TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
TAREHE 23/06/2016
UTAFITI
MIEZI 8 TOKA MHE RAIS JOHN MAGUFULI AMECHAGULIWA KUWA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
Ndugu
waandishi wa habari habari za leo na pole kwa majukumu mazito ya ujenzi
wa Taifa. Taarifa yetu itajikita katika maeneo makuu mawili, Mkutano
Mkuu wa CCM na UTAFITI wa Miezi 8 ya Mhe Rais John Magufuli.
Taasisi
ya CZI ni taasisi huru isiyo ya kiserikali ambayo inajihusisha na
ushauri wa mambo ya HABARI na kijamii, pamoja na tafiti mbalimbali.
Katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita, tulizunguka nchi nzima na
kuuliza wananchi maswali ya papo kwa papo, ama kwa njia ya simu ama kwa
kuhoji kimakundi kulingana na umri wa wahusika.
Tulihoji
Watanzania 2,3oo wa kada mbalimbali katika maeneo kadha wa kadha
tuliyotembelea kuanzia umri wa miaka 14 hadi 18 na kuanzia wenye umri wa
miaka 18 hadi 30 na kuanzia miaka 30 hadi 60.
KUNDI LA 1 UMRI MIAKA 14-18
Kundi
hili baada ya kuhojiwa wanaamini Rais John Magufuli ataleta mageuzi
makubwa ya kiuchumi, na atarejesha nidhamu ya masomo shuleni kuanzia
shule za awali, msingi nasekondari kwa vijana wenye umri kuanzia miaka 7
hadi 18.
Asilimia
78 ya vijana hao kwenye ngazi ya elimu ya msingi na sekondari wanaamini
Mhe Rais Magufuli atasaidia kuleta mageuzi kwenye elimu ikiwa ni pamoja
na kuondoa tatizo la madawati, mitaala na nidhamu ya walimu, huku
asilimia 22 ya vijana hao wakisema Mhe Rais huenda asifanikiwe kwenye
harakati zake za mageuzi kwenye sekta ya elimu. Pia kundi hili linaamini
kuondolewa kwa michezo shuleni kutazidi kudidimiza maendeleo ya michezo
nchini.
KUNDI LA II UMRI MIAKA 18-30.
Watanzania
kuanzia miaka 18-30, asilimia 82 wanaamini serikali ya Rais Magufuli
italeta mageuzi kwenye elimu hususan kwenye mikopo ya wanafunzi wa elimu
ya juu pamoja na kumaliza tatizo la mabweni ya kulala wanafunzi wa vyuo
vikuu. Pia kada hiyo inaamini rais anaweza kupunguza tatizo la ajira
kwa wahitimu wa vyuo vikuu pamoja na vijana nchini Tanzania. Sababu kuu
ambayo inawafanya waseme hayo inatokana na kupambana na wafanyakazi hewa
katika taasisi za serikali ambazo zimekuwa zikichangia kukosekana kwa
ajira kwa vijana. Lakini sababu nyingine ya kuongezeka kwa ajira ni
msimamo wa serikali wa kufufua na kuanzisha viwanda vipya, hasa vya
mazao ya kilimo ili kuongeza mnyororo wa thamani kwa mazao ya kilimo.
Aidha
asilimia 18 ya kada hii haiamini kama serikali ya awamu ya tano italeta
mageuzi yoyote nchini na wanasema ni kawaida ya serikali kuwapa
matumaini wananchi wake lakini mwishoni mambo hubaki vilevile kama awamu
zilizopita.
KUNDI LA III UMRI MIAKA 30-60
Watanzania
wenye umri wa miaka 30-60 waliohojiwa wanasema kuna uwezekano watumishi
wa umma wakarejesha imani kwa serikali kutokana na juhudi za Mhe. Rais
anavyopambana na ufisadi na rushwa kwa dhati.
Aidha
kada hii asilimia 89.0 wanaamini Mhe Rais atamaliza matatizo ya wazee
kwa kuanza kuwalipa posho kwa mwezi lakini pia wanaamini nidhamu ya
watumishi itaongezeka miongoni mwa watumishi wa umma pamoja na binafsi
kutokana na namna serikali inavyopambana na watumishi hewa na utumbuaji
majipu unaoendelea kwenye serikali ya awamu ya tano.
Aidha
kada hii inaamini umoja na mshikamano wa Watanzania utaendelea
kuimarika na moyo wa kusaidiana kwa wananchi wa Tanzania utadumu na
kuimarika pia.
Vile
vile kada hii inasema Rais Magufuli anazidi kuwa maarufu huku wapinzani
wakionekana kupoteza umaarufu kutokana na kushindwa kubuni mbinu mpya
ya mapambano ya kisiasa.
Asilimia
11 ya kada hii inaamini serikali ya awamu ya tano haitaleta mageuzi
yoyote kwa wazee na nidhamu kwa watumishi wa umma haitabadilika kutokana
na aina ya viongozi wanaowasimamia watumishi hao ambao wengi wao siyo
waadilifu na siyo watendaji na wafuatiliaji wa mambo kwenye maeneo yao
ya kazi.
Kwa
ujumla wake mhe rais anakubalika kwa asilimia 89% huku akiwa amewapiku
Edward Lowasa na Mhe Jakaya KIkwete ambao wao wamegawana zilizobaki.
Jakaya Kikwete akiwa na asilimia 7% huku Edward Lowasa akiwa na asilimia
4%.
Mikoa
ambayo tulikwenda ni Dodoma, Mara, Geita, Ruvuma, Arusha, Manyara,
Kusini Pemba, Wete Pemba, Kaskazini Unguja, Tabora, Kigoma, Pwani,
Morogoro, Simiyu, na Tanga, na kuhoji wananchi takriban 2,300.
MAFANIKIO YA MIEZI NANE (8) YA UTAWALA WA RAIS DK. JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI
Mara
tu baada ya kutangazwa mshindi hata kabla ya kuapishwa Novemba 5, 2015
watu wengi walibeza kama angeweza kutekeleza yale aliyoyasema. Wapo
waliosema kwamba asingeweza kupambana na rushwa na ufisadi kwa sababu
mfumo huo umeanzia ndani ya CCM. Walizungumzia kuhusu suala la kufumua
mfumo wa uendeshaji wa Serikali, kuijenga upya CCM, pamoja na namna ya
kushirikiana na upinzani. Wengine wakahoji muundo wa baraza la mawaziri
utakavyokuwa hasa kwa vile lililopita lilikuwa kubwa mno.
Hata
hivyo, katika kipindi cha miezi nane tu, amefanya mambo makubwa mengi
kana kwamba amekuwepo madarakani kwa muda mrefu na kwa kiasi kikubwa
hata ahadi zake nyingi amekwishazitekeleza na nyingine anaendelea
kuzitekeleza. Tutajaribu kukumbusha machache kati ya mengi aliyoyafanya
katika kipindi hicho.
Alielekeza
Shs. 225 milioni zilizochangwa kwa ajili ya kugharamia hafla ya pongezi
za Wabunge Dodoma kutumika kununua vitanda vya hospitali ya Muhimbili
na Shs. 15 milioni tu ndio zitumike kwa ajili ya sherehe hiyo.
1. MPANGO MAHUSUSI WA KURUDISHA NIDHAMU KATIKA UTUMISHI WA UMMA (UTUMBUAJI MAJIPU)
Kurudisha
nidhamu kwa watumishi wa umma ilikuwa moja ya agenda zake na ahadi
aliyoirudia Zaidi ya mara 100 wakati wa kampeni zake na hata sasa bado
anaendelea kusema. Watanzania wamekuwa na kilio cha muda mrefu kwamba
wamekuwa wakishindwa kupatiwa huduma muhimu na watendaji wa serikali,
ambao wengi wao hawatekelezi wajibu wao ipasavyo.
Itakumbukwa
kwamba, hata kabla hajaunda Baraza lake la Mawaziri, Rais Magufuli
alifanya mambo makubwa kadhaa ambayo hayakutegemewa. Kwanza alifanya
ziara mbili kubwa za kushtukiza ambapo Novemba 6, 2015 ikiwa ni siku
moja tu baada ya kuapishwa alitembea kwa miguu kutoka Ikulu hadi Wizara
ya Fedha ambako alipita katika ofisi moja baada ya nyingine na baadaye
alifanya kikao na watendaji. Novemba 9 alifanya ziara nyingine ya
kushtukiza katika Hospitali ya Taifa Muhimbili ambako alivunja Bodi ya
Wakurugenzi, alimwondoa Kaimu Mkurugenzi wa hospitali hiyo, Dk. Hussein
Kidanto na kuamuru mashine muhimu za vipimo za CT-Scan na MRI
kutengenezwa haraka huku akitoa sehemu ya mshahara wake kumlipia mgonjwa
mmoja aliyekuwa anahitaji kufanyiwa kipimo cha CT-Scan.
Ni
katika kipindi hicho ambapo Serikali, katika zile zile ziara za
kushtukiza zilizofanywa na Rais mwenyewe na Waziri Mkuu Mhe. Kassim
Majaliwa, Watanzania walishuhudia vigogo wa Mamlaka ya Bandari Tanzania
(TPA) na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wakiswekwa ndani,
kusimamishwa, kutenguliwa teuzi zao na wengine kufikishwa mahakamani kwa
makossa mbalimbali, yakiwemo uzembe, rushwa na ufisadi na matumizi
mabaya ya madaraka. Tumeona watendaji wa mamlaka nyingi za umma
wakiendelea kusimamishwa/kufukuzwa kazi kama Kamishna Mkuu wa TRA,
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Mkurugenzi
Mkuu wa TAKUKURU, UHAMIAJI na TRL. Hii imerudisha nidhamu kwa watumishi
wa UMMA na kuleta ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi.
2. MPANGO WA KUBANA MATUMIZI
Itakumbukwa
kwamba, Rais Magufuli alipunguza kupunguza sherehe na dhifa za kitaifa
na Jumatatu ya Novemba 23, 2015, alitangaza kufutwa kwa Sherehe za Uhuru
Desemba 9 na kuagiza fedha za maandalizi ya sikukuu hiyo zitumike
kutatua matatizo mengine, ikiwemo kufanya upanuzi wa Barabara ya
Morocco-Mwenge huku akiagiza siku hiyo itumike kusafisha mazingira ili
kupunguza matatizo ya kipindupindu nchini. Alifuta sherehe za Muungano
na kuelekeza kwamba fedha hizo zitumike kupanua barabara ya kutoka
Uwanja wa Ndege jijini Mwanza hadi mjini. Aliagiza pia taasisi hizo
zifanye vikao vyao katika kumbi maalum za idara zao badala ya kwenda
mikoani ama kukodi kumbi za hoteli huku watu akijilipa posho nyingi
wakati vikao hivyo ni vya kiutendaji tu.
Tumeshuhudia
katika uteuzi wa viongozi wa serikali ya Awamu ya 5, Mh. Rais amezuia
shamlashamla za kupongezana viongozi wa serikali wanapoteuliwa na
kufanya uteuzi wa serikali ya awamu ya Tano kutumia bajeti ndogo katika
siku hizo za uteuzi. Mfano, uteuzi wa Wakuu wa wilaya, Mawaziri na wakuu
wa Mikoa hakukuwa na shamlashamla kama ilivyozoeleka katika awamu
zilizopita.
