![]() |
Mkazi
wa mtaa wa Mageuzi, kata ya Ngokolo, manispaa ya Shinyanga, Ibrahimu
Daniel (42) amemuua mke wake, kwa kushindwa kuhifadhi vizuri kachumbari
na kupika mboga isiyo na kiwango.
Aidha
mauaji hayo yaliyofanyika kwa kumporomoshea kipigo yalifanyika kwa kuwa
alipika chakula kingine wakati kilichobaki mchana kilikuwepo.
Aliyeuawa
ni Stella Ibrahimu (39) na alipigwa baada ya mumewe Daniel kurudi
nyumbani na kuuliza kachumbari ambayo alikula jana yake ndipo mtoto
aliyekuwa akimlea Elizabeth Ibrahimu (13) alipomuonesha, lakini
hakuridhika nayo na kuanza kuuliza maswali kwa nini haikuhifadhiwa
vizuri.
Baadhi
ya waandishi wa habari waliofika eneo la tukio walielezwa na mtoto wa
marehemu, Daniel Ibrahimu (12) kuwa baba yake alipofika nyumbani saa
moja usiku alimkuta yeye akiwa na Elizabeth ndipo alipoanza kumhoji
Eliza akimuuliza kachumbari yake iko wapi.
Daniel
alisema baada ya Eliza kumuonesha baba yake kachumbari hiyo aliyoila na
kuibakisha Jumatatu wiki hii, aliiona imechacha na kuonekana na uchafu,
ndipo alitoka nje na kuchukua fimbo anayoihifadhi juu ya nyumba na
kutaka kuanza kumpiga lakini kabla ya kumpiga mtoto huyo alichoropoka na
kukimbia nje.
Aliendelea
kusimulia kuwa baada ya kukimbia na binti huyo, mama yake ambaye
alikuwa kazini alifika nyumbani wakati huo mfarakano ukiendelea na
alimkuta baba yao akifoka na baada ya kuuliza kuna nini, aliambiwa kwa
nini hakupika mboga yenye kiwango na kwa nini alipika ugali mwingine
wakati kulikuwa na ugali uliobaki mchana.
“Mama
alifika na kuanza kunywa chai lakini baba aliendelea kufoka ndipo mama
alimjibu kwa hasira ndipo alipomuuliza baba uliacha fedha ya matumizi ya
kuweza kupika mboga yenye kiwango, alianza kumpiga baadaye alimpiga na
kikombe na mateke akaanguka ndipo mimi nilikimbia kwa majirani
kuwataarifu mama anapigwa, walikuja na kukuta mama ameanguka chini baba
akiwa anamruka ruka,” alisema Daniel.
Baadhi
ya majirani waliofika katika tukio hilo, Gloria Shija na Retisia
Mashalah, walisema kwa nyakati tofauti kuwa, walikuta baba huyo amefunga
mlango na walipomgongea afungue, alikataa na kusema kuwa kuna kazi
kidogo anaifanya wasubiri, lakini baada ya kuchungulia dirishani
walimuona anampuliza puani na masikioni huku akimmwagia maji ili
azinduke, baada ya kuona hazinduki.
Shija
alisema kuwa waliingia ndani na kumkuta akiwa amemkalisha chini huku
akiwa ameinamisha shingo ambapo walimbeba na kumtoa nje, walijaribu
kummwagia maji tena lakini ilishindikana ndipo walichukua uamuzi wa
kumpeleka hospitalini walifika na kuanza kupimwa, lakini alionekana
tayari alishafariki muda mrefu.
Kwa
mujibu wa majirani, waliporudi nyumbani, mwanaume huyo alionekana
kumtuma mara kwa mara mwanawe wa kiume na wakaingiwa na hofu na kutoa
taarifa polisi ambapo walifika na kuwachukua watoto wawili; Daniel na
Eliza kwa mahojiano.
Shangazi
wa marehemu, Getruda Vitalis alisema ugomvi huo ulikuwa ukitokea mara
kwa mara. Mwenyekiti wa mtaa wa Mageuzi, Emmanuel Sama alisema yeye
alikuwa amelala nyumbani kwake aligongewa mlango na kuambiwa kuna tukio
la mwanamke kupigwa na mume wake na ana hali mbaya ndipo aliamka na
kwenda katika tukio.
Baada ya kuuliza aliambiwa chanzo ni kachumbari iliyobaki jana haikuhifadhiwa vizuri na mtoto waliokuwa wakimlea, Elizabeth.
Kaimu
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Elias Mwita, alithibitisha na
kueleza kuwa mtuhumiwa anashikiliwa na Polisi. Alisema uchunguzi wa
awali katika mwili wa marehemu umeonesha kuwa na jeraha katikati ya
kichwa na waliruhusu usafirishwe kesho wilayani Ngara, Kagera kwa
maziko.
|
January 20, 2017
MUME AMUUA MKEWE KWA KIPIGO KISA KACHUMBARI
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment