Na Is-haka Omar, Zanzibar.
KAMATI ya Siasa ya CCM Mkoa wa
Magharibi kichama imeagizwa kukagua na kusimamia vizuri utekelezaji wa
ilani ya Chama ya Mwaka 2015/2020 inayotekelezwa katika majimbo ndani
ya Mkoa huo ili kujiridhisha kama zimetekelezwa kweli au la.
Agizo hilo limetolewa na Naibu
Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, wakati akizungumza na viongozi wa Kamati
hiyo huko Ofisi ya Mkoa huo iliyopo Mwera Unguja.
Alisema kuna baadhi ya viongozi
wa Majimbo hasa Wabunge, Wawakilishi na Madiwani wamekuwa wakitekeleza
Ilani hiyo vizuri na wengine kushindwa kufanya hivyo hali inayosababisha
kuongezeka kwa changamoto zisizokuwa za lazima kwa baadhi ya wananchi.
Vuai aliwambia viongozi wa Kamati
hiyo kuwa pamoja na kufanya kazi za Chama bado wana jukumu la
kuwasimamia Wabunge na Wawakilishi kwa lengo la kuhakikisha wanatekeleza
kwa vitendo ahadi walizotoa kwa wananchi majimboni.
“Msisubiri kusikia katika vyombo
vya habari au kuambiwa katika vikao kuwa Mbunge ama Mwakilishi Fulani
kachimbisha kisima au kajenga skuli (Shule) badala yake nendeni wenyewe
mkakague kwa kina miradi hiyo ili kupata takwimu sahihi za utekelezaji
wa Ilani ya CCM kwa kila jimbo.”, alisema Vuai.
Alisema lengo la CCM ni kuwa na
viongozi imara wanaosimamia maslahi, miongozo na maelekezo ya chama na
wenye uwezo wa kuwatumikia wananchi kwa vitendo ndani ya Majimbo na
Wadi.
Naibu Katibu Mkuu huyo alieleza
kwamba utekelezaji mzuri wa Ilani ya CCM ya mwaka 2015/2020 ndiyo tiketi
halali ya kuirejesha CCM madarakani katika Uchaguzi Mkuu ujao wa mwaka
2020.
Aliwasihi viongozi kushirikiana
na pendana na patakapotokea mtu amekosea watumie vikao halali vya
kikatiba kusululisha kasoro hizo.
Hata hivyo aliwapongeza viongozi
wa Kamati hiyo kwa kuendelea kusimamia vizuri utekelezaji wa Ilani ya
CCM na maagizo ya Chama ambapo juhudi hizo zimesaidia kuongeza
kuimarika kwa hali ya kisiasa ndani ya Mkoa huo.
No comments:
Post a Comment