Hili
limesaidia kuokoa fedha nyingi ambazo zimekwenda kufanya shughuli za
maendeleo ya wananchi. Wale waliodhani kwamba utendaji wa Dk. Magufuli
ni mfumo wa kujilundikia majukumu bila utekelezaji (Slack Management
Style) walikosea sana, kwa sababu tangu wakati ule tumeshuhudia
watendaji wengi wazembe, wala rushwa na mafisadi wakiwajibishwa huku
wengine wakifikishwa mahakamani.
3. WATUMISHI HEWA
Suala
la kuwepo kwa watumishi hewa, ambalo lilikuwa linalalamikiwa kwa muda
mrefu, safari hii Rais Magufuli alilitumbua ambapo tulishuhudia kwamba
kumbe kulikuwa na watumishi hewa zaidi ya 12,000 waliokuwa wanalipwa
mabilioni ya fedha ambazo ziliingia kwa maofisa wajanja. Kuonyesha
kwamba hakuwa na mzaha hata kidogo, alimfuta kazi mara moja Mkuu wa Mkoa
wa Shinyanga baada ya kugundua kwamba alimdanganya kwamba mkoa wake
haukuwa na mtumishi hewa hata mmoja wakati haikuwa hivyo. Mabilioni
mengi ya fedha yameokolewa kutokana na zoezi hilo katika Serikali za
Mitaa.
4. SAFARI ZA NJE KWA WATUMISHI WA UMMA NA VIONGOZI WA KISERIKALI
Rais
Magufuli alianza mara moja kwa kutangaza kufuta safari zote za nje za
mafunzo na ziara kwa maofisa na watendaji wa Serikali katika harakati za
kubana matumizi huku akibainisha kwamba, safari hizo zililigharimu
Taifa mabilioni ya fedha wakati nyingi hazikuwa na tija. Akasema yeyote
ambaye alitaka kusafiri ilikuwa lazima apate kibali maalum kutoka kwa
Katibu Mkuu Kiongozi au kwake yeye. Siyo siri kwamba hili limeondoa zile
‘safari za kufanya shopping’ ambazo maofisa wengi wa serikali
walizitumia kutafuna fedha za umma na kuitia doa Serikali ya CCM.
Uamuzi
wa Mh. Rais kurudisha utaratibu wa vibali vya kwenda nje, umeokoa pesa
nyingi sana ambazo zilikuwa zinatumika na viongozi mbalimbali wa
serikali kusafiri kwenda nchi za nje safari ambazo zilikuwa hazina tija
kwa taifa. Kwa kulitekeleza hili hata yeye mwenyewe katika kipindi cha
miezi 8 ya utawala amesafiri mara 2 tu, kwenda Rwanda na Uganda. Huu ni
mfano ambao unatakiwa kuigwa na kuungwa mkono na watanzania wote walio
na dhamana katika sekata ya umma.
5. ELIMU BURE (CHEKECHEA MPAKA KIDATO CHA NNE)
Katika
kufuata Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015, ameweza kupeleka TShs
bilioni 18 kwa ajili ya kutekeleza mpango huo wa elimu bure kwa shule za
msingi na sekondari. Hivi sasa tunashuhudia idadi kubwa ya udahili wa
wanafunzi wa shule za msingi na kuongeza idadi kubwa ya uhitaji wa
madawati hasa kwa shule za msingi. Wazazi wengi wameitikia na kuamua
kupeleka watoto wao shuleni haya ni matokeo ya Utekelezaji wa Sera ya
Elimu bure katika ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015.
6. PUNGUZO LA KODI KWA WAFANYAKAZI (PAYE) UKUSANYAJI WA MAPATO
Serikali
makini hukusanya kodi! Rais Magufuli katika kipindi kifupi tu ameweza
kusimamia vyema ukusanyaji wa kodi akianza kwa kuwabana wafanyabiashara
wakubwa ambao walikuwa wakwepaji sugu. Lakini pia Serikali imeweza
kupunguza kiasi cha kodi ya PAYE kwa 2% katika mishahara ya wafanyakazi
kila mwezi na kuondoa makali ya kodi kwa wafanyakazi wake.
