Wakati
CCM ikijiandaa kumkabidhi Rais John Magufuli uenyekiti, suala la
masalia ya Edward Lowassa linaweza kuchukua nafasi kubwa katika vikao
vitatu vya juu vinavyofanyika kwa mara ya kwanza tangu kumalizika
Uchaguzi Mkuu mwaka jana.
Ni
dhahiri kuwa Mkutano Mkuu Maalumu ulio na ajenda moja tu ya kumchagua
mwenyekiti mpya hautakuwa na nafasi ya kujadili ajenda nyingine, lakini
Halmashauri Kuu iliyogawanyika baada ya Lowassa kuenguliwa kwenye mbio
za urais, inaweza kuchukua muda kujadili CCM mpya baada ya waziri huyo
mkuu wa zamani kujiondoa Julai 28 mwaka jana.
CCM
itaanzia mikutano yake kwa kikao cha Kamati Kuu, ambayo hufanya
maandalizi ya kikao cha Halmashauri Kuu kitakachofanyika Ijumaa na
kumalizia na Mkutano Mkuu Jumamosi wiki hii.
Pia
kutakuwa na kikao kingine cha Halmashauri Kuu kitakachofanyika Jumapili
ambacho kwa sehemu kubwa kinatarajiwa kujadili taarifa za wasaliti
zilizoandaliwa na kamati za siasa za mikoa na huenda kikatoa maamuzi
mazito yanayobeba mustakbali wa kuijenga “CCM ya Magufuli”.
Lakini
makada wengi waliohojiwa kuhusu suala la masalia ya Lowassa kuibuka
kwenye vikao hivyo, walipinga wakisema waliomuunga mkono mwanasiasa huyo
maarufu, walifanya hivyo wakati akiwa CCM na kwa kuwa hawakumfuata
hawatarajii suala hilo kuibuka tena.
“Makundi ndani ya CCM yalikwisha baada ya Magufuli kupitishwa kukabidhiwa kijiti,”
alisema mwenyekiti wa CCM wa mkoa wa Geita na mbunge wa Geita Vijijini,
Joseph Kasheku Msukuma alipoulizwa kuhusu suala la Lowassa kuibuka
kwenye vikao hivyo vya juu.
Msukuma,
ambaye alifanya mbwembwe za kuhama kambi ya Bernard Membe kwa kutua na
helikopta kwenye mkutano wa Lowassa mjini Arusha, alisema wakati CCM
ikisaka mgombea wake wa urais, kulikuwa na makundi zaidi ya 40.
“Wakati
ule kila mgombea alikuwa na kundi. Ila kwa sasa sidhani kama hali hiyo
bado ipo maana baada ya mgombea kupatikana kila mmoja alimuunga mkono,” alisema Msukuma.
Kauli
kama hiyo ilitolewa na mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Dar es Salaam,
Ramadhan Madabida ambaye alisema kila mwenyekiti huja na timu yake,
hivyo kama kutakuwa na mageuzi, si kitu kinachohitaji mjadala.
“(Rais
wa Awamu ya Tatu, Benjamin) Mkapa alipomuachia uenyekiti (Rais wa Awamu
ya Nne, Jakaya) Kikwete alikuja na timu yake mpya. Kama utakumbuka
katibu mkuu wake alikuwa Yusuf Makamba,” alisema Madabida ambaye naye alikuwa miongoni mwa wenyeviti waliomuunga mkono Lowassa.
“Nina
matarajio na rais. Naamini atakifanya chama kuwa imara zaidi na kuleta
mageuzi ya kisiasa na kiuchumi. Mabadiliko ni kawaida na wenyeviti wapya
huja na kamati kuu na sekretarieti mpya.”
Hata
hivyo, kuanzia Januari mwaka huu kamati za siasa za mikoa zimekuwa
zikikutana kujadili watu wanaoitwa ni wasaliti na kupeleka mapendekezo
ya hatua dhidi yao kwenye vikao vya juu.
Rais
Magufuli, ambaye hajawahi kushika uongozi wa chama, anaaminika kuwa
ataifanya CCM kuwa na sura, mwelekeo na ushawishi mpya, hali
itakayochangia kukata mizizi iliyojengwa na wanasiasa mashuhuri.
Kutokana
na hali ilivyokuwa wakati Lowassa akiondoka CCM na mtikisiko aliouacha,
chama hicho hakitaweza kujipapatua bila kumtaja Lowassa na mtandao wake
wakati kikijadili jinsi ya kusonga mbele.
Mbunge
huyo wa zamani wa Monduli amekuwa akijadiliwa kwa ushabiki mkubwa ndani
na nje ya vikao halali vya CCM tangu alipojitokeza kwa mara ya kwanza
mwaka 1995 kuwania urais akiwa na umri wa miaka 42.
Kuelekea
Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2015, mwanasiasa huyo aliwagawa makada wa CCM
na alipohamia Chadema kuna kundi lilimfuata na jingine kubakia, huku
baadhi ya wanachama kwenye kundi hilo wakituhumiwa kwa usaliti.
