Wadau wa habari nchini wameipongeza Serikali kwa kuwasilisha Bungeni Muswada wa Sheria ya Huduma za habari wa mwaka 2016.
Hayo
yalisemwa na Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Bw.
Theophil Makunga wakati akitoa taarifa kuhusu muswada wa Sheria ya
huduma za habari wa mwaka 2016 kwa waandishi wa habari leo jijini Dar es
salaam.
“Tunaishukuru
Serikali kwa kuanza mchakato wa kuiondoa sheria ya habari ya mwaka 1976
kwa kupeleka bungeni muswada mpya wa Sheria ya Huduma za Habari wa
mwaka 2016,” alisema Makunga.
Alisema
kuwa muswada huo ambao umesomwa bungeni kwa mara ya kwanza na Waziri wa
habari, Utamaduni , Sanaa na Michezo Nape Nnauye utamaliza kilio cha
siku nyingi cha waandishi na wadau wa habari kuhusu sheria ya mwaka 1976
ambayo ilionekana kuwabana katika utendaji wao wa kazi.
Ameongeza
kuwa katika muktadha huo, taasisi mbalimbali za kihabari na wadau wa
habari wanatakiwa kushiriki katika kutoa maoni yao ili kazi ya uandishi
wa habari isiwe na matatizo.
Makunga
amesisitiza kuwa muswada huo siyo mali ya wamiliki wa vyombo vya habari
, wahariri, au vyumba vya habari vilivyopo Dar es Salaam pekee bali
unagusa maslahi mapana ya sekta nzima ya habari nchini.
Aidha,
katika kukusanya maoni hayo ya wadau wa habari wamewekewa mpango
utakaowawezesha kukusanya maoni yao nchi nzima kupitia klabu zao za
waandishi wa habari zilizosambaa nchi nzima.
Wadau
wa habari nchini wataweza kusoma muswada huo na kufanya uchambuzi wa
maudhui yake na hatimaye kutoa maoni yatakayowezesha kupatikana kwa
sheria bora.
Muswada
wa Sheria ya huduma za habari wa mwaka 2016 kwa mara ya kwanza umesomwa
bungeni na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye
katika Mkutano wa Nne wa Bunge la 11 lililomalizika Septemba 16 mwaka
huu.
Na Abushehe Nondo, MAELEZO
No comments:
Post a Comment