Kufuatia
mgogoro uliopo katika Chama cha Wananchi (CUF) baina ya uongozi wa
chama hicho na Profesa Ibrahim Lipumba waliyemfuta uanachama, viongozi
wa CUF wamepanga kwenda mahakamani ili wapate suluhu ya kisheria.
Jopo
la Mawakili wa CUF wakiongozwa na Mwanasheria Tundu Lissu linataraji
kufungua mashitaka mahakamani dhidi ya Lipumba na kundi lake wiki ijayo.
Kwa
madai kuwa Lipumba amevamia ofisi za chama hicho na kuikalia kinyume
cha sheria pamoja na kuharibu baadhi ya mali za chama hicho.
Mwenyekiti
wa Kamati ya Uongozi CUF, Julias Mtatiro wakati akizungumza na mtandao
wa MO BLOG kwa njia ya simu, amesema mawakili hao watakutana siku ya
Ijumaa au Jumamosi ili kuandaa mashitaka na kwamba yatafunguliwa rasmi
mahakamani kuanzia wiki ijayo.
“Mawakili watakutana Ijumaa hii au Jumamosi ili wiki ijayo waanze kufanya hiyo kazi ya mahakamani,” amesema Mtatiro.
Hata
hivyo, Bodi ya Wadhamini ya CUF hapo jana ilitoa tamko la kutaka
kuchukua hatua za kisheria dhidi ya Lipumba ili alipe gharama za hasara,
ilizodai kuwa Lipumba alizisababisha baada ya kuvamia Mkutano Maalumu
wa Taifa wa CUF uliovurugika Agosti 21, 2016 katika Ukumbi wa Blue Pearl
, Ubungo Plaza.
Bodi
hiyo ilidai kuwa hasara iliyosababishwa na Lipumba kwa kuvuruga mkutano
huo ni Milioni 600, na takribani milioni 50 kwa kuvamia ofisi ya chama
hicho iliyopo Buguruni jijini Dar es Salaam na kufanya uharibifu wa mali
za chama hicho zenye thamani ya fedha hiyo.
Bodi
hiyo ilisema itachukua hatua za kisheria zaidi kwa mujibu wa katiba ya
chama hicho kurejesha chini ya himaya yake, mali za chama ikiwemo jengo
la ofisi ya chama hicho kutoka mikononi mwa Lipumba.
Aidha,
baada ya bodi hiyo ya wadhamini kutoa tamko la kumshitaki na
kutomtambua Prof. Lipumba. Upande wa Lipumba ulidai kuwa bodi hiyo haina
baraka na mamlaka ya kuamua jambo lolote juu ya Lipumba.
Abdul
Kambaya, aliye karibu na Lipumba ameuambia mtandao wa Modewjiblog.com
kuwa maamuzi ya kikao cha bodi hiyo hayakuwa halali kwa kuwa akidi ya
wajumbe halali haikutimia.
Ndipo mtandao huu ulipomuhoji Mtatiro zaidi juu ya ufafanuzi wa malalamiko hayo.
Mtatiro
amefafanua kuwa, kikao cha bodi ya wadhamini kilichoketi juzi,
kilikaliwa na wajumbe halali 6, na kwamba wajumbe 3 hawakuhudhuria,
ambapo wawili ni wafuasi wa Lipumba wakati 1 hakuhudhuria kutokana na
kupata udhuru ya safari kwa siku hiyo.
“Idadi
ya wajumbe wa bodi ya wadhamini iko 9, waliofanya kikao 6 akidi hii ni
halali na angekuwepo yule mmoja aliyepata dharura ya safari wangekuwa
saba, Lipumba amebaki na wajumbe wa bodi wawili tu,” amesema.
Mtatiro
amesema maamuzi yoyote yatakayotolewa na bodi hiyo ni halali kwa kuwa
akidi ya wajumbe wake ingawa pungufu lakini inatambulika na kuruhusiwa
kisheria.
Pia
kumekuwepo na tuhuma kutoka upande wa Lipumba kuwa miongoni mwa sababu
ya mgogoro wa chama hicho, ni masilahi binafsi baina ya upande wa
Zanzibar na Bara kwa madai kuwa Zanzibar inanufaika na ruzuku za chama
hicho kuliko Bara.
Mtatiro
amefafanua kuwa, upande wa Bara ndio unaofaidi ruzuku za chama hicho
kuliko Zanzibar na kusema kuwa Baraza Kuu la Uongozi la CUF linatoa
asilimia 70 ya ruzuku ya chama hicho Bara kwa kuwa ina wilaya nyingi za
kichama.
Na kwamba Zanzibar inapokea ruzuku ndogo ya asilimia 30 kwa sababu ina idadi ndogo za wilaya
No comments:
Post a Comment