Wanafunzi
wa Shule ya Msingi ya Mtakatifu Therese wakitoa heshima za mwisho mbele
ya jeneza lenye mwili wa mwanafunzi mwenzao Maria Masala wakati wa
ibada ya kuuaga mwili huo iliyofanyika Kanisa Katoliki la Mtakatifu
Therese Ukonga Madafu Dar es Salaam jana.
Jeneza lenye mwili wa mtoto huyo likiombewa kabla ya
kuingizwa kanisani
Wanafunzi wenzake na mtoto huyo wakiwa katika ibada ya kumuaga mwenzao.
Padre aliyekuwa akiendesha ibada hiyo akilinyunyuzia mafuta ya baraka jeneza lenye mwili wa mtoto Maria.
Msemaji wa familia ya ASP Masala akitoa taarifa na historia
fupi ya marehemu Maria.
Baba wa
marehemu, ASP Masala (wa pili kulia aliyevaa shati la kitenge), akiwa na
ndugu zake na waumini waombolezaji katika ibada ya kuuaga mwili wa
mtoto wake kabla ya kuondoka kwenda nyumbani kwao mkoani Rukwa kwa
mazishi.
Padre aliyekuwa akiendesha ibada hiyo akilinyunyuzia mafuta ya baraka jeneza lenye mwili wa mtoto Maria.
Watawa wa Kanisa Katoliki la Mtakatifu Therese wakitoa
heshima za mwisho.
Waombolezaji wakiwa wamejipanga foleni wakati wakienda
kutoa heshima za mwisho.
Waombolezaji wakiwa katika foleni ya kutoa heshima za mwisho.
Mtawa wa kanisa hilo akisaidiwa baada ya kushindwa kuvumilia uchungu wa kuondokewa na mpendwa wake mtoto Maria.
Ngugu yake Maria akisaidiwa baada ya kutoa heshima
zake za mwisho.
Baba ya mtoto huyo ASP Masala akilia kwa uchungu wakati
akitoa heshima zake za mwisho kwa mwanaye.
Waombolezaji wakiwa wamebeba jeneza lenye mwili wa mtoto Maria wakati wakitoka katika kanisa hilo.
Jeneza likiingizwa katika gari tayari kwa safari ya kwenda
mkoani Rukwa kwa mazishi.
Waombolezaji wakiwa wamepigwa na bumbuwazi
kufuati vifo hivyo.
Ni huzuni na simanzi wakati wa kuuaga mwili wa mtoto huyo.
Na Dotto Mwaibale
WINGU
zito vilio majonzi na simanzi vilitanda kutokana na vifo vya watoto
wawili wa maofisa wa Jeshi la Magereza waliofariki dunia kwa kukosa
hewa baada ya kujifungia kwenye gari la mmoja wa wazazi wao walimokuwa
wakicheza.
Tukio
hilo limetokea juzi jioni katika Kota za Magereza Ukonga jijini Dar es
Salaam, wakati wazazi wao walipokuwa wakitengeneza gari hilo lililogoma
kuwaka.
Watoto
waliopoteza maisha ni mtoto wa Mrakibu wa Jeshi la Magereza (ASP),
Demetrus Masala, aitwaye Maria (6), ambaye alikuwa darasa la kwanza
katika Shule ya Mtakatifu Therese Ukonga na Sajini Francis, ambaye ni
Esther (4), mwanafunzi wa shule ya awali katika eneo hilo.
Kwa
mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo ambao hawakupenda majina yao yaandikwe
kwenye vyombo vya habari kwa sababu si wasemaji wa familia walidai kuwa
watoto hao walipoteza maisha katika gari lenye namba ya usajili T 291
CXR aina ya Toyota Passo ,mali ya ASP Masala.
Mashuhuda
hao walidai kuwa siku ya tukio gari hilo liligoma kuwaka na ndipo
Masala alipokwenda kumuomba jirani yake ambaye anaishi mlango wa pili
Sajini Francis aende kumsaidia kulibusti ambapo alichukua betri katika
gari yake ili amsaidie jirani yake huyo.
Ilielezwa
kuwa licha ya kuibusti betri ya gari la ASP Masala haikupokea moto
ikiashiria kuwa Alternator ilikuwa ni mbovu kwani ilikuwa haifui umeme.
Baada ya
kushindikana kuiwasha gari hilo waliamua kuachana nalo na kushauriana
ASP Masala aende kumfuata fundi na ndipo alipolifunga gari lake na
kuondoka pasipo kujua watoto wao walikuwa ndani ya gari hilo kwani
walipokuwa wakilitengeneza walionekana wakiwa pembeni yake.
Wazazi
hao hawakujua watoto hao waliingia saa ngapi ndani ya gari hilo lakini
ilidaiwa kuwa awali wakati wakicheza jirani na gari hilo waliwafukuza
ambapo baadae waliingia tena bila ya wao kufahamu hasa kutokana na gari
hilo kuwa na vioo vya giza isipokuwa cha mbele ambapo walikuwemo ndani
ya gari hilo kuanzia saa 7 mchana hadi saa 11 jioni.
