Waziri
wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi Dkt. Charles Tizeba amelazimika kutoa
ufafanuzi kuhusu hali ya chakula nchini huku akisisitiza kuwa Tanzania
ina chakula cha kutosha na haina njaa kabisa.
Dkt.
Tizeba ametoa ufafanuzi huo leo wakati akiongea na waandishi wa habari,
na kusema kuwa watu wanaoneza taarifa za kuwepo kwa njaa Tanzania wana
lengo la kuingiza mahindi yao yasiyo na ubora ili wafanye biashara,
jambo ambalo serikali imelikataa.
Akizungumzia
uhalisia wa hali, amesema kilichotokea ni kupanda kwa bei ya mahindi,
hali iliyosababishwa na uamuzi wa serikali kuuza nafaka hiyo katika
mataifa jirani yaliyokuwa na uhitaji mkubwa, ingawa kiwango kilichouzwa
kilikuwa ni sehemu ya mahindi ya ziada.
"Mwaka
jana gunia la mahindi kwa bei ya wastani wa kitaifa ilikuwa 65,000
lakini sasa ni 85,000 na wala haijafikia mara mbili mara tatu kama
inavyosemwa ingawa kuna maeneo kama rorya imefikia hadi 150,000 kutokana
na wao kutegemea misimu miwili wakajikuta wanatumia akiba yao lakini
hali ya hewa ikawa tofauti kwahiyo kuna wafanyabishara wakaamua kutumia
hiyo fursa kupandisha bei zaidi" Amesema.
Ameendelea kusema ..... "Mavuno
ya nafaka yalikuwa tani milioni 16 wakati mahitaji yakiwa tani milioni
13 kwahiyo ziada ilikuwa tani milioni 3, kwahiyo katika hiyo ziada
milioni 1.5 ikasafirishwa nje, wenzetu walikuwa wananunua kwa gharama
yoyote kwa kuwa walikuwa na shida, hiyo ndiyo maana bei ya nafaka
imepanda sana hasa mahindi, kwa sasa bei imefika hadi mia 8 mia 9 na
wauzaji ni walewale, kwahiyo hawezi kuuza ndani kwa bei ya chini lakini
kupanda huko kulitarajiwa"
Amesema
kupanda bei kwa mahindi kulitarajiwa na ni kwa kawaida na wala hakuwezi
kumaanisha kuwa Tanzania kuna njaa wakati nafaka zote zinapatikana kila
kona ya Tanzania
"Hakuna
soko halina mahindi, hakuna soko halina mchele, hakuna soko halina
maharage, masoko ya mijini yamejaa viazi..... nchi ina ziada tani
milioni 3 kwanini mnataka tukanunue tena tani milioni 1 za nini?"
Kuhusu
ukame, amesema ni kweli kuna hali ya upungufu wa mvua, na hiyo
inafahamika maana ilishatabiriwa na kuwataka wananchi watunze akiba yao
ya chakula na wasidanganyike kukiuza, kwa sababu hali ya hewa haitakuwa
nzuri katika baadhi ya maeneo.
Amewasihi
wananchi waache tamaduni ya kung'ang'ania chakula cha aina moja na
kuwataka kutumia mchele na viazi kama wanaona mahindi yamepanda bei.. "Nafaka siyo mahindi tu, tunao mchele na mpunga wa kutosha, na viazi vipo kutoka Tunduma, watumie hivyo"
Waziri
huyo amepiga marufuku mtu yoyote kutoa taarifa za njaa kwa kuwa
serikali ndiyo inayojua hali ya chakula kupitia vyanzo vyake.
No comments:
Post a Comment