KWA MAONI AU USHAURI E-mail: inocomm2014@gmail.com, PIGA SIMU: 0714555668

www.utt-pid.org


TEMBELEA: www.utt-pid.org

February 8, 2017

MBUNGE AMVAA MAKONDA KUHUSU UTAJIRI WA MALI ALIOUPATA NDANI YA KIPINDI KIFUPI....ATAKA VYOMBO VYA DOLA VIMCHUNGUZE

MBUNGE wa Geita Vijijini (CCM), Joseph Msukuma, amemlipua bungeni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kwa kudai kuwa anastahili kuchunguzwa kutokana na mali kibao anazomiliki ndani ya kipindi kifupi ikiwamo jengo la ghorofa, viwanja na magari ya kifahari.

Akizungumza bungeni jana, mbunge huyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM katika Mkoa wa Geita, alisema Makonda hakuwa na utajiri alio nao sasa mwaka 2015, na hivyo akataka achunguzwe ni kwa namna gani amebadilika ghafla baada ya kushika nafasi za ukuu wa wilaya na baadaye ukuu wa mkoa, huku akisisitiza kuwa yeye yuko tayari kuvisaidia vyombo vya dola kuonyesha utajiri aliojilimbikizia mkuu huyo ndani ya kipindi kifupi.

Alitaja sababu nyingine za kumchunguza Makonda kuwa ni pamoja na kufanya ukarabati ofisi yake kwa Sh. milioni 400 na pia akayataja magari ya kifahari anayomiliki katika kipindi hicho kifupi kuwa ni pamoja na la aina ya Lexus alilodai lina thamani ya Sh. milioni 400 na lingine la thamani kubwa alilolitaja kuwa ni V8.

Aliposimama bungeni, Msukuma ambaye kabla ya jana alishagusia tuhuma dhidi ya Makonda kwa kuzungumzia safari alizokwenda Marekani, Dubai na Jiji la Paris nchini Ufaransa, jana alianza kwa kuomba mwongozo kwa Spika akitumia kanuni ya 68(7), akisema anashangaa ni kwa namna gani mawaziri wanaosimamia masuala ya utawala bora wamepigwa ganzi kiasi cha kushindwa kushughulika na Makonda na kumsubiri Rais.

“Mheshimiwa Spika, nasimama kwa kanuni ya 68(7) kuhusu jambo lililojitokeza jana (juzi) wakati wa mjadala wa Bunge…naomba mwongozo wako.

"Mimi binafsi naunga mkono jitihada za Rais kukamata wauza dawa za kulevya, lakini dalili ya kwanza ya kuanza kumhisi mtu kama anajishughulisha na biashara ambazo hazieleweki, kwanza ni mwenendo wa mtu yeyote…siyo mbunge wala siyo nani,” alisema Musukuma.

Alisema mkuu huyo wa mkoa, mwaka 2015 alikuwa akiishi kwa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje, Bernard Membe, lakini sasa wakati amekuwa Mkuu wa Mkoa, anatumia magari ya kifahari, ana jengo la ghorofa Mwanza na pia anamiliki viwanja maeneo mbalimbali.

“Anatumia Lexus ya petroli ya Sh. milioni 400, lakini imekarabatiwa ofisi (yake) ya RC Dar es Salaam kwa zaidi ya Sh. milioni 400 bila kufuata utaratibu wa manunuzi wa serikali.

“Ana ma-V8 na Mwanza amejenga jengo la ghorofa…ni kina nani wanaotakiwa kujadiliwa na kufanyiwa uchunguzi?” Alidai Musukuma kabla ya kuongeza:

“Na hawa mawaziri tulionao humu, kwa nini wamepigwa ganzi? Utawala bora, Mambo ya Ndani na Waziri wa Sheria…kwa nini mmepigwa ganzi?”

Musukuma aliongeza: “Kwa nini mmepigwa ganzi? Mnalifanya suala hili ni la Rais, kuanza kuhangaika na Mkuu wa Mkoa…na hata kama anachangiwa na wahisani, Sheria ya Maadili inatutaka anayekuchangia umtangaze.Lini amemtangaza aliyemchangia fedha?”

Musukuma alisema anaomba mwongozo kama wengine wanafanya mambo ya ovyo na wanakuwa na kinga na mawaziri wakapigwa ganzi na hawataki kufuatilia.

“Tunataka RC achunguzwe mali zake alizonazo… kwa mwaka mmoja huwezi kumiliki magari ya kifahari, ukajenga Mwanza, ukaenda Marekani, ukanunua maviwanja.

"Wala siyo suala la kuogopa. Mimi nasema nipo tayari kuwasaidia mawaziri na vyombo vya usalama tuwaonyeshe,” alisema Musukuma.

Msukuma ametoa kauli hizo ukiwa ni mwendelezo wa kumtuhumu Makonda baada ya kufanya hivyo bungeni juzi aliposema anashangaa kuona Taifa linaifanyia kazi taarifa ya mkuu huyo wa mkoa juu ya wauza dawa za kulevya, wakati mawaziri wa zamani wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe na Charles Kitwanga, wamewahi kusema wana orodha ya watu wanaouza dawa za kulevya na hakuna hatua zilizochukuliwa.

“Wauza dawa za kulevya wanajulikana na hata walio mstari wa mbele kukamata wenzao wanashinda nao na kuwasafirisha nchi mbalimbali kama Marekani.

“Kwanini vyombo vya ulinzi na usalama visimchunguze Makonda maana anasafiri sana Ulaya, Ufaransa na Dubai, hivi anasafiri kwa mshahara upi alionao?

“Tunaambiwa juu ya vita ya kupambana na dawa za kulevya halafu tunawakamata akina Ray C na Chidi Benz wakati hao ni wagonjwa.

“Kama Rais Magufuli amesema kama mkewe Mama Janet anahusika na dawa za kulevya akamatwe, kwanini Makonda naye asihojiwe kwa sababu amewapangisha watu nyumba wakati wanajihusisha na dawa za kulevya?” alisema Msukuma. 

Hivi karibuni, Makonda aliongoza kasi katika vita dhidi ya dawa za kulevya kwa kuamuru watu kadhaa wanaodaiwa kujihusisha na dawa hizo jijini Dar es Salaam waripoti polisi wakiwamo wasanii Wema Sepetu, Khalid Mohamed ‘TID’, Dogo Hamidu na Tunda.

Aidha, aliwataja askari polisi kadhaa wanaohusishwa pia na dawa za kulevya akiwamo aliyewahi kuwa Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Christopher Fuime. Askari hao walisimamishwa kazi na Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Ernest Mangu, ili kupisha uchunguzi wa kina dhidi yao kuhusiana na tuhuma alizoziibua Makonda.

Ufafanuzi wa Naibu Spika
Akifafanua mwongozo huo, Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson, alisema Mbunge huyo amezungumza jambo ambalo ni kinyume cha kanuni za chombo hicho cha kutunga sheria.

“Mheshimiwa Mbunge, umetoa maelezo mengi siwezi kuyarejea hapa…maana nitakuwa kama natoa msisitizo, jambo ambalo kanuni zetu zinakataza, kwa maana mambo aliyoyataja, yule mtu aliyemtaja na wengine waliohusika, kama jambo alilolisema si sahihi, wanaweza kuja bungeni,” alisema Dk. Tulia.

Naibu Spika huyo alisema kwa mujibu wa kanuni ya 68 (7), mwongozo unatakiwa kuombwa kwa jambo lililotokea bungeni mapema na kwamba, kama ni jambo la juzi, atumie kanuni nyingine kuleta hoja yake.

No comments:

Post a Comment