WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amesema Serikali imetoa sh. bilioni 2.4 kwa ajili ya kuboresha mradi wa
maji katika mji wa Makambako mkoani Njombe
Ametoa kauli hiyo jana jioni
(Alhamisi, Januari 19, 2017) wakati akizungumza na wananchi katika
uwanja wa Polisi Makambako ulipofanyika mkutano wa hadhara akiwa katika
ziara yake ya kikazi mkoani Njombe.
Waziri Mkuu alisema lengo la
Serikali ni kuhakikisha kila mwananchi anapata maji safi za salama
katika umbali usiozidi mita 400 kama inavyosema sera ya maji.
Hata hivyo aliwataka wananchi
kutofanya shughuli za kijamii katika vyanzo vya maji ili kuvilinda.
Alisema Serikali inatumia fedha nyingi kutafuta maji kwa sababu vyanzo
vingi zimekauka kutokana na shughuli za kibinadamu.
Katika hatua nyingine Waziri Mkuu
alizungumzia suala la madai ya fidia kwa wananchi waliopisha ujenzi wa
kituo cha ukaguzi cha pamoja na soko la kitamaifa katika eneo la
Makambako aliahidi kuwa watalipwa.
“Fidia zenu mtalipwa hivi katibuni
baada ya Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango kukamilisha
taratibu za ulipaji,” alisema. Wananchi hao walilalamikia ucheleweshwaji
wa malipo ya fidia hizo kupitia katika mabango mbalimbali pamoja na
mbunge wa Njombe, Mheshimiwa Deo Sanga.
Serikali imeanzisha eneo la Idofi
lililoko Makambako kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha ukaguzi wa pamoja wa
magari ya mizigo ili kupunguza vikwazo vya kibiashara barabarani kwa
nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Kituo hicho kitakuwa na vituo
vidogo vya Polisi, Uhamiaji, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Maliasili
pamoja na vituo vya mizani.
Awali mbunge wa jimbo la Njombe
Mheshimiwa Sanga alisema moja ya changamoto inayowakabili wakazi wa mji
wa Makambako ni ucheleweshwaji wa malipo ya fidia kwa waliopisha ujenzi
wa kituo hicho hali inayosababisha baadhi yao kwenda kudai fidia hiyo
kwake.
”Mheshimiwa Waziri Mkuu leo na
sisi wananchi wa Makambako tutapona. Baba Majaliwa hawa wananchi wanadai
fidia yao kwa muda mrefu na baadhi yao wamefikia hatua ya kuja kulala
nje ya nyumba yangu wakigoma kuondoka hadi niwape ufafanuzi wa malipo
yao,” alisema.
Mbali na kuwasilisha changamoto
hiyo mbunge huyo pia aliishukuru Serikali ya Awamu ya Tano kwa jitihada
zake za kuboresha maendeleo ya wananchi hususan wakazi wa jimbo la
Njombe.
Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa
Njombe, Bw. Christopher Ole Sendeka alisema Serikali imetenga sh.
bilioni 2.8 kwa ajili ya ujenzi wa daraja la chuma lenye urefu wa mita
95 katika mto Ruhuhu.
Alisema mkataba wa ujenzi wa nguzo
za daraja tayari umesainiwa kati ya mkandarasi wa kampuni ya M/s Lukolo
na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kwa gharama ya sh bilioni
6.17 na muda wa utekelezaji ni miezi 24.
Akizungumzia mapambano dhidi ya
ugonjwa wa ukimwi Bw. Ole Sendeka alisema mkoa unaendelea na kampeni za
upimaji, zilizowezesha watu kufahamu afya zao na kuchukua tahadhari ya
jinsi ya kujikinga na kuepuka maambukizi mapya.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
IJUMAA, JANUARI 20, 2017.
|
January 20, 2017
SERIKALI IMETOA SH. BILIONI 2.4 KUBORESHA MRADI WA MAJI MAKAMBAKO-MAJALIWA
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment