Kampeni
za uchaguzi mdogo wa udiwani zimeanza kuingia dosari baada ya mfuasi wa
Chadema, Martha Maenda (33) mkazi wa Kichangani, Manispaa ya Morogoro
kuchomwa mkuki mkono wa kulia tukio linalohusishwa na masuala ya
kisiasa.
Maenda
aliyelazwa wodi namba tatu katika Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Morogoro,
alichomwa mkuki juzi saa 10:00 alfajiri, tukio linalohusishwa na
uchaguzi mdogo wa udiwani Kata ya Kiwanja cha Ndege mkoani hapa.
Akizungumza
akiwa hospitali, Maenda alisema akiwa pamoja na wenzake wakiandaa chai
kwenye kambi ya Chadema iliyopo Mtaa wa Kimunyu, walivamiwa na watu
wenye silaha za jadi ambao anadai ni wafuasi wa CCM.
Hata
hivyo, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Morogoro, Fikiri Juma alikana chama
hicho kuhusika akitaka Chadema waseme ukweli wa kilichotokea.
“Nikiwa
na wenzangu tukiandaa chai, lilipita gari dogo lililosimama usawa wa
nyumba tuliyoweka kambi; waliteremka wanaume wasiopungua wanne waliokuwa
na mapanga, rungu, sime, fimbo, mkuki na kutuvamia,” alidai Maenda.
Alidai
wenzake walikimbia, yeye alipojaribu alikamatwa na mmoja wa vijana hao
aliyemchoma mkuki mkono wa kulia akiwa chini baada ya kuanguka.
Baadaye
watu hao walitoweka kwa kutumia gari. Mganga msaidizi wa wodi
aliyolazwa Maenda, Dk John Muneja alithibitisha kumpokea majeruhi huyo
saa 11:00 alfajiri.
Msemaji
wa Chadema wilayani Morogoro, Shaaban Dimoso alisema tukio hilo
linalenga kudhoofisha kampeni za chama hicho na kwamba, siyo la kwanza
kwani Januari 13, saa mbili usiku kuna mtu alivamia kambi hiyo akiwa na
panga lakini alidhibitiwa na taarifa ilitolewa polisi.
Kaimu
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Leonce Ferdinand alithibitisha
kupokea taarifa za mtu mmoja kujeruhiwa na mkuki na uchunguzi
unaendelea.
Wakati hayo yakitokea Morogoro,
wananchi wa Kata ya Ngarenanyuki wilayani Arumeru mkoani Arusha,
wamepinga kitendo cha baadhi ya wanasiasa kuweka mashada ya maua kwenye
kaburi la Naftari Ndekirwa, aliyekuwa diwani wa kata hiyo aliyefariki
kwa ajali ya kuangukiwa na mti.
Mkazi
wa Kijiji cha Olkung’wado, Anael Naftari alisema kitendo cha kwenda
kumsalimia mjane na kuweka mashada ya maua baada ya msiba kumalizika
muda mrefu linamzidishia uchungu.
Mkazi
mwingine, Ndekirwa Urasa alisema hayo yanafanyika yakiwa ni mtaji wa
kisiasa ili kupata kura. Katika uchaguzi huo, Chadema kimemsimamisha
Aminiel Mungure kuwania udiwani, huku mgombea wa CCM ni Zacharia Nko.
Katika
maeneo mengine ya kampeni, Mbunge wa Mufindi Kusini, Mendrad Kigola
aliwataka wakazi wa Kata ya Igombavanu kumchagua diwani wa CCM ili
kurahisisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Kigola
alitoa kauli hiyo juzi akimnadi mgombea udiwani wa kata hiyo, Rashid
Mkuvasa ambaye yeye alijinadi kwamba anao uzoefu na kazi hiyo kwa kuwa
amekuwa diwani kwa kipindi cha miaka 10.
No comments:
Post a Comment