Vitendo vya ukatilitili wa kijinsia kwa watoto vimeendelea kuongezeka kwa kasi nchini katika kipindi cha mwezi Januari hadi Julai mwaka huu ambapo zaidi ya watoto 2,570 wa kike na kiume wamelawitiwa na kubakwa.
Akizungumza katika sherehe za maadhimisho ya miaka 21 ya Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) yaliyofanyika leo katika Makao makuu ya watoto yaliyopo Kurasini jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC Helen Kijo-Bisimba amesema idadi hiyo ni kubwa ukilinganisha na ya mwaka jana.
Hata hivyo, Mama Bisimba amesema kwa mujibu wa Msemaji wa Jeshi la Polisi, takwimu hizo zinaweza kuwa ndogo kutokana na kesi nyingi za ubakaji na ulawiti kwa watoto kutoripotiwa polisi kwa sababu ya mila na desturi za maeneo mengi nchini.
“Ripoti ya Jeshi la Polisi kupitia dawati la jinsia kati ya Januari na Machi 2016 inaonyesha matukio ya watoto kubakwa na kulawitiwa yakiendelea kuongezeka kutoka 180 hadi 1765 hayo ni matukio yaliyotolewa taarifa katika vituo mbalimbali vya polisi nchi nzima ukilinganisha na matukio 1585 mwaka 2015. Hata hivyo waliohusika na matukio hayo wameonekana wakirandaranda bila kuchukuliwa hatua za kisheria, ” amesema.
Amesema ripoti hiyo inaonyesha kuwa kesi 1,203 zipo katika hatua ya upelelezi, 822 zipo mahakamani na watuhumiwa 234 wamekwisha hukumiwa.
“Pia utafiti uliofanywa na Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto kwa kushirikiana na Tanzania kitengo cha ustawi wa jamii unaonyesha kati ya watoto 10 wa kike 4 wamebakwa, na kati ya watoto 10 wa kiume 3 wamelawitiwa zaidi ya mara tatu. Utafiti huo unaonyesha kwa ujumla kuwa watoto wa kike na wa kiume 6 walifanyiwa ukatili huo na watu ndani ya familia,” amesema.
Bisimba amesema asilimia 49 ya ukatili hufanyika nyumbani, 23 hufanyika njiani wakati wa kwenda shule au kurudi, na asilimia 15 hufanyika shuleni. Pia ripoti hiyo ya UNICEF inaonyeaha kuwepo kwa matukio ya watoto kulawitiana na kubakana wenyewe kwa wenyewe kutokana na kuvizoea vitendo hivyo.
LHRC imeitaka serikali kupitia Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto pamoja na Wizara ya Katiba na Sheria kuifanyia marekebisho sheria ya mtoto na kutilia mkazo malezi bora kwa watoto ikiwemo kuweka kipengele kitakachotoa adhabu kali kwa familia itakayoshindwa kutoa malezi bora kwa mtoto.
LHRC inayoshughulika na utetezi wa sheria na haki za binadamu ilianzishwa Septemba 26, 1995.