KWA MAONI AU USHAURI E-mail: inocomm2014@gmail.com, PIGA SIMU: 0714555668

www.utt-pid.org


TEMBELEA: www.utt-pid.org

July 15, 2016

RAIS MAGUFULI AFUFUA SAFARI YA KUHAMIA DODODMA KWA KUWAPELEKA MASHUJAA DODOMA


RAIS John Magufuli ameonesha nia ya kuhamia Dodoma kwa kuanza kushughulikia masuala muhimu, ikiwamo ya kuzindua awamu ya kwanza ya upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Dodoma na kuhamishia maadhimisho ya Siku ya Mashujaa mkoani Dodoma.

Akizungumza juzi wakati wa mkutano wa kitaifa wa amani ulioandaliwa na Jumuiya ya Ahamadiyya, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana alisema katika kuonesha dhamira ya kuhamia Dodoma ambao ulitangazwa kuwa Makao Makuu ya Tanzania miaka ya 1970, Rais alielekeza fedha zilizobaki kwenye bajeti iliyopita zitumike kwa ajili ya upanuzi wa uwanja wa ndege ambao pia ujenzi wake utazinduliwa na Rais mwenyewe Julai 22, mwaka huu.

Aidha, Rugimbana alisema Rais Magufuli pia ameagiza maadhimisho ya Siku ya Mashujaa mwaka huu yahamie Dodoma ambapo kwa miaka mingi sasa yamekuwa ikifanyika kwenye Viwanja vya Mashujaa, Mnazi Mmoja Dar es Salaam.

“Ndio natoka kwenye kikao cha kuzungumzia maadhimisho hayo kufanyika Dodoma hilo linadhihirisha wazi dhamira ya Rais kuhamia Dodoma,” alisema Rugimbana na kuongeza kuwa Rais Magufuli atashiriki Mkutano Mkuu Maalumu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) utakaoanza Julai 23, mwaka huu.

Akizungumzia suala la amani, mkuu huyo wa mkoa alisema serikali itawachukulia hatua kali viongozi wa taasisi mbalimbali ambao wamekuwa na tabia za kutumia nafasi zao kuhubiri uchochezi na hivyo kutishia amani na utulivu wa nchi.

Alisema viongozi ambao wamekuwa na tabia za kutumia taasisi zao kama sehemu ya kuhubiri masuala ya uovu, ikiwemo kushawishi vitendo vya uvunjifu wa amani, serikali haitawafumbia macho.

Aliwataka viongozi wa dini nchini kutimiza wajibu wao kwa mujibu wa Katiba za taasisi zao na siyo kufanya mambo kwa maslahi yao binafsi na tamaa. Alisema pia serikali inaunga mkono jitihada za taasisi za dini katika kuhubiri amani na utulivu wa nchi ambazo zimekuwa zikifanywa na viongozi mbalimbali.

“Kama serikali, tunaunga makono jitihada zenu mbalimbali ikiwemo kupinga vitendo vya maovu pamoja na ufisadi ambao umekuwa ukilitafuna taifa letu,” alisema.

Naye Mwakilishi wa Jumuiya hiyo ya Ahmadiyya, Abdulrahman Ahmed akitoa mada kuhusu amani, alisema Waislamu wanatakiwa kuzingatia miiko ambayo imewekwa na dini hiyo katika kusaidia kudumisha amani na utulivu.

Wakati huo huo, mapema wiki hii Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa alisema serikali inakarabati na kuongeza ukubwa wa Uwanja wa Ndege wa Dodoma ili upokee ndege kubwa za mizigo, abiria na viongozi wa kitaifa na kimataifa, ikiwa ni maandalizi ya kuufanya mkoa kuwa makao makuu ya nchi kivitendo.

Ujenzi huo unatarajia kugharimu kiasi cha Sh bilioni 11.5 ambazo ni fedha za ndani na utakamilika kwa muda mfupi ili kutoa fursa kwa mashirika ya ndege kuanza huduma mkoani Dodoma, ikiwemo ndege kubwa zitakazonunuliwa na serikali mwaka huu.

Profesa Mbarawa akizungumza baada ya kukagua uwanja huo alisema uamuzi huo unafikiwa kutokana na Serikali ya Awamu ya Tano kutaka kuufanya Dodoma makao makuu ya nchi kivitendo, jambo linalotarajiwa kuongezeka shughuli mbalimbali zikiwemo za kiutawala, uchumi, biashara na diplomasia sambamba idadi ya wageni.

Kwa upande wake, Meneja Mradi wa Upanuzi wa uwanja huo kutoka Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Mbila Mdemu alisema mpaka sasa mita 900 zimekamilika kwa kuweka tabaka la kwanza lami katika eneo la kuruka na kutua ndege na kazi ya kuchimba na kusawazisha eneo la kurefusha njia imekamilika.

Alisema wanatarajia kukamilisha kazi hiyo kwa muda mfupi. Upanuzi wa uwanja huo unahusisha njia ya kuruka na kutua kwa ndege yenye urefu wa Km 2.5 na mita 500 za taa za kuongozea ndege na usalama wa kuruka kwa ndege.

No comments:

Post a Comment