7. VITA DHIDI YA MAFISADI
Mh.
Rais pia ameweza kuanzisha mahakama ya mafisadi kwa lengo la kupambana
na mafisadi ambao wamelifikisha taifa la Tanzania kwa wizi mkubwa wa
mali za umma pamoja na matumizi mabaya ya fedha za serikali. Hili
alilisema katika kampeni na amelitekeleza kwa asilimia 80 akionyesha
dhamira yake ya kushughukia watu wa namna hiyo.
Katika
sherehe za kuanza mwaka wa kimahakama Mh. Rais aliweza kuahidi na kutoa
jumla ya Tshs Bilion 12 ili kuharakisha utendaji wa mahakama jambo
ambalo halijawahi kufanyika na kila mwaka awamu zilizopita bajeti
haitoshelezi kwa muhimili huu. Fedha hizo zilikabidhiwa kwa Idara hiyo
mwezi Februari 2016.
Ajabu
ni kwamba, kasi ya kuwawajibisha watumishi wa umma ikaanza kupingwa na
baadhi ya wapinzani, hususan wale ambao walikuwa wanaahidi kwenye
kamepni zao kwamba wangeweza kupambana na ufisadi! Siyo siri kwamba,
tayari kasi yake hiyo ilikuwa imewapoteza wapinzani hata kabla hajaunda
baraza la mawaziri – wakati huo akiwa na wasaidizi watatu tu – Katibu
Mkuu Kiongozi, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu!
8. UJENZI WA MABWENI KWA WANAFUNZI WA CHUO KIKUU CHA DAR ES SALAAM
Mh.
Rais amehaidi kujenga mabweni kwa ajili ya wanafunzi wa chuo kikuu cha
Dar es salaam jambo ambalo lilipigiwa kelele sana na wanafunzi katika
awamu zilizopita lakini leo litafanyika kupitia Mh. Rais wa awamu ya
Tano kama alivyo ahidi.
Yako
mengi sana aliyoyatekeleza ambayo hayawezi kutosha hapa, lakini Rais
Magufuli, ambaye kimsingi ameisongesha mbele Tanzania katika kipindi
kifupi, anaweza kufanya mambo makubwa zaidi hasa atakapokabidhiwa
uenyekiti wa taifa wa CCM, chama tawala na kikongwe kabisa barani
Afrika, kwa sababu huko nako ataondoa mfumo mbovu wa uongozi unaokifanya
chama hicho kilalamikiwe na kiwe agenda kuu ya wapinzani kila mara.
Wale
wanaobeza utendaji wake wanapaswa kukaa kimya, kwani Wananchi
waliomweka madarakani ndio watakaompima na kumhukumu, kwa sababu hakuna
aliyetegemea kama serikali hii ingeweza kuondoa Service Charge kwenye
umeme wa majumbani ambapo wananchi walikuwa wanaumizwa sana na hili
jambo.
Mwenye
nia njema na maendeleo ya taifa hili, anapaswa kuiunga mkono kwa dhati
kabisa serikali ya Dk. Magufuli kwa utendaji huu na siyo kumhujumu,
kumbeza ama kutoka visingizio vyovyote vile.
Tudumishe umoja, mshikamano na Amani. Mungu Ibariki Afrika, Mungu Ibariki Tanzania!
Imeandaliwa na:
David Saire Manoti-Mwanasiasa Kijana
Raphael Nyang’i Awino- Mwanasiasa kijana
Cyprian Musiba Nyamagambile- Mwandishi/Mtafiti
Dotto omary Nyirenda - Mwanadiplomasia kijana
Daniel Mahelela - Mtafiti
Juma George Chikawe-Mwanasheria
No comments:
Post a Comment