Bodi
ya Wadhamini ya Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) imesema
kuwa haiwezi kuzungumzia lolote kuhusu hatma ya aliyekuwa Mkurugenzi
Mkuu wa shirika hilo, Dk Ramadhani Dau kwa vile si mwajiriwa wao.
Akizungumza
na mwandishi wa habari hizi jana kwa simu, Mwenyekiti wa Bodi hiyo,
Profesa Samwel Wangwe alisema bodi inashughulika na wafanyakazi wa sasa
katika shirika hilo na siyo walioondoka.
“Bodi
haiwezi kuchukua hatua dhidi yake (Dk Dau).Vyombo husika ndivyo
vitaamua kuhusu hilo,” alisema Profesa Wangwe alipoulizwa kuhusu hatma
ya Dk Dau ambaye alikuwa bosi na msimamizi mkuu wa menejimenti
iliyosimamishwa kazi.
Pia,
katika kipindi ambacho Dk Dau alikuwa mkurugenzi mkuu, aliyekuwa
Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi iliyopaswa kutoa idhini ya ujenzi wa
kila mradi uliopangwa alikuwa Abubakar Rajabu.
Profesa
Wangwe alisema hayo alipoulizwa kuhusu hatma ya Dk Dau baada ya bodi
hiyo juzi kuwasimamisha wakurugenzi sita wa shirika hilo na mameneja
sita kupisha uchunguzi wa tuhuma za ubadhirifu na matumizi mabaya ya
ofisi.
Dk
Dau amekuwa mkurugenzi mkuu wa NSSF kwa miaka kadhaa hadi Februari
mwaka huu alipoondolewa baada ya kuteuliwa na Rais John Magufuli kuwa
balozi, ingawa bado hajapangiwa nchi.
Katika
kipindi alichoondolewa NSSF, ripoti ya ukaguzi uliofanywa na kampuni ya
Ernst & Young kwa hisani ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali (CAG) ilivuja ikionyesha ubadhirifu wa fedha katika miradi
mikubwa ya ujenzi wa majengo ya kisasa yakiwemo ya mji mpya wa Kigamboni
jijini Dar es Salaam uitwao Dege Eco Village.
Miradi
mingine ambayo ilichunguzwa na CAG akatilia shaka ni ujenzi mradi wa
Arumeru, Arusha ambapo NSSF ilikubali kujenga majengo ya kisasa katika
viwanja vya mbia mwenzake kampuni ya Azimio Housing Estate Limited
ambavyo ekari moja ilithaminishwa kwa Sh1.8 bilioni.
Hata hivyo, mradi huo wenye thamani ya Sh7.2 trilioni ulisimamishwa Januri mwaka huu.
Machi
19, Rais John Magufuli alimteua Profesa Godius Kahyarara kuchukua
nafasi ya Dk Dau na Juni 28, Profesa Wangwe aliteuliwa kuwa Mwenyekiti
wa Bodi. Uteuzi wake ulianza Mei 30.
Bodi
ya NSSF, katika kikao cha 106 kilichoketi Julai 15, chini ya Profesa
Wangwe ilijadili ripoti mbalimbali na kufikia hatua ya kuwasimamisha
vigogo hao ikisema mbali ya ubadhirifu na matumizi mabaya ya ofisi pia
wanakabiliwa na tuhuma za kutofuata kanuni, sheria na taratibu za
manunuzi katika uwekezaji na usimamizi wa miradi, manunuzi ya ardhi na
ajira.
Wakurugenzi
waliosimamishwa ni Yacoub Kidula (Mipango, Uwekezaji na Miradi),
Ludovick Mrosso (Fedha), Chiku Matessa (Rasimali Watu na Utawala), Sadi
Shemliwa (Udhibiti Hadhara na Majanga), Paulin Mtunda (Ukaguzi wa
Mahesabu ya Ndani) na Crescentius Magori (Uendeshaji).
Mameneja
waliosimamishwa ni Amina Abdallah (Utawala), Abdallah Mseli
(Uwekezaji), John Msemo (Miradi), Davis Kalanje (Mhasibu Mkuu), Chedrick
Komba (Meneja Kiongozi Temeke) na Mhandisi John Ndazi ambaye ni meneja
mradi.
Taarifa
zaidi zilizopatikana zilieleza kuwa baadhi ya maofisa wa shirika hilo
walifikishwa juzi katika Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa
(Takukuru) kwa tuhuma ambazo hadi jana hazikuwa zimewekwa wazi.
Mkurugenzi
wa Mawasiliano Takukuru Mussa Misalaba alipoulizwa alisema hawezi
kusema ndiyo au hapana, lakini hiyo ipo chini ya taasisi hiyo.
“Siwezi
kukutajia majina kwamba nani na nani wanachunguzwa na Takukuru, sababu
kufanya hivyo ni kuwadhalilisha. Kwa kifupi hiyo ni kazi yetu,” alisema.
Aidha,
Profesa Wangwe alisema maofisa hao waliosimamishwa kazi juzi kupisha
uchunguzi wa tuhuma za ubadhirifu na matumizi mabaya ya ofisi,
watachunguzwa na vyombo kulingana na aina ya makosa yao.
Alipoulizwa kuhusu vyombo vinavyowachunguza maofisa hao alisema hafahamu ni vipi na ni vingapi.
“Vyombo vinavyohusika vitafanya uchunguzi kulingana na aina ya tuhuma zinazowakabili. Siwezi kusema ni vingapi,”alisema Profesa Wangwe.
Kwa
mujibu wa ripoti kamili ya CAG, Profesa Mussa Assad iliyowasilishwa
bungeni mjini Dodoma Aprili mwaka huu, kuna utata wa ardhi ya mradi mpya
wa mji wa Kigamboni unaojengwa na NSSF kwa ubia na kampuni ya Azimio
Housing Estate.
Ramani
ya mradi huo wenye thamani ya Dola za Marekani 653.44 milioni (Sh1.254
trilioni) inaonyesha utakapokamilika utachangia kubadili sura ya jiji la
Dar es Salaam kwani kutakuwa na nyumba za kifahari, majengo ya hoteli,
maduka makubwa, eneo la wazi la mapumziko, baa, shule, hospitali, kumbi
za mikutano, nyumba za ibada na migahawa.
Profesa
Assad katika ripoti hiyo alitilia shaka uhalali wa Azimio kumiliki
ekari 20,000 za ardhi ambazo imetoa kama sehemu ya asilimia 20 ya
mchango wake katika mradi huo na kwa kuanzia imetoa ekari 300.
“Ukaguzi
wa hatimiliki umeonyesha kuwa Azimio inamiliki viwanja viwili, kiwanja
chenye hatimiliki Na. 81828 chenye ukubwa wa hekta 1.98 na chenye
hatimiliki Na. 105091 chenye ukubwa wa hekta 114.11,” anasema CAG.
“Viwanja
vyote vinapatikana katika eneo la Rasi Dege ambavyo kwa pamoja
vilihamishiwa kwa Hifadhi Builders kutoka kwa Azimio kwa ajili ya Awamu
ya Kwanza ya mradi.
"Kwa
kutumia kizio cha ekari 2.47 kwa hekta, hatimiliki hizi zitakuwa na
ukubwa wa jumla wa ekari 286.74, pungufu ya ekari 13.26 kutoka kwenye
ekari 300 ambazo zilipangwa kwa ajili ya awamu ya kwanza ya mradi,” anafafanua CAG.
CAG
anasema katika kipindi chote cha ukaguzi wa mradi huo ulioanzishwa
mwaka 2014, hakuwahi kupatiwa hatimiliki za ardhi ambayo Azimio aliahidi
kutoa kama uchangiaji wa mtaji.
Vilevile,
CAG aliitaka NSSF kuhakikisha inakirejesha katika muda uliopangwa kiasi
cha Dola za Marekani milioni 20.1 (Sh43.9 bilioni) ambazo iliilipa
Azimio kwa ushauri wa ujenzi wa mradi wa mji wa Arumeru, Arusha.
“Katika
ukaguzi imeonekana Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii limepokea
upembuzi yakinifu wa mradi pendekezwa kutoka Azimio Housing Estate Ltd
kupitia barua yake ya Mei 16, 2013 yenye kumbukumbu Na.
Azimio/NSSF/Arumeru/13/5. Bodi ya Wadhamini iliidhinisha kuingiza katika
ubia ardhi iliyotolewa na kampuni ya Azimio katika mikoa ya Lindi,
Mtwara, Mwanza na Arusha kwa ajili ya uwekezaji unaofanana na huu,” anasema.
“Ada
ya ushauri kwa ajili ya kubuni mradi huo ni Dola za Marekani milioni
218.09 (Sh 468.9 bilioni) na ilipangwa Sh 2.4 bilioni zitumike katika
awamu ya upangaji wa mradi. Hata hivyo, kiasi hicho kiliongezwa hadi
kufikia Sh 102 bilioni bila ya idhini ya Bodi,” anaeleza.
Kwa
kuwa baadaye NSSF na Azimio walikubaliana kufuta mradi wa Arumeru wenye
thamani ya Sh 7.2 trilioni huku Sh43.9 bilioni zikiwa zimetolewa, CAG
ameitaka NSSF kuhakikisha mbia huyo anazirejesha katika muda wa miaka
mitatu kwa kuangalia riba iliyoko katika soko la wakati huo.
|
No comments:
Post a Comment