupunguza utegemezi wa misaada kutoka nje ambayo imezidi kupungua kila mwaka.
Ametoa mfano wa mwaka wa fedha
unaoishia Juni mwaka huu ambapo hadi Machi, wadau wa maendeleo wametoa
shilingi bilioni 1,064.89 sawa na asilimia 46 ya fedha zote
zilizoahidiwa kutolewa na wadau hao hali iliyoathiri utekelezaji wa
miradi mbalimbali iliyokusudiwa
Ametaja sababu za hali hiyo kuwa
ni kupungua kwa misaada toka nje kunatokana na kujiondoa kwa baadhi ya
Washirika wa Maendeleo wanaochangia kupitia Misaada na mikopo ya
kibajeti na baadhi ya Washirika wa Maendeleo kupunguza ahadi zao.
“Wafadhili wanaochangia kupitia
misaada ya kibajeti walipunguza michango yao kutoka shilingi bilioni 660
mpaka shilingi bilioni 399 katikati ya mwaka wa fedha 2015/16 na
wengine kuhusisha utoaji wa fedha na masharti ambayo hayakuwemo katika
makubaliano ya awali” Aliongeza Dkt. Mpango
Alisema kuwa katika kushughulikia
changamoto hizo, Serikali inaendelea na mazungumzo na Washirika wa
Maendeleo ili kuhakikisha kwamba fedha zilizoahidiwa zinatolewa kwa
wakati.
WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dkt.
Philip Mpango, ameliomba Bunge, liidhinishie Wizara yake kupitia mafungu
yote tisa ya kibajeti, jumla ya Shilingi Trilioni 8.7 kwa ajili ya
Matumizi ya Kawaida na shilingi Bilioni 791.99 kwaajili ya miradi ya
maendeleo.
Amesema kuwa Kati ya fedha
hizo,shilingi bilioni 45.45 ni kwa ajili ya Mishahara na shilingi
bilioni 8,671.04 ni kwa ajili ya Matumizi Mengineyo.
|
June 2, 2016
WIZARA YA FEDHA NA MIPANGO KUSIMAMIA UKUAJI WA UCHUMI KWA MAENDELEO YA NCHI
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment