Na. Immaculate Makilika- MAELEZO
- Awataka watanzania kumsaidia katika vita hiyo
Mtafiti wa masuala ya Uchumi na
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Dkt.Haji Semboja anasema kuwa
amefurahishwa na ripoti ya Kamati Maalum iliyoteuliwa na Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania John Pombe Magufuli ya kuchunguza mchanga wa
madini kwenye makontena 277 yaliyozuiwa na serikali kusafirishwa kwenda
nje kwaajili ya uchenjuaji.
Akizungumza Jijini Dar es Salaam
katika mahojiano na mwandishi wa habari hii, Dkt.Semboja alisema kuwa,
hatua hiyo ni nzuri na ya kuridhisha kwa vile Rais Magufuli amefanyia
kazi suala hilo ambalo limekua likizungumzwa kwa muda mrefu na baadhi ya
wasomi,wanaharakati na hata wanasiasa hapa nchini.
“Mimi ni kati ya Watanzania
waliofurahishwa na maamuzi ya Rais, nina furaha kubwa hasa ukizingatia
niliwahi kushiriki katika uandaaji wa sera za madini na uwekezaji, na ni
wazi kuwa tumekuwa tukiibiwa kwa kiwango kikubwa katika sekta ya
madini” alisema Dkt.Semboja.
Malalamiko haya ya wizi na
utoroshaji wa madini yamekuwepo kwa muda mrefu, kitu ambacho tulikua
tukizungumza sasa kimethibitishwa , baada ya Rais Magufuli kupokea
ripoti hiyo ya mchanga”, aliongeza Dkt.Semboja.
Aidha, Dkt.Semboja amemshauri
Rais Magufuli kuendelea kuwatumia wataalamu mbalimbali waliopo nchini
na kuiomba Serikali iwe na utaratibu wa kuwatumia watu wake ambao wengi
ni wazalendo na wana uchungu na nchi yao.
Pia ameishauri Serikali kuzipitia
upya Sheria, Sera na mikataba inayohusu madini pamoja na kuzisimamia
vyema taasisi zilizowekwa kushughulikia sekta ya madini, ikiwa ni
pamoja na nchi kujijengea uwezo wa kuchenjua madini bila kuwepo kwa
ulazima wa kupeleka mchanga nje ya nchi. Pia ameishauri serikali kuweka
mikakati ya kuyaongezea thamani madini ili yauzwe hapahapa nchini
tofauti na ilivyo sasa ambapo serikali inategemea kuchukua kodi tu na
mrabaha.
“Tanzania inapoteza kiasi cha
Tsh. Bilioni 829.4 hadi Trilioni 1.439 kwa kusafirisha mchanga nje ya
nchi,hivyo ni vyema tukasimamia sekta ya madini kikamilifu kwani
kiuchumi inaweza kututoa hapa tulipo na kutuletea maendeleo
tunayoyataka”, alisema Dkt.Semboja.
Naye Mtendaji Mkuu wa Shirikisho
la Vyama vya wachimba Madini Wadogowadogo Tanzania (FEMATA), Haruni
Kinega alisema kuwa wamefurahishwa na wanampongeza Rais Magufuli kwa
hatua ya kusitisha usafirishaji wa mchanga wa madini kwa vile kuna
faida kubwa kutokana na kutosafirishwa kwa mchanga huo.
“Hii ni fursa na faida kwa wadau
na wafanyabiashara wa sekta ya madini kuleta mashine za uchenjuaji wa
madini pamoja na kuwezesha shughuli za uchakataji wa madini kufanyika
hapa nchini”, alisema Bw.Kinega.
Pia Bw. Kinega alieleza kuwa kuna
baadhi ya viwanda vyenye uwezo wa kufanya uchakataji wa madini hapa
nchini lakini vinakosa malighafi ya kutosha na hivyo vinajiedesha kwa
hasara na kuyalazimu makampuni kupeleka mchanga nje ya nchi.
Aidha Bw.Kinega alisema FEMATA
itaendelea kuunga mkono juhudi za Rais Magufuli za kuhakikisha
watanzania wananufaika na raslimali zilizopo nchini na kuzitaka kampuni
zinazofanya shughuli za madini nchini kuwa wawazi na kufuata sheria za
nchi.
Kwa upande wake, Idrisa Kaloli
mkazi wa Jiji la Dar es Salaam, alisema kuwa ripoti ya mchanga wa madini
ina manufaa kwa umma kwa vile imesaidia kudhibiti mianya ya uvujaji wa
raslimali za Watanzania, kwani fedha zote ambazo zingepotea kwenye
madini yaliyokuwa yasafirishwe zitasaidia kuleta maendeleo ya Watanzania
kama kujenga barabara, mashule, hospitali na hata kununulia madawa na
vifaa tiba.
Alisema nchi yetu inautajiri wa
kutosha wa rasilimali hivyo ni vyema zikasimamiwa kikamilifu ili ziwweze
kuunufaisha umma wa watanzania na sio watu wachache wenye uchu wa
utajiri.
No comments:
Post a Comment