MKUU
wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali, Ernest Mangu amefunguka kuhusu
mambo juu ya utendaji wa jeshi hilo na kueleza kuwa wakati wowote
litamburuza mahakamani Katibu Mkuu wa Taifa wa Chama cha Wananchi (CUF),
Maalim Seif Shariff Hamad kwa kuhamasisha uchochezi visiwani Zanzibar.
Amebainisha kuwa jeshi hilo, kamwe halikandamizi wala kuonea chama chochote cha siasa, kwani limekuwa likitekeleza wajibu wake kwa kufuata sheria na taratibu zilizopo.
Amebainisha kuwa jeshi hilo, kamwe halikandamizi wala kuonea chama chochote cha siasa, kwani limekuwa likitekeleza wajibu wake kwa kufuata sheria na taratibu zilizopo.
Akizungumza
katika mahojiano yaliyofanyika kwenye kipindi cha Funguka,
kinachorushwa na Kituo cha Televisheni ya Azam jana, IGP Mangu alisema
hali ya siasa Zanzibar ilikuwa shwari katika chaguzi zote mbili na
kwamba machafuko na vurugu vilianza kutokea baada ya uchaguzi wa pili.
Alisema
vurugu hizo zilianza baada ya kubainika kuwa Maalim Seif, alikuwa
akifanya mikutano ya ndani na mingine ya chini kwa chini na wafuasi wake
katika maeneo ya Kaskazini na Kusini.
“Kwa
sababu ilikuwa ni mikutano ya ndani, Polisi hatukuona tatizo na wala
hatukumzuia, tuliona ni mwananchi anataka kuzungumza na wafuasi wake,
tukasema mwache aongee nao tu,” alisema IGP Mangu.
Alisema
baadaye jeshi hilo liligundua kuwa kiongozi huyo wa CUF, alikuwa
anawachochea wananchi waichukie serikali iliyopo madarakani na wapinzani
wao ambao ni Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kuwafanyia uhalifu.
Alisema
baada ya vikao hivyo vya Maalim Seif, visiwani humo kukaanza kuibuka
matukio ya vurugu kama vile mashamba kuchomwa moto na mazao kung’olewa.
“Haya mambo hayakutokea kabla ya vikao vya Seif, yalitokea baada ya vikao vyake,” alifafanua mkuu wa polisi.
Alisema
wafuasi hao walichochewa, kiasi cha kususa hadi shughuli za kijamii,
kama vile misiba na wakati mwingine ilifikia hatua ya kususa kuwauzia
bidhaa wafuasi wa CCM.
“Tukasema
kama wameona kugeuza biashara zao siasa, basi waendelee tu. Biashara
inadumu kwa sababu unatengeneza faida, sasa kama umeamua kuchagua wa
kumuuzia ni shauri yako. Hawa tuliwaacha kwa sababu tuliona hawana
makosa,” alisema.
Hata
hivyo, alisema jeshi hilo kamwe halikuwanyamazia wahalifu waliochoma na
kung’oa mazao kwenye mashamba ya wenzao, eti tu kwa kigezo cha ufuasi
wa chama au siasa.
“Hawa
tuliwakamata na wapo wengine tunaendelea kuwatafuta, watakapoacha ndio
hatutawatafuta. Wale wahalifu ndio tunaowatafuta. Pengine kwa sababu ya
siasa wanadhani Polisi tunawaonea wananchi tunawakamata bila sababu.
Sasa hawa watu tunawaoneaje wakati tunawapeleka mahakamani?” Alihoji.
Maalim Seif kuhojiwa
Alisema
kutokana na matukio hayo, tayari Maalim Seif amehojiwa na jalada lake
halijaamuliwa, lipo kwa Mwendesha Mashtaka wa Serikali (DPP) Zanzibar. “Lakini pia tunataka tumpeleke mahakamani kumshitaki kwa makosa aliyofanya ya kuchochea fujo,” alieleza.
Alisema
kazi kubwa ya Polisi kwa sasa si kujiingiza kwenye siasa au kupatanisha
pande mbili zinapokwaruzana, bali kazi yake ni kuhakikisha inadhibiti
na kuwakamata wahalifu.
Alisema
endapo vyama viwili vinavyolumbana visiwani Zanzibar, vitaamua kuchukua
hatua za kisheria kumaliza tofauti zao, polisi haina tatizo, lakini
endapo vyama hivyo vitachukua hatua za kijinai au kukomoana, jeshi hilo
halitokaa kimya.
“Kazi ya polisi iko wazi, tunakamata tunapeleleza na kupeleka mahakamani umma unatuona tunachofanya hatuna cha kuficha,” alisisitiza.
No comments:
Post a Comment