Baada
ya kujiondoa CCM Julai 28, 2015 na kujiunga Chadema alikoteuliwa kuwa
mgombea urais na kuungwa mkono na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya
Wananchi (Ukawa), mashambulizi mengi kutoka CCM yalielekezwa kwake.
Vikao
vinavyosubiriwa kutia muhuri mapendekezo ya kamati za siasa za mikoa
ndivyo vinavyofanyika wiki hii mjini Dodoma baada ya CCM kuitisha
mkutano mkuu maalumu ili kukamilisha taratibu za kumkabidhi Rais
Magufuli usukani wa chama hicho.
Halmashauri Kuu ya JPM
Halmashauri
Kuu ya JPM inatarajiwa kutumbua watendaji wazembe, goigoi, wasiokwenda
na kasi yake, wabadhirifu wa fedha za chama na wengine ambao uwapo wao
ni mzigo kwa CCM.
Hivyo, Halmashauri Kuu itasuka upya chama, pia kwa kujaza nafasi za watendaji waliojiuzulu kutokana na desturi ya chama hicho.
Kwa
kawaida, CCM inapopata mwenyekiti mpya, sekretarieti yote hujiuzulu ili
kumpa nafasi kiongozi huyo kupanga safu yake, alisema msemaji wa chama
hicho, Christopher Ole Sendeka juzi alipoongea na waandishi wa habari
mjini Dodoma.
Sekretarieti
inaongozwa na katibu mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, ambaye anaaminika
kuwa alifanya kazi kubwa ya kukirudishia chama hicho nguvu wakati wa
kuelekea Uchaguzi Mkuu uliopita ambao ulikuwa na ushindani mkubwa.
Wengine
ni Vuai Ali Vuai (Naibu Katibu Mkuu Zanzibar), Rajab Luhavi (Naibu
Katibu Mkuu Bara), Mohamed Seif Khatib (Katibu wa Oganaizesheni) na Nape
Nnauye (Katibu wa Itikadi na Uenezi).
Wengine ni Dk Asha-Rose Migiro (Katibu wa Idara ya Mambo ya Nje), na Zakia Meghji (Katibu wa Uchumi na Fedha).
Halmashauri
Kuu ya JPM inatarajiwa pia kujadili hali ya hewa ya kisiasa ndani ya
chama, kupanga mikakati ya kuimarisha uchumi na kutekeleza mapendekezo
ya kuwafukuza wasaliti, ambao wanatuhumiwa kuwa waliendelea kumuunga
mkono Lowassa wakati wa kampeni na kusababisha chama kupoteza baadhi ya
majimbo.
Oktoba
30, 2015 baada ya kukabidhiwa cheti cha ushindi wa urais na Mwenyekiti
wa Tume ya Uchaguzi (NEC), Jaji Damian Lubuva iliandaliwa hafla fupi
makao makuu ya CCM Lumumba, ambako Dk Magufuli alimwambia mwenyekiti
wake akisema: “Umezungukwa na wanafiki na watu ambao ulidhani watakusaidia kwenye chama, lakini wamekuangusha”
Miongoni
mwa watu ambao hata wakati wa kampeni alikuwa anawashutumu ni waliowahi
kushika nyadhifa za juu serikalini, lakini wakahamia upinzani na
kuibeza Serikali.
Dk Magufuli anaonekana alikuwa anawalenga Lowassa na mwenzake Frederick Sumaye ambao waliunda safu kabambe ndani ya Chadema kuisakama CCM.
Orodha
ya watakaotumbuliwa na NEC ya JPM ni ndefu. Baadhi yao ni makada
waliojitokeza hadharani kupinga utaratibu uliotumiwa na wazee kukata
jina la Lowassa kugombea urais.
Hata baada ya CCM kumteua Dk Magufuli kuwa mgombea urais, bado wapo waliompinga wakidai hana mizizi katika chama.
Wengine
wanaoweza kutumbuliwa ni walioanzisha wimbo wa “Tuna imani na Lowassa”
ndani ya kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM wakionyesha utiifu wao kwa
Lowassa badala ya Mwenyekiti Kikwete aliyeongoza kikao cha Kamati Kuu
kilichotoa majina matano ya waliopitishwa kugombea urais bila ya jina la
Lowassa kuwamo.
Wengine wanaoweza kutupiwa virago ni makada waliosusa kumpigia debe Dk Magufuli pamoja na waliodaiwa kukitelekeza chama.
Habari
nyingine zinasema waliopendekezwa kufukuzwa na vikao vya wilayani ni
wanaodaiwa kubadilika usiku na kusaidia Ukawa, wakiwamo wenyeviti wa
mikoa na makatibu.
Pia,
wamo baadhi ya wabunge na wafanyabiashara waliokuwa wanawabeba mamia
kwa makumi ya wanachama kwenda nyumbani kwa Lowassa mjini Dodoma
kuonyesha kumuunga mkono
|
No comments:
Post a Comment