Ilidaiwa
kuwa baada ya kukaa kwa muda mrefu Francis ambaye ni dereva ofisi ya
Mwanasheria Mkuu wa Serikali alibaini watoto hao wawili hawaonekani
katika eneo hilo ndipo walipoanza kuwatafuta katika nyumba za jirani
bila mafanikio.
Inadaiwa
wakati wakiendelea kuwatafuta kuna kijana aliwadokeza kuwa wakati gari
hilo likiendelea kutengenezwa watoto hao walikuwa ndani ya gari hilo.
Kauli
hiyo inadaiwa ndiyo iliyomshtua Francis na kuamua kuchungulia ndani ya
gari hilo ambapo waliwaona watoto hao wakiwa wamekaa siti ya nyuma
wamelala fofofo huku mwingine akivuja damu puani.
Hali hiyo
ilisababisha Francis na watu wengine waliokuwepo eneo hilo kusogea na
kuvunja kioo kidogo cha gari hilo na kuwatoa watoto hao wakiwa katika
hali mbaya.
Imedaiwa
kwa sababu ya hali waliyokuwa nayo waliamua kuwakimbiza katika Hospitali
ya Kardinal Rugambwa Ukonga kwa ajili ya matibabu ya haraka lakini hata
hivyo walibaini mtoto Maria tayari alikuwa amekwisha fariki dunia.
Madaktari
walijaribu kumpa huduma ya kwanza mtoto Esther kwa kumuongezea Oksjeni
na baadaye walimkimbiza Hospitali ya Mkoa wa Ilala ya Amana ambapo naye
walibaini kuwa tayari alikuwa amekwisha fariki.
Baadhi ya
waumini wa Kanisa Katoliki la Ukonga la Mtakatifu Therese wakizungumza
na wanahabari walielezea kusikitishwa na tukio hilo, wakidai mtoto Maria
juzi asubuhi walishiriki naye Jumuiya ya Mtakatifu Maria Consolata
ambayo ilifanyika nyumbani kwao.
Walisema kwa nyakati tofauti mtoto huyo alishiriki na wazazi wake kupanga viti tayari kwa maandalizi ya jumuiya.
Mkazi mmoja wa eneo hilo alidai, kifo cha watoto hao ni pigo kwa wazazi hao ambao ni majirani na marafiki wa muda mrefu.
Imedaiwa
kuwa wazazi hao kila mmoja alikuwa na watoto wawili, wa kwanza wote
wakiume na wapili wa kike ambao ndio waliofariki katika tukio hilo la
kusikitisha.
“ Kifo
hiki kimeacha pengo kwani wote wameondokewa na watoto wao wa pili
kuzaliwa na wote ni wa kike wamebaki wakiume tu…inauma sana na ni funzo
kwetu kuwa tayari wakati wowote,” ilielezwa.
Mwili wa mtoto Maria ulisafirishwa jana kwenda mkoani Rukwa kwa mazishi ambayo yanatarajia kufanyika kesho.
Hata
hivyo inadaiwa mama mzazi wa Maria hayupo jijini Dar es Salaam alisafiri
kwenda Rukwa kwa ajili ya sherehe za mwisho wa mwaka na bado yupo huko.
Familia ya Francis inatarajia kufanya mazishi ya mtoto wao Esther leo katika Makaburi ya Segerea, Ukonga.
Padre
aliyeongoza ibada ya kuuaga mwili wa mtoto Maria aliwataka wazazi na
waumini wa kanisa Katoliki la Mtakatifu Therese kutohusisha tukio hilo
na imani potofu na kusema kila binadamu anakuja duniani kwa mpango wa
mungu na kuondoka kwa mpango wa mungu ingawa vifo vya watoto hao ni
vyakusikitisha hasa ukizingatia umri wao mdogo waliokuwa nao na kuwa
kazi ya mungu haina makosa.
Akizungumzia
tukio hilo, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mwembe Madafu, Deus
Nchimbi alisema, kifo cha watoto hao ni pigo kwa familia hizo marafiki.
“Kikubwa
ni kuomba amani na kuwaombea marehemu lakini watoto wamekufa kifo cha
uchungu kwa kukosa hewa huenda wangekuwa na wakubwa wangeweza kufungua
gari,”alisema Nchimbi.
Alisema
kilichobaki ni kuikumbusha jamii kuwa makini na vyombo vya moto na
kuwapa uhuru watoto waweze kufahamu aina ya mali zilizopo nyumbani.
Changamoto
kubwa iliyoibuka katika tukio hilo ni kwa wazazi wote wa pande mbili
kugoma kulizungumzia tukio hilo kwa waandishi wa habari kwa madai kuwa
wanaopaswa kulizungumzia ni Jeshi la Magereza wakati suala hilo ni la
kifamilia zaidi na linagusa maisha ya kijamii.
“Tumepewa
maagizo kutoka juu kuwa waandishi wa habari hampaswi kuchukua taarifa
hii kwani ndugu za marehemu bado wanamajonzi hivyo subirini wakisha zika
mje kuwahoji wafiwa hayo ndiyo maagizo na jeshini hatuna kauli nyingi
ni moja tu” alisema ofisa mmoja wa jeshi hilo ambaye hakujitambulisha
jina lake.
No comments:
Post a Comment