Kampuni
ya Acacia imesema ripoti kuhusu mchanga wa dhahabu aliyopewa Rais John
Magufuli Jumatano ya wiki hii imejaa upotoshaji wa hali ya juu na
imependekeza kufanyika kwa uchunguzi mpya ambao ni huru ili kuweza
kupata ukweli.
Katika
taarifa yake ya jana, Kampuni ya Acacia, yenye makao makuu jijini
London, Uingereza, imesema kwamba, imejaribu mara kadhaa kuomba nakala
ya ripoti hiyo nzima pamoja na utaratibu wa kuchukua sampuli kwenye
uchunguzi huo, lakini mpaka sasa haijapewa.
“Kwa
kuzingatia data tulizo nazo kwa zaidi ya miaka 20 ambazo tunaweza
kuzitoa kwa ajili ya uchunguzi zaidi, hatuwezi kukubaliana na matokeo ya
Tume. Data hizi ni data ambazo zimechambuliwa na kuandaliwa na
Watanzania, wataalamu pamoja na taasisi za kimataifa na zimekuja na
matokeo yanayofanana.
“Data
hizi huru ambazo zinaweza kuthibitika zimeonyesha kuwa dhahabu kwenye
mchanga ni chini ya asilimia moja ya kumi ya kiwango ambacho kimetajwa
na ripoti ya tume. Kama data za ripoti ya tume zingekuwa kweli,
Bulyanhulu na Buzwagi zingekuwa ndiyo wazalishaji wakubwa wa dhahabu
duniani. Kutokana na upotoshaji huu, tunaamini tathmini mpya ambayo ni
huru inahitajika,” inasomeka sehema ya Acacia kwa umma.
Zaidi
ripoti hiyo inaeleza kuwa, Acacia imekuwa ikilipa mrahaba ambao ni
asilimia 4 kwa mujibu wa makubaliano kati yake na Serikali pamoja na
sheria za Tanzania na kuongeza kuwa, pamoja na kuwa kweli kuna baadhi ya
aina nyingine za madini kama chuma, sulphur, rhodium na mengineyo
kwenye mchanga, aina hizo hazina thamani kibiashara na kampuni hiyo
haipati mapato yoyote kutokana nayo.
Kampuni
hiyo imesisitiza kuwa, imekuwa ikilipa mrahaba kwa mujibu wa sheria kwa
madini wanayoyazalisha na kusema kuwa, katazo hilo la kusafirisha
mchanga kutoka migodi hiyo miwili inaifanya kampuni hiyo kupoteza zaidi
ya shilingi bilioni 2.2 kila siku, huku ikisisitiza itachukua hatua zote
kuhakikisha haiendelei kupata hasara.
Taarifa
hiyo ya jana imekuja zikiwa zimepita siku mbili baada ya kampuni hiyo
kutoa taarifa nyingine ya kukosoa ripoti ya uchunguzi wa makinikia
ambayo imewasilishwa kwa Rais.
Kupitia
taarifa hiyo, Acacia ilidai kuwa, haijaona nakala ya ripoti hiyo ambayo
inaonyesha kuwa kiwango cha madini kilichopo kwenye makinikia
yanayoshikiliwa katika Bandari ya Dar es Salaam ni mara kumi zaidi ya
kiwango kilichoainishwa kwenye data zilizowasilishwa awali.
Kwa msingi huo, uongozi wa Acacia ulisema kuwa unaendelea kusubiri nakala zaidi za ripoti hiyo kwa ajili ya kutolea ufafanuzi.
No comments:
Post a Comment