Na: Lilian Lundo – MAELEZO – Dodoma
Serikali inatarajia kupiga
marufuku utengenezaji na uingizaji wa pombe za bei rahisi maarufu kama
“Viroba” Nchini, ndani ya miezi mitatu ijayo.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Hamisi Kigwangalla ameyasema hayo
leo Bungeni, Mjini Dodoma alipokuwa akijibu hoja za wabunge waliokuwa
wakilalamikia kilevi hicho kinavyopunguza nguvu kazi ya Taifa, wakati
wa uwasilishwaji wa taarifa za kamati ya kudumu ya Bunge ya masuala ya
Ukimwi pamoja na Huduma na Maendeleo ya Jamii kwa mwaka 2016/17.
Dkt. Kigwangalla amesema kuwa
baada ya miezi mitatu kilevi hicho kitapigwa marufuku kutengenezwa au
kuingizwa nchini pamoja na kuziba mianya yote ya uingizaji wa kilevi
hicho ambacho kimekuwa kikitumiwa na vijana wengi, hivyo kuharibu nguvu
kazi ya Taifa.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la
Tarime Mjini Esther Matiko amesema kwamba pombe hiyo inasababisha vifo
vya vijana wengi nchini ambao ndio tegemeo kubwa na nguvu kazi ya Taifa.
“Katika kipindi hiki kifupi cha
likizo yangu, nilikuwa jimboni kwangu na tumezika vijana wanne ambao
wamefariki kutokana na matumizi ya viroba. Hivyo wananchi wa jimbo langu
wameniagiza kuja kulieleza Bunge athari za pombe hiyo ili tuweze
kujadili na kuona namna gani ya kuliokoa Taifa hasa vijana kutoka
katika janga hilo,” alifafanua Matiko.
Akiwasilisha taarifa ya Kamati,
Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile amesema kuwa
Kamati imebaini uwepo wa uhusiano mkubwa kati ya matumizi ya pombe hizo
na kuongezeka kwa tabia hatarishi zinazochangia ongezeko la vijana
katika matumizi ya dawa za kulevya.
Aidha amesema kuwa hali hiyo
inaathiri ufanisi wa nguvu kazi ya Taifa kutokana na madhara ya matumizi
ya dawa za kulevya. Hivyo Kamati imeishauri Serikali kufungia kabisa
uzalishaji na uuzwaji wa pombe hizo za viroba ili kulinusuru Taifa.
|
February 7, 2017
SERIKALI KUPIGA MARUFUKU MATUMIZI YA POMBE AINA YA VIROBA NCHINI
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment